Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgunda aahidi taji la CECAFA Simba Queens

Mgunda X Simba Queens Mgunda aahidi taji la CECAFA Simba Queens

Thu, 15 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati msafara wa wachezaji 25 wa Simba Queens wakiondoka jana kuelekea Ethiopia ambako timu hiyo itashiriki mashindano ya klabu bingwa wanawake ya baraza la vyama vya mpira wa miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), kocha wa timu hiyo, Juma Mgunda ametamba kutwaa ubingwa.

Mashindano hayo ya kila mwaka, bingwa wake ndio hupata nafasi ya kushiriki mashindano ya klabu bingwa Afrika kwa wanawake ambayo tarehe na nchi ambako yatafanyika kwa mwaka huu bado haijapangwa.

Mgunda alisema kuwa wamefanya maandalizi ya uhakika ambayo yanampa matumaini kwamba watafanya vizuri wakiwa Ethiopia na kuitoa kimasomaso nchi kwa kurudisha taji Tanzania.

"Tunashukuru kambi imekwenda vizuri na tukiamka salama leo tunaanza safari tukiwa na wachezaji 25 ambao wamesajiliwa na timu na tunaamini tutakwenda kufanya vizuri," alisema Mgunda.

Mgunda alisema katika kundi la wachezaji ambalo limeenda Ethiopia, yupo Aisha Mnunka ambaye aliripotiwa kutoroka na kutojiunga na wenzake kambini licha ya kuwa na mkataba wa mwaka mmoja umesalia wa kuichezea timu hiyo.

"Mnunka ni moja ya wachezaji tuliowajumuisha na kwa sasa sio muda mzuri wa kuzungumzia hilo lakini fahamuni kuwa tuko vizuri na jana (juzi) tulikaa na viongozi wakazungumza na wachezaji kuwapa hamasa na tunawashukuru kwa kutimiza matakwa ya benchi la ufundi kwa kusajili watu tuliowataka," alisema Mgunda.

Katika mashindano hayo ya Cecafa, Simba Queens imepangwa kundi B na timu za PVP Buyenzi ya Burundi, Kawempe Muslim Ladies ya Uganda na FAD ya Djibouti.

Agosti 18 itaanza kuminyana na FAD, Agosti 21 dhidi ya Kawempe kisha kufunga hesabu na PVP Agosti 24 kwenye hatua ya makundi.

Simba inatafuta tiketi ya kucheza klabu bingwa Afrika kwa wanawake kwa mara ya pili kwani ilishiriki mara ya kwanza 2022 na kumaliza nafasi ya nne, huku msimu uliopita ilienda JKT Tanzania ambayo ilitolewa hatua ya makundi.

Chanzo: Mwanaspoti