Simba ilirejea jana mchana Dar es Saalam ikitokea Cairo, Misri baada ya kumalizika kwa mechi ya marudiano ya michuano mipya ya African Football League (AFL) dhidi ya Al Ahly iliyoisha kwa sare ya mabao 1-1, na Wekundu wa Msimbazi kuondolewa kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya kutoa sare ya jumla ya mabao 3-3, huku kocha aliyekuwa hasikiki Juma Mgunda akiibuka na kutoa kauli ya kupongeza.
Benchi la ufundi la Simba limewapa mapumziko ya siku moja wachezaji wake kisha leo jioni watarejea uwanjani kujiandaa na mechi zijazo za ligi ambazo wamepania kufanya vizuri zaidi.
Simba inajiandaa na mchezo dhidi ya Ihefu ambao awali ulikuwa umepangwa kupigwa Jumapili, lakini jana ulitangazwa kuwa utapigwa keshokutwa Jumamosi.
Kocha Mkuu wa Simba, Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’, alisema; “Mchezo wetu na Al Ahly umeona ulivyokuwa, tulijipanga kushinda mechi lakini imemalizika kwa sare.
“Huko tumetoka tayari na sasa tunaangalia kilicho mbele yetu. Tuna mechi za ligi ambazo tunahitaji kushinda hivyo hatuwezi kupumzika hadi pale tutakapomaliza misheni yetu kwa msimu huu na lengo ni kutwaa ubingwa,” alisema kocha huyo.
MGUNDA ANENA
Baada ya ukimya wa muda mrefu, kocha Juma Mgunda aliyekaimu nafasi ya kocha Mkuu Simba kabla ya ujio wa Robertinho kisha kuwa msaidizi wake na baadaye kubadilishiwa majukumu, jana alipiga stori na Mwanaspoti na kuwamwagia sifa, benchi la ufundi, wachezaji, viongozi na mashabiki wa Simba kwa kile walichokifanya.
Mgunda ambaye kwa sasa ni moja ya wataalamu wa ufundi ndani ya Simba akihudumu katika timu zote (Vijana, Wanawake na kubwa), kwa majukumu tofauti ameliambia Mwanaspoti licha ya timu hiyo kushindwa kutinga nusu fainali ya AFL, lakini wanastahili zaidi pongezi kwani wameiheshimisha nchi.
“Simba imeiheshimisha nchi, kutoa sare mbili mfululizo tena dhidi ya timu namba moja kwa ubora Afrika sio jambo dogo, kila mmoja ndani ya Simba ametimiza wajibu wake licha ya kwamba mwisho wa siku kanuni zimeamua matokeo.
“Kuanzia kwa Wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki kila mmoja anastahili kujivunia hiki kilichofanywa na Simba kwani timu yetu imeonyesha kuwa haikuwa bahati mbaya kuchaguliwa kati ya timu nane shiriki katika mashindano haya makubwa kwa mara ya kwanza. Hili ni jambo la kupongezwa,” alisema Mgunda ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Simba na kuongeza;
“Ninachowaomba na kuwasihi wachezaji wetu, haya waliyotuonyesha yawe endelevu. Wasibweteke, bado tuna michuano mikubwa kama Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu, tunahitaji kufikia malengo kwenye kila taji tunalowania hivyo ile ari ya upambanaji waliyoonyesha kwenye mechi hizi mbili dhidi ya Ahly wanapaswa kuwa nayo katika kila mchezo.”