Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgunda katika njia ya Tito Mwaluvanda

Ff RvZeXkAAd7a Juma Mgunda

Wed, 26 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Mwaka 1997, Yanga ilimfukuza kocha wake raia wa Uingereza, Steve McLennan na timu kubaki kwa msaidizi wake, Juma Pondamali hadi mwisho wa msimu.

Msimu mpya wa 1998 ulipoanza, mwenyekiti wa klabu hiyo, Rashid Ngozoma Matunda (marehemu), akasema klabu ipo kwenye mchakato wa kutafuta kocha mpya huku akimtangaza Tito Oswald Mwaluvanda (marehemu) kama msimamizi wa mazoezi.

Mwaluvanda hakuwa maarufu sana wakati huo hivyo mwenyekiti aliona aibu kumtaja kama kocha mkuu, akiepuka siasa za Kariakoo.

Mwaluvanda akawa anasaidiwa na nahodha wa zamani wa klabu hiyo, Fred Felix Minziro.

Mungu si Athuman, Mwaluvanda ‘kama msimamizi wa mazoezi’, akafanya maajabu.

Yanga yake ikatinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tena kwa kishindo baada ya ushindi mnono wa nyumbani wa mabao 6-1 dhidi ya Coffee United ya Ethiopia kufuatia sare ya 2-2 ugenini.

Ni rahisi mtu kusikia habari za Coffee United na kuidharau, lakini ilikuwa timu ngumu ambayo hadi inakutana na Yanga iliitoka kuitoa Al Ahly ya Misri.

Na kuitoa kwenyewe ni katika ardhi ya Farao, Mjini Cairo. Mechi ya Addis Ababa iliisha kwa sare ya 1-1.

Kwa ubabe wa Al Ahly nyumbani, ikaonekana kabisa Coffee United imeshatoka. Lakini haikuwa hivyo, wakaenda Cairo na kulazimisha sare ya 2-2...Al Ahly chali!

Lakini walipokutana na Yanga ya msimamizi wa mazoezi, wakapwaya na kuyaaga mashindano.

Msimamizi wa mazoezi Mwaluvanda akawa amefanya makubwa ambayo makocha wengi huko nyuma walishindwa.

Siyo Mwingereza McLennan wala siyo mzawa Sunday Kayuni waliotangulia kabla yake.

Na tangu 1998, Yanga haijafuzu tena hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa licha ya kuwa na makocha wengi, wa ndani na nje.

Isitoshe tangu 1998, hakuna kocha yeyote mzawa aliyefika hatua hiyo ya mashindano makubwa zaidi barani Afrika, hadi Juma Mgunda akiwa na Simba mwaka huu, 2022.

Kama Mwaluvanda, Mgunda naye ameichukua Simba baada ya kuondoka kwa Kocha Mkuu, Zoran Maki, kutoka Croatia.

Timu ikabaki kwa nahodha wa zamani Seleman Matola ambaye anaendelea kuwa msaidizi wake.

Kama Yanga ya Matunda, Simba nao walimtambulisha Mgunda kama kocha wa muda tu, huku wakiwa katika mchakato wa kutafuta kocha mpya.

Lakini kufumba na kufumbua, Mgunda anafanya makubwa. Anaiongoza klabu hiyo kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Taarifa za chinichini zinasema Simba imeamua kumuachia kabisa timu Juma Mgunda aendelee nayo kwenye hatua ya makundi.

Hiyo ni heshima kubwa sana kwa makocha wazawa ambao klabu zetu, hasa hizi kubwa, ni kama zimekuwa zikiwapotezea.

Kwa mfano, Azam FC haijawahi kuwa chini ya kocha mzawa, tangu ipande Ligi Kuu mwaka 2008.

Mara zote imekuwa na makocha wa kigeni lakini hakuna ambacho imekipata huku ikiishia kuwatimua makocha hao bila kumaliza msimu.

Ni mara moja tu, ndiyo Azam FC ilianza msimu na kuumaliza na kocha huyo huyo.

Huo ulikuwa msimu wa 2011/12, ambapo Muingereza, Stewart John Hall aliumaliza msimu katika nafasi ya pili kwenye ligi.

Kabla ya hapo na hata baada ya hapo, hakuna kocha yoyote wa klabu hiyo aliyefanikiwa kuuanza msimu na kuumaliza akiwa Chamazi.

Hata Stewart mwenyewe ambaye aliondoka na kurudi na kuondoka na kurudi tena klabuni hapo, alishindwa kumaliza msimu.

Makocha wote hao ni wageni, hakuna hata mzawa mmoja. Ingekuwa makocha wa kigeni wana kitu ambacho makocha wa Kitanzania hawana, basi Azam FC ingeshafika mbali sana...lakini wako hapa hapa.

Nadhani Mgunda anaweza kubadilisha fikra mgando za viongozi wa klabu kama Azam FC na kuanza kuwafikiria makocha wazawa.

Mwaluvanda alifanya makubwa akiwa kama ‘msimamizi wa mazoezi’, Mgunda anafanya makubwa akiwa kama kocha wa muda.

Mgunda kuwa kocha wa Simba inamfanya kuwa mzawa wa pili Msimbazi tangu 2013 pale timu ilipokuwa chini ya wazawa, Abdallah Seif Athuman (Kibaden) na Jamhuri Kihwelo (Julio).

Yanga mara ya mwisho kuwa na kocha mzawa ilikuwa mwaka 2019, Juma Mwambusi.

Makocha vijana kama kina Mecky Mexime na Shadrack Nsajigwa, wanatamani siku moja wawe kama Mgunda. Ni muda sasa wa klabu zetu kuwaamini wazawa.

Mambo makubwa kwenye mpira wa Tanzania yamefanywa na makocha wazawa, siyo wageni.

Simba ilipofika nusu fainali ya klabu bingwa Afrika mwaka 1974, kocha alikuwa mzawa Paul ‘West’ Gwivaha.

Simba ilipofika fainali ya Kombe la CAF 1993, kocha alikuwa mzawa Kibaden.

Namungo ilipofika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2020, kocha alikuwa mzawa Hemed Suleiman ‘Morocco’.

Nadhani Mgunda amebeba hatima ya imani ya klabu zetu kwa makocha wetu.

Mafanikio yake kwenye hatua ya makundi yatamfanya aaminiwe zaidi na kufungua milango kwa wazawa wengine kuaminiwa zaidi.

Simba nayo impe ushirikiano kama ambao kocha wa kigeni angepewa.

Isije ikamfanyia kama Mwaluvanda ambaye kwenye hatua ya makundi aliondolewa baada ya mechi moja tu. Yanga ilianza kwa sare ya 1-1 na Manning Rangers ya Afrika Kusini, baada ya huo mchezo, msimamizi wa mazoezi Mwaluvanda akaondolewa.

Nafasi yake ikachukuliwa na Raoul Shungu, kocha wa Rayon Sport ya Rwanda ambayo Mwaluvanda aliitoa kwenye raundi ya kwanza ya klabu bingwa Afrika kabla ya kukutana na Coffee United.

Shungu akachezea vichapo hatari. Alianza kwa kipigo cha 2-1 kutoka kwa Asec Mimosas ya Ivory Coast, akafuatia kipigo cha 6-0 kutoka Raja ya Moroicco, akaja na kipigo cha 4-0 kutoka Manning Rangers na baadaye kipigo cha nyumbani cha 3-0 kutoka Asec.

Shungu aliambulia sare moja tu ya 3-3 dhidi ya Raja hapa nyumbani.

Ukipima huwezi kuona kama mabadiliko ya Mwaluvanda kwa Shungu yalileta matunda yoyote.

Wakati Mgunda anapita njia ya Mwaluvanda, basi apitie sehemu nyingine tu lakini siyo hii ya kuondolewa baada ya mechi moja ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Chanzo: Mwanaspoti