Achana na ushindi mnono kilioupata kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Mwanza Kombaini, kikosi cha Kagera Sugar kimeongezewa mzuka kabla ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold baada ya nyota waliokuwa majeruhi, Yusuph Mhilu na David Luhende kupona.
Kagera ilitua juzi jijini hapa na kupata ushindi dhidi ya Mwanza Kombaini kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, ikishinda mabao 6-0 yaliyofungwa na Abdallah Seseme, Abeid Athuman, Hamis Kiiza, Kassim Feka, Abubakar na Meshack Mwamita kujiandaa kuikabili Geita, Jumatano.
Nahodha David Luhende alikosekana mechi mbili za kwanza ugenini dhidi ya Azam na Simba kutokana na majeraha, wakati Mhilu aliyerejea kutoka Simba akiukosa mchezo wa pili dhidi ya Wekundu, lakini juzi wote walirejea na kuleta faraja.
Mhilu alikiwasha kwa dakika 60 akicheza winga ya kulia na baadaye kushoto na kushiriki kwenye bao moja akitoa asisti kwa Seseme, huku Luhende akiingia dakika ya 62 kukiwasha eneo la beki wa kushoto na kuisaidia timu yake kupata mabao matatu kwenye dakika 45 za pili.
Akizungumzia kurejea kwa nyota hao, Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar, Marwa Chambeli alisema ni faraja kubwa kwani watawaongezea nguvu na wigo wa kufanya machaguo kuelekea mchezo huo na wanatumaini wachezaji hao watapatikana siku hiyo kuisaidia timu kuvuna pointi tatu za kwanza msimu huu. “Wanatupa na kuongeza nguvu katika timu inakuwa na ‘stability’, tuliwakosa kutokana na majeraha lakini tuna imani watakuwepo siku ya mechi na sisi kama makocha, tunaona wameongeza nguvu pale ambapo tulikuwa tunaona panalegea tunakuwa na nguvu kwenye mechi inayokuja,” alisema Chambeli.
Kocha huyo wa zamani wa Biashara United akizungumzia ushindi wa mabao 6-0 na maandalizi dhidi ya Geita Gold, alisema kilikuwa kipimo kizuri na wanafanya maandalizi ya nguvu kuelekea mchezo ujao ili wapate ushindi huku akikiri utakuwa mchezo mgumu kutokana na upinzani wao.