Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgunda azua hofu Simba, afunguka aliko

Juma Mgunda Kocha Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda

Sun, 21 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa Simba wameingiwa na hofu kutokana na kutoonekana mazoezini kwa kocha msaidizi, Juma Mgunda, huku kukiwa na taarifa za chinichini huenda akatemwa na kurejea kwenye klabu yake ya zamani ya Coastal Union, lakini mwenyewe ameibuka na kutuliza presha hiyo.

Hofu ya mashabiki wa Simba ilitokana na kukosekana kwa kocha huyo kwenye mazoezi ya timu hiyo ilikuwa ikijiandaa kucheza na Ruvu Shooting na kuibuka uwanjani, pia kuonekana kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga wakati Wagosi wa Kaya walipovaana na kuifunga Ihefu kwa bao 1-0.

Ipo hivi. Tangu Simba irejee mazoezini kujiandaa na mechi zilizosalia na kocga huyo hajaonekana mazoezini na kuzua presha kwa mashabiki waliohudhuria mazoezi hayo ya juzi na jana, huku ikielezwa taarifa yupo mbioni kupigwa chini ndizo zinazomnyima raha na kutoweka kambini, hata hivyo ameibuka na kufunguka kuwa, alikosekana kikosini kwa matatizo ya kifamilia na leo atakuwapo.

"Ni kweli sikuwepo mazoezini kwa sababu nilikuwa na mambo yangu ya kifamilia lakini kesho (leo) nitakuwepo kuendelea na kazi, kwani mimi bado ni mfanyakazi wa Simba," alisema Mgunda alipozungumza na Mwanaspoti jana asubuhi.

Licha ya Mgunda kusisitiza kwamba bado anaendelea kuitumikia timu hiyo iliyopo nafasi ya pili ya Ligi Kuu kwa sasa nyuma ya mabingwa Yanga, lakini inaelezwa kitendo cha kuonekana kwenye mechi ya Coastal na Ihefu iliyopigwa wiki iliyopita iliwashtua zaidi mashabiki wa Msimbazi.

Hata hivyo, Mwanaspoti iliamulia kuulizia kwa Wagosi juu ya taarifa za kuitaka kuimrejesha kocha huyo kipenzi cha mashabiki wa Simba na kuelezwa kwa sasa akili za mabosi wa klabu hiyo ya Tanga ni kujikita zaidi kuhakikisha inashinda mechi zao mbili zilizobaki na kubaki ligi ya msimu ujao.

Ofisa Habari wa Coastal, Jonathan Tito alipoulizwa juu ya mipango ya kumrejesha Mgunda kikosini alijibu kuwa; "Sisi tunaye kocha na kama mipango ya kutafuta kocha mpya basi sio kwasasa, kikubwa tunachokifikiria ni namna gani ya kumaliza mechi zetu mbili zilizobaki ili tushinde.

"Mgunda ni kati ya makocha wazuri wazawa, lakini suala la kusema anarejea au kuwepo kwenye mipango ya kumrejesha silifahamu kwa sasa. Sidhani kama lipo kwani halijajadiliwa popote ndani ya timu yetu, ninachofahamu hadi sasa ni kwamba Mgunda ni kocha wa Simba," alisema Tito.

Mgunda alijiunga Simba, Septemba 7, mwaka jana na mechi ya kwanza kuiongoza timu hiyo ilikuwa kwenye mechi za awali za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Big Bullets ya Malawi na kushinda ugenini kwa mabao 2-0, kisha kuiongoza kwenye Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons na kushinda 1-0.

Katika hatua nyingine, Simba leo itashuka uwanja wa Mo Siomba Arena kwa kuvaana na Ngome katikia mchezo wa kirafiki kujiandaa na mechi za ligi ambazo zinaelezwa zimeahirishwa hadi mwezi ujao. Simba imesaliwa na mechi dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union, itakayocheza pia na Azam kufunga msimu wa 2022-2023.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: