Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgunda atoa neno mastaa Simba

Mgunda Neno Staa Mgunda atoa neno mastaa Simba

Wed, 28 Sep 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mastaa wa Simba washindwe wenyewe, kwani kocha Juma Mgunda anajaribu kumpa nafasi kila mchezaji kuonyesha kipaji chake na atakayemshawishi kwa kuonyesha kiwango cha juu, ataunda kikosi chake cha kwanza.

Katika mazungumzo yake Mgunda alisema anamthamini kila mchezaji aliyepo ndani ya kikosi hicho na anaamini ana kitu cha kufanya kwa ajili ya kuinufaisha timu, hivyo kumpa nafasi kila mmoja anajua kutatengeneza kikosi bora zaidi.

“Kuna faida nyingi kila mchezaji akijihisi ni muhimu kwenye timu, kwanza kunakuwa na ushindani wa namba ambao utatengeneza kikosi bora zaidi na kumfanya anayepata nafasi kulinda kiwango chake, jambo la pili mchezaji anayeanza na kuingia wote wanakuwa wana ubora uleule,” alisema na kuongeza;

“Ukiachana na hilo, pia wachezaji wanakuwa na morali ya juu ya kuhakikisha kila mchezo unaokuwa mbele yao wanakuwa wanatamani kushinda na ukizingatia msimu huu umekuwa na ushindani na kila timu imejipanga kufanya malengo yake mapema.”

Mgunda alisema hadi sasa anawaona mastaa wa timu hiyo, wamekuwa na njaa ya mafanikio ya kutamani kufanya vitu vikubwa, hivyo anawapa maarifa na mbinu za kuhakikisha wanaishi ndoto zao.

“Nimeona wachezaji jinsi ambavyo wana hamu ya kuonyesha viwango vyao, hilo ni jambo linalotia moyo pia linaleta umoja wa kufanya kazi kwa mshikamano ambao utafanya tutimize malengo yetu kwa ushujaa,” alisema.

Simba ilimchukua Mgunda baada ya kuondoka aliyekuwa kocha wao, Zoran Maki na ameiongoza timu hiyo dhidi ya Nyasa Big Bullets mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo aliifunga jumla ya mabao 4-0 na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Prisons timu yake ikishinda bao 1-0.

“Ndio tumeanza bado safari ipo, lakini jeshi langu lipo kamili kwa ajili ya kazi, jambo zuri zaidi napata muda wa kuendelea kukiangalia kikosi kupitia mechi za kirafiki zinazochezwa huku Zanzibar,” alisema.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz