Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mhilu mzuka umepanda

Mhilu Data Mchezaji wa Simba, Yusuph Mhilu

Sun, 3 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Kupewa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha Simba katika mechi dhidi ya Dodoma Jiji, kumempa mzuka mshambuliaji chipukizi, Yusuph Mhilu aliyesema hataki kuchezea nafasi aliyopewa na kocha Didier Gomes na kwamba anaamini moto utaendelea ili kuleta heshima Msimbazi.

Mhilu pia aliingizwa kipindi cha pili kwenye mechi ya kwanza ya msimu akiwa na Simba dhidi ya Biashara United, pambano lililoisha kwa suluhu kabla ya juzi kuanzishwa na kumtoa kipindi cha pili kumpisha Duncan Nyoni wakati Simba ikiifumua Dodoma kwa bao 1-0 jijini Dodoma.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mhilu amesema kitendo cha kuanzishwa kikosini amekichukulia kwa uzito mkubwa kutokana na ushindani wa namba uliopo katika nafasi anayocheza na kusema inamfanya aongeze bidii zaidi ili asimuangushe Gomes na Wanasimba kwa ujumla waliomsajili msimu huu kutoka Kagera Sugar.

“Japo kocha ndiye anajua nilichokifanya dhidi ya Biashara, ndio maana akanipa nafasi nyingine ya kuanza kikosi cha kwanza na Dodoma Jiji. Ninachokiangalia ni kujituma ili nisimuangushe,” alisema Mhilu aliyeibuliwa Yanga na kukipiga pia Ndanda.

Amesema kwa namna Simba ilivyo anataka mashabiki waipe muda ili wachezaji wazoeane kabla ya kuwanyamazisha wote wanaoibeza hasa baada ya kuanza msimu na suluhu, huku ikitoka kupoteza katik Simba Day dhidi ya TP Mazembe na Ngao ya Jamii walipocharazwa na Yanga bao 1-0. “Tukizoena Simba hii itawashangaza wengi, kwani wachezaji ambao tumejiunga nayo msimu huu, tunahitaji kuandika rekodi ya kuendeleza ubingwa na kuvaa medali za heshima,” alisema Mhilu aliyemaliza msimu uliopita na mabao tisa, ikiwa ni manne pungufu na ule wa 2019-2021 aliofunga mabao 13.

Juu ya utofauti wa maisha ya Kagera na Simba, Mhilu amesema inachangiwa zaidi na malengo ya kila timu akisema Kagera huwa inapambana kumaliza nafasi za juu na kuepuka kushuka, lakini Simba inawaza ubingwa kila msimu, hivyo kufanya akili za kila mchezaji kukaa sawa ili kutoangusha lengo hilo.

Juu ya kiwango alichoanza kukionyesha Msimbazi, nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Ulimboka Mwakingwe amesema kwa rekodi zake katika timu alizopita na alivyofanya misimu miwili iliyopita ana uhakika wa kuingia anga la ushindani na John Bocco, Meddie Kagere na Chris Mugalu.

“Amejiunga na Simba yenye mastraika wenye njaa na mabao, hilo litamsaidia kukua zaidi,” amesema Mwakingwe huku straika wa Simba Queens, Opah Clement akisema Mhilu ni miongoni mwa wafungaji wazawa walio bora. “Naamini kuja kwake Simba atafanya mambo makubwa na atakuwa tishio,” amesema.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz