Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgunda apewa ushindi Dabi ya Kariakoo

Juma Mgundaaa Kocha Juma Mgunda

Fri, 21 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kiungo wa zamani wa Yanga na Toto African, Castory Mumbala amesema licha ya wadau na mashabiki wengi kuweka mchezo wa dabi kama kipimo kwa kocha Juma Mgunda kupewa mkataba wa kudumu Simba, lakini hilo linabaki kwa wachezaji wanaopaswa kumbeba kama wanahitaji kuwa naye.

Dabi ya Kariakoo itapigwa Jumapili saa 11 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huku Yanga ikiwa na rekodi nzuri kwenye mechi tano za karibuni ikishinda tatu na sare mbili ukiwemo ushindi wa 2-1 kwenye Ngao ya Jamii msimu huu.

Mumbala ambaye msimu uliopita alikuwa kocha wa viungo wa Kagera Sugar iliyopo Ligi Kuu Bara, aliliambia Mwanaspoti kuwa, Mgunda hana presha kama watu wengi wanavyodhani bali wenye presha ni wachezaji wanaopaswa kupambana kumbakisha.

“Kwa michezo ya ndani Yanga wamekuwa bora kwa miaka ya karibuni kwani Simba ni kama walikuwa bado wanapambana kuiweka timu sawa. Mgunda hana presha, presha iko kwa wachezaji kama watakuwa wamemkubali basi itawabidi kupambana ili wabaki naye,“ alisema Mumbala aliyewahi kucheza soka la kulipwa nchini Nepal katika klabu za Three Stars na Himalayan Selva 2010 na 2011.

Kiungo huyo wa zamani wa Coastal Union na aliyewahi kukipiga Kenya, alisema mtanange huo utakuwa mgumu kutokana na matokeo ya sasa ya Yanga baada ya kuondolewa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kufungwa na Al Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-1.

“Mechi itakuwa ngumu ukiangalia Yanga wametoka kwenye mchezo mgumu na wametolewa kwahiyo watakuja na nguvu kubwa ili kurudisha imani kwa mashabiki wao. Simba wanaimarika na mzuka umeongezeka baada ya mechi hizi mbili dhidi ya Primeiro de Agosto) na kupata matokeo,” alisema.

Mechi ya Jumapili inatarajiwa kukutanisha vikosi bora vya timu hizo isipokuwa wachezaji wachache ambao ni majeruhi au wenye adhabu akiwamo Bernard Morrison aliyefungiwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live