Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miaka kumi ya mkasa wa Patrick Muntari na ‘ambulance’ za Azam Complex

Patrick Muntari Df Miaka kumi ya mkasa wa Patrick Muntari na ‘ambulance’ za Azam Complex

Tue, 19 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwenye kanuni za uendeshaji na usimamizi wa ligi kuu, sura ya sita kanuni ya 20, inazungumzia huduma ya kwanza.

Kanuni hii yenye ibara nne, inazungumzia zaidi uwepo wa gari la wagonjwa (Ambulance), uwanjani wakati wa mchezo wa ligi kuu.

Kanuni ilitungwa mwaka 2013, kabla ya kuanza kwa msimu wa 2013/14 kufuatia mkasa mkubwa uliotokea Oktoba 28, 2012, kwenye mchezo wa JKT Ruvu Stars (sasa JKT Tanzania) dhidi ya Coastal Union, Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Dakika ya 66 ya mchezo, mshambuliaji wa Coastal Union, Nsa Job Mahinya, aliumizwa vibaya na kipa wa JKT Ruvu Stars, Patrick Muntari.

Bahati mbaya uwanjani hakukuwa na gari la wagonjwa, ikabidi Nsa Job apelekwe barabarani kusubiri daladala. Bahati mbaya daladala lilichelewa kupita na mgonjwa akalazwa chini akiugulia maumivu.

Aliendelea kubaki chini akiugulia hadi wauguzi walipopata wazo la kusimamisha gari lolote litakalopita. Mungu si Athuman, lilipita gari la msamaria mwema mmoja, likasimamishwa na dereva kuombwa asaidie.

Mtu huyo akaingiwa na huruma na kumsaidia mgonjwa kumkimbiza hospitali. Huu ndiyo ulikuwa mchezo wa mwisho wa Nsa Job kwani majeraha haya yalimuathiri vibaya.

Hii ilikuwa aibu kubwa sana kwa mpira wetu na kuanzia hapo, ndipo ilipotungwa kanuni ya kulazimisha uwepo wa ‘ambulance’ uwanjani.

AMBULANCE TENA Machi 10, 2024, miaka zaidi ya 10 baada ya tukio la Nsa Job, umetokea tena mkasa wa Ambulance kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Ilikuwa kwenye mchezo wa ligi kuu kati ya KMC na Tabora United. Mchezaji mmoja wa KMC, Fred Tangalu, aliumia na kuhitaji huduma ya kwanza. Baadaye inaonekana haitoshi, anatakiwa apelekwe hospitali.

Akakimbizwa kwenye gari la wagonjwa ili awahishwe hospitali…lakini kwa bahati mbaya dereva wa gari hilo hakuwepo.

Akapigiwa simu, hapokei. Akaanza kutafutwa kama mbuzi aliyetoroka malishoni. Saka şaka na wewe, hayupo. Cha ajabu ufunguo aliuacha kwenye gari.

Akajitokeza mtu mwingine anayejua kuendesha gari, akaliwasha na kutoka nalo. Dereva alipoona ‘ofisi’ yake inatoka, akakurupuka kulifukuza…ndipo akabainika kumbe alikuwa ‘bize’ jukwaani akiangalia mpira.

PATRICK MUNTARI Machi 6, 2024, miaka zaidi ya 10 baada ya Patrick Muntari kukatisha soka la Nsa Job, amerudia tena, mara hii akiwa na Mashujaa ya Kigoma. Safari hii ni dhidi ya mchezaji wa timu yake ya zamani, JKT Tanzania, Edward Songo.

Katika mchezo wa Mashujaa na JKT Tanzania uliofanyika Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, Muntari alimuumiza vibaya Edward Songo na kukaribia kukatisha siyo tu soka lake bali maisha yake.

Edward Songo alıbidi akimbizwe kwa ndege kutoka Kigoma hadi Dar es Salaam hospitali ya Muhimbili, ile ile aliyokimbizwa Nsa Job. Alibainika fuvu lake limevunjika na meno yake yamehama eneo lake kurudi nyuma kwa sentimita zaidi ya tano.

Simulizi hizi ni kama za kufurahisha lakini kwa kweli ni za aibu kubwa sana kwa ligi yetu ambayo ni namba sita kwa ubora baranı Afrika. Dereva wa gari la dharura la wagonjwa anajisahau na kunogewa na mpira kiasi cha kutopatikana pale kazi iliyomleta ilipohitajika!?

Unaangalia tukio hili halafu unaongeza na matukio ya mashabiki kuingia uwanjani kutoa aidha mataulo ya makipa au maji ya kunywa wanayoweka pembeni.

Au wachezaji kugombania mataulo wakati mchezo unaendelea, unashika kichwa na kusema kuna jambo linatakiwa kufanyika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live