Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miaka mitano ya Maxime Kagera Sugar

Maxime Pic Data Miaka mitano ya Maxime Kagera Sugar

Sat, 20 Mar 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

HESHIMA. Ndiyo ameondoka na heshima. Ndivyo unaweza kuelezea safari ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime ambaye aliachana na timu hiyo hivi karibuni.

Maxime ambaye alidumu Kagera Sugar kwa miaka mitano licha ya misukosuko kadhaa aliyopitia ndani na nje ya uwanja, lakini Nahodha huyo wa zamani wa Taifa Stars, ameondoka kwa heshima.

Hivi karibuni uongozi wa Kagera Sugar, ulitangaza kuvunja mkataba wa kocha huyo pamoja na wasaidizi wake kwa madai ya kutofurahishwa na matokeo ya timu ambapo nafasi yake imechukuliwa na Francis Baraza kutoka Biashara United.

Mwanaspoti inakuletea changamoto na mafanikio ya kocha huyo ambaye alidumu kwa miaka mitano kabla ya kutimuliwa,

TOP 3 VPL

Related MEDDIE KAGERE: Sijakata tamaa, nitacheza tuMsimu wake wa kwanza kutua klabuni hapo 2016/17, Maxime aliiwezesha Kagera Sugar kumaliza nafasi ya tatu na kuchaguliwa kuwa kocha bora wa msimu huo.

Hatua hiyo iliipa heshima timu na yeye katika medani ya soka nchini kutokana na jinsi alivyoweza kutengeneza timu kwa muda mfupi na kuwafanya wachezaji kucheza soka la ushindani.

Msimu huo ulimfanya kocha huyo kutengeneza wasifu mzuri na kufanya baadhi ya timu kubwa nchini kumuwinda kuhitaji huduma yake ikiwamo Yanga ambao walipambana bila mafanikio.

Hata hivyo kuondoka kwake huenda ikawa pigo kwa wachezaji kutokana na ushirikiano aliokuwa ameuweka na jinsi alivyokuwa akiwatenegeneza kiushindani.

Wachezaji kama Ramadhan Kapera, Awesu Awesu, Christopher Edward, Kassim Khamis, Zawadi Mauya na wengine ni miongoni mwa nyota waliotoka mikononi mwa Kocha huyo.

MSUKOSUKO KWA MASHABIKI

Licha ya kazi nzuri aliyoifanya Maxime, lakini hatasahau kadhia aliyokutana nayo msimu wa 2018/19 aliposhikiwa mabango na mashabiki wakimtaka aachie timu.

Licha ya kwamba viongozi wa timu hiyo walikomaa lakini haikuwa kazi rahisi kwake kuvumilia matusi na kejeli za hapa na pale kwa mashabiki waliomtaka aachie timu.

Msimu huo Kagera Sugar iliponea chupuchupu kushuka daraja baada ya kuangukia kwenye hatua ya mchujo ‘Play Off’ kwa kuifunga Pamba mabao 2-0 mchezo wa mwisho.

Kipindi hicho kilikuwa kigumu kwa Maxime kwani ilimfanya aliyekuwa Mkuu wa jeshi la polisi mkoani humo, Agustino Ollomi kuingilia kati kuzima maandamano ya mashabiki.

Kundi la mashabiki walivamia barabarani majira ya jioni wakati timu ikitoka ugenini kucheza mechi ya Ligi Kuu kwa mabango wakishinikiza kocha huyo aachie timu.

Hata hivyo vyombo vya usalama vilikuwa makini kusambaratisha kundi hilo, pia hata viongozi wa timu waliweza kusimamia walichokiamini kwa kutosikiliza kelele za mashabiki.

Uongozi uliendelea kumuamini kocha huyo kwani msimu uliopita baada kumalizika kwa ligi, uliweza kumpa mkataba wa miaka miwili ikiwa ni njia ya kuzima harakati za Yanga waliokuwa wakimsaka.

Hata hivyo mkataba huo haujamalizika hata mwaka mmoja kwani mapema mwezi Machi ndoa ilivunjwa na sasa timu inanolewa na Francis Baraza raia wa Kenya.

KAITABA NOMA

Pamoja na kuondoka ndani ya timu hiyo, Maxime pia hawezi kusahau ishu ya uwanja wa Kaitaba ambao kwa kiasi kikubwa ulikuwa mgumu kwake kupata matokeo mazuri.

Kagera Sugar haswa msimu uliopita ilicheza mechi sita mfululizo ugenini na kushinda nne na sare mbili lakini iliporudi nyumbani mambo yalikuwa mazito.

Kocha huyo alijikuta katika wakati mgumu na kufikiria kuamua kubadili uwanja, lakini baadaye aliamua kukomaa japokuwa uwanja wa Kaitaba haukuwa rafiki kwake.

Hata hivyo hatua ya kutemwa kikosini pengine ni faida na heshima kubwa kwake kutokana na muda wote huo hakuweza kuishusha timu, hivyo kuendelea kuaminiwa na wadau wa soka nchini.

MSIKIE MAXIME

Kocha huyo mwenye misimamo mikali, anasema hawezi kuzungumza ubaya wowote kwa kipindi chote alichodumu Kagera Sugar kwani amefanya kazi zake kwa uhuru.

Anasema kwa muda wote alipewa ushirikiano na hakuna kitu kilichomfanya kujutia kufanya kazi na taasisi hiyo na kwamba kama kuna jambo baya lilitokea hakumbuki na huenda lilikuwa la kiubinadamu.

“Siwezi kuwasema vibaya, nimefanya kazi kwa uhuru sikuingiliwa na mtu kwenye majukumu yangu, kama ilitokea basi sikumbuki na labda ni mambo ya kibinadamu,” anasema

Kocha huyo anaeleza kuwa kwa sasa yuko huru na kazi yake ni soka hivyo timu yoyote inayohitaji huduma yake yuko tayari na kwamba kwa sasa ameamua kupumzika kidogo nyumbani.

Anafafanua kuwa kwa muda aliotumikia timu hiyo anajivunia kuiacha Ligi Kuu na kwenye mashindano mengine ikiwamo Kombe la Shirikisho (ASFC) licha ya changamoto za matokeo zilizomkuta.

“Ni kweli naweza kusema nimeondoka kwa heshima kwa sababu timu niliikuta Ligi Kuu na nimeiacha palepale, Kagera Sugar bado timu nzuri,” Maxime.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz