Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgunda: Tunasubiri hatima yetu

Juma Mgunda Sababu.jpeg Kocha Juma Mgunda.

Mon, 27 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha wa Simba, Juma Mgunda, amesema kwa hali ilivyo sasa, mechi watakayocheza dhidi ya JKT Tanzania na ile kati ya Geita Gold dhidi ya Azam FC, ndiyo itakayoamua hatima ya timu gani kati yao na Wanalambalamba hao watakwenda Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza baada ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC walioibuka na ushindi wa bao 1-0, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Mgunda alisema katika mechi hiyo ya juzi walihitaji ushindi wa mabao mengi, lakini kwa bahati mbaya haikuwa hivyo, hivyo hawana la kufanya na hatima yao itaamuliwa katika mechi hizo.

"Lengo letu ilikuwa tupate pointi tatu na mabao mengi lakini haikuwa hivyo, kwa sababu hiyo ni mapema zaidi sasa kusema lolote, kilichobaki tunakwenda kwenye viwanja vya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mechi iliyobakia.

Ukweli ni kwamba hizi mechi ni ngumu, ikumbukwe kuwa KMC nao walikuwa wanaisaka nafasi ya nne walikuwa wanagombania na Coastal Union," alisema Mgunda.

Kocha huyo alisema japo timu yake ina baadhi ya wachezaji wazuri, lakini imekuwa na mapungufu mengi ambayo watayaweka hadharani ikifika wakati wa kufanya hivyo.

"Niwapongeze wachezaji wangu wamecheza vizuri, lakini timu ina mapungufu kadhaa ambayo ikifika wakati wake tutayazungumza," alisema kocha huyo aliyechukua kijiti kutoka kwa Abdelhak Benchikha ambaye alibwaga manyanga.

Aidha, Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, alisisitiza kuwa sasa wanasubiri mechi za mwisho kujua hatima yao.

"Malengo matatu yote yamekamilika, ilikuwa ni kuwaletea mechi mashabiki wa Arusha, pili kuona mechi yetu inakuwa na watazamaji wengi, tatu ilikuwa ni kupata ushindi na yote yametokea.

Unaweza kuwa siyo ushindi wa kuridhisha sana kwa sababu ya mbio zilizopo sasa, hatukutakiwa kushinda tu, bali kwa idadi kubwa ya mabao kwa sababu hali inavyoonekana, nafasi ya kwenda Ligi ya Mabingwa haitaamuliwa na kushinda tu, kila mtu ana uwezo wa kushinda mechi zake, kinachokwenda kutengeneza utofauti ni idadi ya mabao. Pamoja na yote mwamuzi ni mechi za mwisho," alisema Ahmed.

Mpaka sasa timu ambazo zina tiketi mkononi ya kucheza mashindano ya kimataifa ni Yanga ambayo itacheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, Coastal Union itakayocheza Kombe la Shirikisho kwa kuwa inashika nafasi ya nne kwa pointi 42 ambazo hazitofikiwa na timu yoyote iliyo chini yake.

Azam iko nafasi ya pili ikiwa na pointi 66 na mabao 61, Simba ya tatu ikiwa na mabao 66 na mabao ya kufunga 57.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live