Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miaka 25 ya masimango Yanga ilivyohitimishwa Chamazi

Yanga Mashabiki Ks Miaka 25 ya masimango Yanga ilivyohitimishwa Chamazi

Mon, 2 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kwa mujibu wa Wikipedia, Clement Mzize amezaliwa Januari 7, 2004. Wakati mwingine wanasoka wa Afrika huwa wanadanganya umri. Fanya kwamba Clement alidanganya umri. Labda alizaliwa miaka kadhaa kabla ya hapo. Bado alikuwa hajazaliwa wakati Yanga ikiingia hatua ya makundi michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Juzi alifanikiwa kuhitimisha kazi ambayo Yanga ilikuwa imeianza Kigali wiki mbili zilizopita. Kazi ya kuipeleka Yanga hatua ya makundi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutimia miaka 25 bila ya kufanya hivyo. Fahari iliyoje kwao na kwa Mzize binafsi.

Mechi ilizaliwa katika ratiba ya CAF, ikafa Kigali halafu ikazikwa juzi Chamazi. Yanga ilikuwa imeshapita tangu Kigali. Ilichopaswa ilikuwa ni kuwa na nidhamu na kulinda matokeo yake iliyopata awali. Na ndicho ilichofanya kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho.

Ni kweli kwamba ilikuwa imetuliza vichwa kwa sababu tayari ilishashinda mabao 2-0 katika ardhi ya Paul Kagame. Yanga haikuwa na haraka katika kutengeneza mashambulizi kuanzia nyuma kwenda mbele. Ilipoteza nafasi za kutosha katika kipindi cha kwanza lakini haikuona uharaka katika kutafuta ushindi.

Muda mwingi wa mchezo Yanga ilikuwa timu bora uwanjani ikithibitisha kwamba haikushinda kwa bahati mbaya kwenye Uwanja wa Pele Kigali (zamani Nyamirambo), jijini Kigali. Kipindi cha pili rafiki zetu wa Sudan kiliwakumba kile ambacho kiliwakumba pale Kigali. Walijikuta wamechoka baada ya kukimbiza mpira kwa muda mrefu katika kipindi cha kwanza.

Pale Kigali, kocha Miguel Gamondi alimuingiza Clement Mzize kwa ajili ya kusaidiana na Kennedy Musonda katika mashambulizi. Wote wakafunga mabao. Safari hii alimtoa Musonda na kumuingiza Mzize aliyekwenda kufunga bao la kwanza lililokataliwa. Maxi Nzingeli alionekana kuuingiza ndani mpira ambao ulishatoka nje.

Baada ya dakika chache Mzize akafunga bao ambalo liligeuza shingo ya mwamuzi aliyeuweka mpira kati. Shukrani kwa krosi nzuri ya Joyce Lomalisa. Mzize akafunga na kushangilia kama Fiston Mayele. Tofauti ni kwamba wakati mwenzake alikuwa akishangilia kwa kutetema, yeye alikuwa anakata viuno. Akili za Watanzania.

Mpira ulikuwa umeishia hapo. Hakukuwa na namna ambayo ingewarudisha Al Merrikh mchezoni. Kwa mechi zote mbili Djigui Diarra alikuwa likizo. Isingewezekana kwa dakika chache zilizobaki akatoka likizo na kuingia katika kazi ngumu. Ni wazi kwamba kwa mechi mbili hizi ambazo Yanga ilikuwa imecheza na Wasudan kulionekana tofauti kubwa kati ya soka la Sudan tunalolijua dhidi ya soka la Tanzania ya sasa.

Nini kimewatokea Wasudan? Nadhani ni vurugu zinazoendelea kwao. Sawa Yanga ni bora, lakini Al Merrikh hii haikuweza kabisa kukabiliana na Yanga katika dakika 180 za Kigali na Mbagala. Pengo lilikuwa kubwa. Al Merrikh ilistahili kutolewa kwa idadi kubwa ya mabao.

Nini kinafuata? Yanga imetinga hatua ya makundi baada ya miaka 25 tangu ifanye hivyo. Mara ya mwisho ilipofanya hivyo Benjamin William Mkapa alikuwa na miaka mitatu tangu aingie madarakani na kuwa Rais wa tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwaka 1998.

Mara ya mwisho tangu ifanye hivyo, dunia ilikuwa haijaingia katika karne mpya. Nawakumbuka kina Shaaban Ramadhan, Edibily Lunyamila, Kennedy Mkapa, Abdul Maneno, Monja Liseki na wengineo ambao walifanya kazi hiyo. Baadaye ikawashinda watu wengi hadi walipokuja GSM na wahuni wapya pale Yanga.

Imeonekana kama ni kitu cha kawaida kwa Yanga kwenda katika makundi kwa sababu wametengeneza timu ambayo ghafla imeonekana kama vile kwenda makundi ni kitu cha kawaida. Kabla ya hapo Yanga ilikuwa inapanda Mlima Kilimanjaro katika safari yake ya kwenda makundi.

Simba ndio iliyokuwa inaifundisha Yanga namna ya kwenda hatua ya makundi katika miaka ya karibuni. Na haikuwa inafanya kwa bahati mbaya kwa sababu ilikuwa inapitiliza kwenda robo fainali kabisa. Na msimu uliopita nusura iende nusu fainali kama sio mabao ya wazi iliyoyakosa katika pambano la kwanza dhidi ya Wydad Casablanca pale Temeke.

Miaka ya karibuni Yanga imekosa mara mbili kwenda makundi. Mara ya kwanza ilikuwa pale Nigeria ilipochemka kuandikisha majina ya Khalid Aucho na Fiston Mayele katika daftari la CAF. Ikatolewa na Rivers United ya Nigeria pale Port Harcourt.

Ikajaribu tena lakini ikatolewa na Al Hilal ya Sudan. Iligeuka kichekesho huku Mnyama akifanya yake kila uchao. Hata katika msimu bora zaidi katika historia yao ambapo ilifika fainali za Kombe la Shirikisho msimu uliopita bado Simba ilikuwa robo fainali za CAF akisaka nusu fainali.

Na sasa imetinga hatua ya makundi ikifanya kitu ambacho mamia ya viongozi na maelfu ya wachezaji wa Yanga walishindwa kufanya kwa miaka 25 iliyopita. Nadhani asilimia 95 ya Watanzania hawakuishuhudia hatua hii ya Yanga mwaka huo. Marais watatu wamepita baada ya hapo.

Yanga imetuahidi hatua ya makundi kama lengo lake halisi la msimu huu. Sidhani kama inasema kweli. Mdomoni viongozi wake wanasema hivyo, lakini mioyoni hawasemi kweli. Wanataka kwenda mbali zaidi. Hawawezi kuridhika na hatua ambayo watani wao wanaiona kama kitu cha kawaida. Kwa Simba hatua hii sio mafanikio na Yanga wanajua.

Kitu ambacho kinaweza kuwanyamazisha Simba ni Yanga kwenda robo fainali halafu Simba isiende hatua zaidi ya hiyo. Hiyo itakuwa ngoma droo, ingawa Simba bado atatembea kifua mbele zaidi kwa sababu ameichezea hiyo hatua mara nyingi katika miaka ya karibu.

Kama Yanga akienda nusu fainali halafu Simba asiende walau ndicho kitu ambacho kitawanyamazisha Wanasimba kwa sababu hawajafikia hatua hiyo tangu mwaka 1974 wakati huo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiendesha Operesheni Vijiji vya Ujamaa katika nchi yake ya Tanzania. Kila la kheri kwa safari mpya ya Yanga mpya katika michuano hii. Ina kitu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live