Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Michuano ya Euro 2024 itakavyowaweka sokoni mastaa hawa

Joshua Kimmich Joshua Kimmich

Sat, 15 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Michuano mikubwa ni fursa adhimu kwa mchezaji kujiweka sokoni hasa ukizingatia mikikimikiki hiyo inafanyika wakati wa dirisha la usajili wa wachezaji likiwa wazi.

Na mikikimikiki ya Euro 2024 haina tofauti na michuano mingine mikubwa, kwamba itakuwa mahala mwafaka kwa wanasoka kufurahia, kuonyeshwa viwango vyao na hatimaye kunaswa na timu nyingine zitakazonogewa zaidi.

Kwa mfano, kiungo Enzo Fernandez alipata dili la kuhamia Chelsea baada ya staa huyo kufanya vizuri kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 alipokuwa na kikosi cha Argentina kwenye michuano hiyo iliyofanyika Qatar.

Ukizungumzia michuano ya Euro, Andrey Arshavin alijiweka sokoni na kusakwa na timu kibao za Ulaya baada ya kufanya vizuri akiwa na Russia kwenye fainali za Euro 2008 na hapo akanaswa na Arsenal.

Renato Sanches aliikamata dunia ya soka wakati aliposaidia Ureno kufanya kweli kwenye Euro 2016 baada ya hapo, akanasa dili la kwenda kujiunga na Bayern Munich.

Katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi huko Ulaya, fainali za Ujerumani zitakuwa nafasi muhimu kwa baadhi ya wachezaji kujiweka sokoni na kutafuta timu nyingine za kucheza baada ya michuano ya Euro 2024.

Kuna baadhi ya wachezaji ni maarufu na vipaji vyao vinafahamika, lakini wapo kwenye nyakati ngumu kwenye timu zao za sasa, hivyo watahitaji kutumia jukwaa la fainali za Euro 2024 kutafuta timu nyingine za kuwasajili kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.

Hawa hapa mastaa ambao fainali za Euro 2024 zinaweza kufungua fursa kwao za kujiweka sokoni na msimu ujao wakawa kwenye timu mpya.

Joshua Kimmich

Kiraka huyo mwenye uwezo wa kucheza beki na kiungo, Kimmich atakuwa kwenye kikosi cha Ujerumani chenye matumaini ya kufanya vizuri kutokana na fainali hizo za Euro 2024 kufanyika kwenye ardhi yao. Kimmich ameshinda mataji karibu yote akiwa na Bayern Munich, akinyakua Bundesliga na Champions Leagues - lakini mkataba wake unaelekea ukingoni huko Allianz Arena.

Baada ya Bayern kuwa na wakati mgumu msimu uliopita, Kimmich ameripotiwa kuwa mmoja wa wachezaji huenda wakaachana na timu hiyo ya Allianz Arena. Barcelona ilipeleka ofa ya kumsajili, ikagomewa na mabosi wa Bayern. Lakini, kwa sasa Manchester City ya kocha wake wa zamani, Pep Guardiola inahitaji saini yake na huenda ikafanya mchakato wa kumsajili baada ya kukamilika kwa fainali za Euro 2024.

Martin Zubimendi

Real Sociedad imetengeneza kipaji kingine matata kabisa kupitia kwa kiungo wao fundi wa mpira, ambaye amekuwa kwenye rada za makocha wengi wakihitaji huduma zake, Martin Zubimendi. Na kinachoelezwa ni kwamba hata kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wake kinachotaja bei anayoweza kuuzwa mchezaji huyo si kubwa sana kiasi cha kutishia dili hilo lisifanyike kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Zubimendi aliisaidia Sociedad kufika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Na sasa yupo kwenye kikosi cha Hispania kilichopo kwenye fainali za Euro 2024 na bila shaka, kutamba kwenye fainali hizo zitampa dili la kunasa katika dirisha hili. Arsenal inahitaji saini yake kwa ajili ya kwenda kuboresha safu yao ya kiungo yenye wakali matata kabisa kama Martin Odegaard na Declan Rice.

Goncalo Inacio

Beki huyo kinda ameonyesha kiwango bora sana akiwa na kikosi cha Sporting Lisbon na hivyo kupata nafasi ya kuwapo kwenye timu ya Ureno iliyokwenda kwenye fainali za Euro 2024. Uwepo wa mchezaji kama Inacio kwenye kikosi cha Ureno unafanya timu hiyo kupewa nafasi kubwa pia ya kufanya vizuri kwenye fainali hizo. Bei anayouzwa Inacio kulingana na kipengele kilichopo kwenye mkataba wake unazifanya klabu za Manchester United na Liverpool kupigana vikumbo kuhitaji saini yake.

Kutokana na hilo, beki huyo mwenye umri wa miaka 22, atavutia timu nyingine na kupambana kumsajili kwenye dirisha hili kama atafanya vyema kwenye fainali za Euro 2024. Mwanzoni Inacio alianza kucheza kama beki wa kati, lakini baadaye alihamishiwa kwenye beki ya kushoto, ambako ameonyesha ubora mkubwa.

Youssouf Fofana

Staa huyo wa Monaco anatazamwa kwa jicho la karibu kuona kama atafanya vyema kwenye kikosi cha Ufaransa katika fainali hizo za Euro 2024. Mchezaji huyo mwenye ujuzi mkubwa kwenye kukaba, ni kipenzi cha huko Stade Louis II kutokana na ubora wake uwanjani, ambapo amekuwa mzuri pia kwenye kushambulia.

Mkataba wa Fofana huko Monaco unaelekea ukingoni na mchezaji mwenyewe ameweka wazi kwamba yupo tayari kuhamia kwneye timu nyingine kama tu kutakuwa na timu itakayofika bei. Les Blues ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye Euro 2024 na Fofana ni moja ya mastaa wa kizazi kipya wanaotazamwa kwa ukaribu na timu zinazowataka.

Teun Koopmeiners

Wiki chache zimepita tangu aliposhangilia ubingwa wa Europa League akiwa na kikosi cha Atalanta, Koopmeiners kwa sasa atakuwa na majukumu ya kuisaidia timu yake ya Uholanzi kwenye fainali za Euro 2024 huko Ujerumani. Kucheza kwa kiwango kikubwa katika fainali hizo bila shaka kutafungua milango ya kuwindwa na timu nyingine ambacho zimeonyesha nia na dhamira ya kunasa saini yake kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Atalanta ilinasa saini yake kutoka AZ Alkmaar na bila shaka kama kutakuwa na ofa ya kutoka kwa moja ya klabu kubwa kwenye bara hilo la Ulaya, staa huyo hawezi kufunga milango yake ya kwenda kujiunga na na tmu hiyo. Hata hivyo, kiwango cha juu kwenye mikikimikiki ya Euro 2024 itafanya bei yake sokoni kupanda zaidi.

Chanzo: Mwanaspoti