Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgunda anukia Singida Fountain Gate

Mgunda Pic Siri Kocha Juma Mgunda

Thu, 7 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Singida Fountain Gate imelivunja benchi lote la ufundi la timu hiyo lililokuwa chini ya kocha Thabo Senong, na tayari mabosi wa klabu hiyo wameanza msako wa kocha mkuu mpya, huku Juma Mgunda 'Guardiola Mnene' a.k.a Mzee wa Boli Litembee, akitajwa yupo mbioni kubeba mikoba hiyo.

Mwanaspoti imepenyezwa taarifa kwamba Singida inamsaka kocha mkuu ili kuendeleza pale alipoishia Msauzi Senong aliyekuwa akiinoa timu hiyo baada ya Mjerumani Ernst Middendorp kutimkia Afrika Kusini.

Inaelezwa kwamba kiuchumi hali ya Singida haipo vizuri, jambo linawafanya na baadhi ya wachezaji ambao hawakutaka kutaja majina yao, kujiandaa kuvunja mikataba yao mwishoni mwa msimu huu, kama ilivyotokea kwa Bruno Gomes aliyeachana na timu hiyo hivi karibuni na anayetajwa kuwindwa na Ihefu

Habari kutoka ndani ya Simba zinadokeza kuwa, Mgunda aliyebakisha muda mfupi wa mkataba yupo mbioni kutua Singida akiwa ni kati ya makocha waliopo kwenye rada za mabosi wa klabu hiyo ya Ligi Kuu Bara.

"Mgunda amebakiza mkataba mfupi, hivyo viongozi wa Singida wametuma maombi, kuwaruhusu wamuachie akawasaidie kumalizia msimu huu," kilisema chanzo makini kutoka ndani ya Simba, huku kigogo mmoja kutoka Singida ambaye naye hakutaka kutaja jina kwa upande wake amekiri juu ya msako wa kocha mpya.

"Ni kweli ishu ipo ila bado haijakamilika, wamezungumza na makocha wengi ila Mgunda ndiye ana asimilia kubwa ya kupatikana."

Kwa upande wa Mgunda, aliyewahi kutamba na Coastal Union enzi akicheza kabla ya kugeukia ukocha akiinoa timu hiyo na kuajiriwa Simba misimu uliopita kabla ya kuhamishiwa Simba Queens, alipoulizwa juu ya taarifa hizo za kujiandaa kutua Singida amesema;

"Ndio kwanza nakusikia wewe ndugu mwandishi, ila waswahili wanasema dalili ya mvua ni mawingu, japo mawingu yanaweza yakatanda na mvua isinyeshe, ila kwa sasa karibuni kwenye mazoezi ya Simba Queens."

Singida Fountain Gate imekuwa na mwenendo mbaya katika Ligi Kuu ikicheza mechi tano bila ushindi, huku ikiwa imekimbiwa na baadhi ya mastaa waliohamia Ihefu ambayo imetangaza kuhamia kwenye Uwanja wa Liti, Singida kutoka Highland Estate uliopo Mbarali Mbeya.

Timu hiyo kwa sasa inashika nafasi ya 11 ikitoka ya nne iliyokuwa inaishikilia kabla ya ligi haijasimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 ikiwa na pointi 21 kutokana na mechi ya 19

Chanzo: www.tanzaniaweb.live