Kuanzia mwaka 2002 hadi sasa, kumekuwa na utitiri wa wachezaji kutoka DR Congo ambao wamekuwa wakija nchini kuzitumikia timu mbalimbali za Ligi Kuu na hata zile za Ligi Daraja la Kwanza.
Historia inakumbusha kuwa ujio wa wachezaji kutoka DR Congo hapa Tanzania ulianzia miaka ya 1970 baada ya Yanga kumsajili Mayaula Mayoni (sasa marehemu) ambaye alikuja miaka hiyo kuishi nchini na baba yake ambaye alikuwa ofisa wa ubalozi wa nchi hiyo zamani ikiitwa Zaire.
Baadaye Mayaula aliyekuwa akicheza nafasi ya ushambuliaji, aliondoka nchini na kuelekea Ubelgiji na baadaye alirejea tena Tanzania ingawa hakurudi kama mchezaji bali mwanamuziki.
Baada ya Mayaula, mwaka 1974, Yanga ilimpata kocha Tambwe Leya (sasa marehemu) ambaye ni miongoni mwa makocha waliopatia mafanikio timu hiyo kwa kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati.
Kocha huyo baadaye aliondoka nchini na kurejea tena miaka ya 90 na alipoinoa timu hiyo kwa mara ya pili, alimsajili mchezaji mwenye jina kubwa zaidi duniani aliyewahi kuchezea Yanga, Nonda Shaban ‘Papii’ ambaye baadaye alikuja kuwa tishio Ulaya katika timu za Monaco, Galatasaray, AS Roma, Blackburn Rovers, Rennes na FC Zurich.
Upepo wa nyota kutoka DR Congo ulitulia kwa muda hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000 Yanga ilipowasajili, Pitchou Congo, Patrick Katalay, Alou Kiwanuka, Aime Lukunku ambao waligeuka kuwa vipenzi katika timu hiyo na soka la Tanzania kiujumla.
Baada ya hapo ni kama milango ilifunguliwa rasmi na idadi kubwa ya timu zikaanza kusajili wachezaji kutoka DR Congo ambapo baadhi ya mastaa wa huko waliotamba na Simba kwenye miaka ya hivi karibuni ni Doyi Moke aliyekuwa kipa, kiraka Banza Shikhala, Patrick Mafisango na Kanu Mbiyavanga. Usisahau majembe yao ya sasa Henock Inonga na Chris Mugalu.
Yanga licha ya kuwauza Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe, imebakiwa na Heritier Makambo, Fiston Mayele, Jesus Ducapel Moloko, Yanick Bangala, Djuma Shabaan na Chico Ushindi.
Azam wao wanatamba na straika matata, Idris Mbombo. Kumekuwa na kundi kubwa la wachezaji kutoka taifa hilo waliopo katika timu za Ligi Kuu, ligi ya Championship na wengine hata katika timu za madaraja ya chini na mchangani wakisaka mkate wao wa kila siku kupitia soka.
Swali ambalo pengine wengi wanajiuliza ni kwa nini upepo umekuwa ukiwakubali wachezaji kutoka taifa hilo hapa nchini kulinganisha na nyota wa nchi nyingine ambao baadhi licha ya kuwa na vipaji vikubwa wamekuwa hawadumu hapa Tanzania kwa muda mrefu.
Gazeti la Mwanaspoti limefanya utafiti na kubaini mambo mbalimbali ambayo yamefanya mastaa kutoka DR Congo kuliteka soka la Tanzania na kulowea hapa.
Urahisi wa maisha
Uzoefu wa baadhi ya Watanzania waliowahi kufika nchini DR Congo unaonyesha kuwa kumekuwa na ugumu wa maisha kwa watu wa daraja la kati na lile la chini nchini humo hasa katika jiji la Kinshasa ambalo ni makao makuu ya nchini hiyo ambalo wachezaji wengi wanaokuja Tanzania huwa wanatokea klabu za hapo.
Bei za bidhaa ziko juu na inahitajika mtu kutumia kiasi kikubwa cha fedha kupata mahitaji yake ya kila siku na hivyo kumfanya apate wakati mgumu katika kuweka akiba.
“Kinshasa maisha pale ni pagumu na kwa mfano hata hoteli na nyumba za kulala wageni za kawaida gharama yake ni kubwa kuanzia angalau Sh115,000 na hizo hazina huduma na hadhi nzuri.
Nilikaa pale siku chache lakini muda wote nilitamani kuondoka kurudi nyumbani Tanzania, imefikia wakati fedha zao na dola ya Marekani hazina tofauti unaenda dukani au kwenye mgahawa unatumia kama Faranga ya kawaida,” anafichua mwandishi mwandamizi wa Mwanaspoti, Khatimu Naheka.
Hiyo ni tofauti na Tanzania ambako wachezaji wa Kikongo, wamekuwa na maisha rahisi kutokana na unafuu wa gharama za maisha jambo linalowafanya wawe na uwezo wa kutumia vizuri fedha wanazopata hata kama kiasi ni kidogo au cha wastani. “Nikuibie siri hawa wachezaji wa Kikongo hapa Tanzania kuna wengine hata fedha zao za mishahara na posho hawatumii, wanapata kila kitu kwa mashabiki inategemea na kile wanachofanya uwanjani,” aliongeza Naheka.
Uvumilivu na Kujituma
Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ anafichua kuwa wachezaji kutoka DR Congo wamekuwa wakifanikiwa sana katika soka la Tanzania kutokana na hulka yao ya kutokubali kuathirika na presha pamoja na changamoto za nje ya uwanja kutokana na vilevile na wengi wao kukulia kwenye misingi ya soka.
Anaeleza kuwa sio rahisi kwa mchezaji wa Kikongo kukata tamaa pindi anapokutana na changamoto za nje ya uwanja au hata kutopata nafasi ya kucheza anapojunga na timu.
Akimuelezea Nonda, Malima anafichua kuwa alipokuja nchini alianza kuishi katika mazingira magumu na kucheza ligi za mtaani lakini uvumilivu na juhudi pamoja na kutokata tamaa vilimbeba.
“Kaka yake Nonda, alikuwa anaitwa Vincent, alikuwa rafiki yangu ndiye aliyeniambia niangalie kipaji cha mdogo wake ambaye alikuwa akicheza katika mashindano ya mtaani na kocha kumpeleka kikosi B ni kwa sababu Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ kuwa kwenye ubora nyakati hizo, hivyo asingeweza kupata nafasi moja kwa moja,” alisema.
“Bidii yake ilimfanya mwaka 1995 apande kikosi cha wakubwa na mechi iliyomfanya ang’are ni dhidi ya Vaal Professional ya Afrika Kusini, tulicheza kwao kwenye Kombe la Washindi, Nonda alifunga mabao yote mawili, mchezo ukimalizika kwa sare ya mabao 2-2,” alisema Malima.
Ikumbukwe kuwa Nonda wakati alipokuwa akiichezea Yanga, alikuwa akiishi na Bakari Malima.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ anasema; “Huwa wanakuja na malengo, wanafahamu nini kimewaleta Tanzania, hivyo wanakomaa hadi malengo yao yatimie, hawakubali kushindwa kizembe, ni wabishi na kipindi hiki wana uhakika wa kuja kucheza sio kupambana kutafuta nafasi ya kucheza.”
Mazingira na ushabiki
Mahaba ya mashabiki wa soka Tanzania kwa timu, wachezaji na nyota wa kigeni hasa wale wanaofanya vizuri, ni sababu nyingine ambayo Mwanaspoti limebaini imekuwa ikiwavutia wachezaji wa DR Congo nchini.
“Ushabiki wa soka sehemu kama Kinshasa au Lubumbashi upo kwenye timu kubwa tena kwenye mechi chache, tofauti na Tanzania ambako hata timu ikienda mkoani inajaza kwelikweli, mimi nilishangaa sana wakati nafundisha timu ya wakubwa wa Yanga,” aliwahi kunukuliwa Mwinyi Zahera kocha wa zamani wa Yanga, raia wa Congo.
Nyota wa zamani wa Simba, Malota Soma anasema wachezaji wengi kutoka DR Congo wanapatamani Tanzania kutokana na mazingira bora ya kufanya kazi haswa kwa mtu mwenye juhudi.
“Wachache sana ndiyo soka la Tanzania linawakataa lakini wengi wanafanikiwa, kikubwa ambacho kinawafanya kukomaa hapa nchini kwanza ni maslahi, lakini pia wanapata nafasi ya kucheza na mazingira ya Tanzania,” anasema Malota.
Kiwango bora na ufiti
Tofauti na wachezaji kutoka mataifa mengine, nyota kutoka DR Congo wamekuwa wakionyesha kiwango bora ambacho kimekuwa kikizisaidia timu zao kufanya vyema lakini pia wamekuwa hawapati majeraha ya mara kwa mara na muda mwingi huwa fiti jambo linalowafanya wazitumikie timu zao katika idadi kubwa ya mechi.
Starehe
Utulivu na amani uliopo Tanzania na uwepo wa starehe za aina mbalimbali, umewafanya wachezaji wengi kutoka DR Congo kupenda kuishi na kuchezea timu za hapa.
Tofauti na kwao ambako kwa muda mrefu kumekuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika baadhi ya maeneo, kwa hapa Tanzania wamekuwa na uhakika wa usalama na hakuna sheria kali ambazo zinaweza kuwabana kwenda kustarehe.
Ndio maana imekuwa sio jambo la ajabu kuona idadi kubwa ya wachezaji kutoka DR Congo katika klabu za usiku na kumbi za starehe hasa kunapokuwa na bendi za muziki wa asili ya kwao na hata muziki wa hapa.
Beki wa zamani wa Simba, Lubigisa Madata anasema wachezaji wengi kutoka DR Congo wanapokuja nchini, maisha ya Tanzania huwavutia.
“Wengi wana historia ya kucheza Yanga, sababu ya historia ya klabu hiyo mfano Nonda aliwahi kuwa rafiki yake na Bakari Malima.
“Hivyo wengi wao wanapokuja wanafiti mfumo wa klabu hiyo na hata tabia na wana uvumilivu wa hali ya juu,” anasema Lubigisa.
Nyota Wazawa wawavulia kofia
Beki wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ anafichua kuwa wachezaji kutoka DR Congo wamekuwa wakijituma vilivyo mazoezini na kwenye mechi akimtolea mfano Fiston Mayele.
“Ana nidhamu kubwa ya kazi yake, mcheshi kwa kila mtu na mpenda mazoezi, hivyo ndivyo ninavyomfahamu,” anasema Ninja.
Aliyekuwa beki wa Yanga, Adeyum Saleh ambaye kwa sasa anacheza Geita Gold anasema wachezaji kutoka DR congo ni wapambanaji akimtolea mfano beki mwenzake, Shaban Djuma
“Anapenda kazi yake kuwa bora uwanjani, alikuwa anapambana bila kukata tamaa, akishindwa kucheza vizuri leo, anajiandaa na kesho yake bora zaidi ya kuonyesha kiwango,” anasema Adeyum.
Wenyewe wajifagilia
Kiungo wa zamani wa Yanga, Papy Tshishimbi ambaye kwa sasa anaitumikia Kitayosce iliyopo Ligi ya Championship, anasema siri ya Wakongo kufanikiwa ni nidhamu, malengo, bidii na kupenda kazi yao.
“Sina maana kwamba ni wachezaji wanaokuja Tanzania tu, bali wanapopata nafasi ya kucheza popote, wanapambana na siyo wepesi wa kukata tamaa hata kama wanapitia changamoto kiasi gani.” anasema.