Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda, amesema malengo ya kwanza yametimia ya kufuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, na sasa sasa anapiga hesabu za kufuzu robo fainali ya michuano hiyo.
Kauli hiyo ameitoa mara baada ya Simba kufuzu hatua ya makundi ya mashindano hayo yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kuwaondoa Primeiro De Agosto ya Angola kwa jumla ya mabao 4-1.
Akizungumza na Spoti Xtra, Mgunda alisema ana furaha kubwa kwake kutimiza malengo aliyowekewa na uongozi ya kuipeleka timu hatua ya makundi kimataifa.
Mgunda alisema baada ya kufanikisha malengo hayo, sasa anataka kuona akiweka rekodi ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo.
Aliongeza kuwa, hilo linawezekana kwao kufuzu robo fainali kutokana na ubora wa kikosi chao na maandalizi anayoendelea kuyafanya ya kukisuka kikosi chake.
“Niwashukuru wachezaji waandamizi ambao nimewakuta hapa Simba, nawazungumzia kina Bocco (John), Chama (Clatous), Mkude (Jonas) na Manula (Aishi) ambao wamenipokea vizuri na kunipa ushirikiano ambao leo hii unatupeleka makundi kimataifa.
“Wakati nakabidhiwa timu, uongozi ulinipa malengo ambayo ni kuifikisha timu katika hatua ya makundi kimataifa ambayo nimeyatimiza kwa kuwaondoa De Agosto.
“Hivyo basi ninataka kuvuka malengo nikiwa na Simba ambayo ni kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hii ya kimataifa,” alisema Mgunda.