Waholanzi wao wanamwita, Miano van den Bos. Ni kijana wa Kitanzania ambaye siku chache zilizopita alikuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars', ambacho kilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Zanzibar Heroes kwa ajili ya ufunguzi wa Uwanja wa New Amaan Complex ambao unatumika kwenye mashindano ya Mapinduzi Cup.
???????????????????? ???????????????????????? kama ambavyo wengine wanamfahamu, ni miongoni mwa maingizo mapya kwenye kikosi cha Taifa Stars ambacho kipo kambini kwa ajili ya maandalizi ya fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) ambazo zitafanyika mwezi huu huko Ivory Coast.
Wadau na mashabiki mbalimbali wa soka wameonekana kuvutiwa na kiwango chake kwenye mchezo wa kirafiki ambao Kilimanjaro Stars ilitoka suluhu dhidi ya Zanzibar Heroes, ambao alitumika upande wa beki ya kulia. Lakini jamaa ana uwezo pia wa kucheza beki ya kati na hata eneo la kiungo, huku kasi na maarifa aliyonayo ni kati ya mambo ambayo yanaonekana yanaweza kuongeza kitu kwenye kikosi cha Adel Amrouche.
Miano mwenye miaka 20, anacheza soka la kulipwa Hispania akiwa na Villena CF ambayo inashiriki Lliga Comunitat FFCV (Ligi Daraja la Sita), ni kati ya wachezaji watano tu wa kigeni kwenye timu hiyo licha ya kuwa na umri mdogo mabosi wa timu hiyo walivutiwa naye na kumsajili akitokea Uholanzi ambako alikuwa akichezea FC Eindhoven.
Haikuwa kazi nyepesi kwake kufanya uamuzi wa kuondoka Uholanzi tena kwenye klabu kubwa kama FC Eindhoven na kutua Hispania katika timu ya chini ukilinganisha na kule ambapo alitoka lakini imekuwa njia kwake ya kuonekana zaidi na hatimaye kupata nafasi ya kulitumikia taifa la Tanzania katika ngazi ya kimataifa.
Huyu hapa Miano anasimuliwa mambo yalivyokuwa; "Miezi sita iliyopita kwa bahati mbaya ilinibidi kuiaga klabu yangu ya zamani FC Eindhoven. Ingawa ulikuwa uamuzi wa kuumiza mwanzoni, niliamua kuchukua hatua mara moja.
"Chaguo hili lililofikiriwa vyema lilinipa fursa ya kucheza sana na kuzingatia kikamilifu maisha yangu ya soka. Nilichanua, haswa kiakili," anasema.
Kinda huyo anaendelea, "Sasa, miezi sita baadaye, kwa neema ya Mungu nimeweza kuichezea timu ya taifa ya Tanzania kwa mara ya kwanza. Hapo awali ningeweza tu kuwa na ndoto hii. Shukrani zangu za dhati ziwaendee wote waliochangia kuniletea maendeleo, wafanyakazi wa FC Eindhoven, VRS Academy (ambapo bado nafanya kazi), wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania walionipokea kwa upendo na wafanyakazi walionipa nafasi ya kunisaidia."
Miano ambaye mzazi wake mmoja ni Mtanzania huku mwingine akiwa Mholanzi, amezaliwa na kukulia kwenye taifa hilo ambalo wametoka wachezaji wengi wakubwa ambao wametikisa dunia kama vile Johan Cruyff (marehemu), Marco van Basten, Ruud Gullit na Frank Rijkaard.
KLABU YAKE
Baada ya Miano kuitwa Taifa Stars, klabu yake ilitoa taarifa kama ifuatavyo; "Tunayo furaha kutangaza kwamba Miano van den Bos, beki wetu, sasa ni mchezaji wa tatu kujiunga na wachezaji wengine wawili wa kimataifa baada ya miaka 5 katika akademi. Kutoka FC Eindhoven, Miano alikuja kwenye kituo chetu nchini Uhispania Agosti, ambapo juhudi zake za ajabu zilisababisha maendeleo yake makubwa.
"Lengo la Miano ni zaidi ya uteuzi wa awali, anatamani kuwa sehemu muhimu ya Kombe la Dunia la FIFA mwaka wa 2025. Nia yake inaonyesha azimio la akademi yetu la kuendeleza wachezaji ambao sio tu wanafanya vyema uwanjani hadi nje ya uwanja."
Taarifa hiyo haikuishia hapo iliendelea kwa kusema maono ya akademia yao yanatokana na maendeleo kamili ya kiroho na kimwili kama wanasoka, kwa mwongozo wa Mungu. Akademi hiyo inaamini katika kumtengeneza mchezaji kuwa na kipaji kikubwa pamoja na tabia njema, ambayo Miano anatoa mfano wake.
ATABIRIWA MAKUBWA
Ismael Francois ambaye ni kipa anayecheza timu moja na Miano, amemtakia kila la kheri swahiba wake huku akimtabiria kuwa anaweza kufanya vizuri kwenye fainali za Afcon kama atapata nafasi kutokana na ukubwa wa kipaji alichonacho.
"Pamoja na kwamba umri wake ni mdogo lakini tayari ni mchezaji ambaye anaonekana kuwa amekomaa, anaweza kucheza vizuri tu katika nafasi ya beki wa kati au pembeni na akafanya vizuri, sio mchezaji mwenye hasira ambaye unaweza kusema muda wowote ataigharimu timu, ni mtulivu na mwenye akili kubwa ya mpira," anasema.
Ismael ni mchezaji wa kimataifa wa Haiti ambaye naye anajitafuta huko Hispania kama ilivyo kwa Miano huku wakiwa na matumaini kila mmoja ya kupata mafanikio nchini humo.
Villena CF imekuwa na utaratibu wa kutoa wachezaji wake kwa mkopo kwenda klabu mbalimbali kubwa ambazo zimekuwa zikivutiwa nao. Hivi karibuni Guilliendrick Kierindongo aliula kwa kupata nafasi ya kwenda Elche kufanya majaribio.