Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgunda: Itakuwa zaidi ya vita

Sadio Kanoute Goal Itakuwa zaidi ya vita

Tue, 31 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Juma Mgunda amekiri haikuwa rahisi kuifunga Coastal Union na kuing’oa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) kutokana na aina ya soka inalocheza na upinzani mkubwa uliopo, lakini akisema mechi ijayo ya 16 Bora dhidi ya African Sports itakuwa vita zaidi baina yao.

Simba ilipata ushindi wa bao 1-0 katika pambano kali lililopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi usiku, kiungo mkabaji Sadio Kanoute akitupia kambani dakika ya 56 akimalizia pasi tamu ya Pape Ousmane Sakho ambaye awali alifumua kombora akipokeza pasi ya Clatous Chama, lakini mabeki wa Coastal wakaokoa na kuwahi mpira aliompasia mfungaji aliyepiga shuti kali la chinichini.

Kocha Mgunda anayeiongoza timu kwa sasa baada ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kwenda kwao kwa dharura ya kifamilia, alisema alijua tangu mapema mechi hiyo ingekuwa ngumu kwa aina ya soka inalocheza akiwa ametoka kuifundisha hivi karibuni.

Alisema kocha anayeinoa Coastal ni mtu aliyefanya naye kazi kwa muda mrefu hivyo anajua kila kitu kuhusu yeye na ile falsafa ya boli litembee, ndio maana alisema mapema isingekuwa kazi rahisi, lakini anashukuru wamepambana na kushinda na sasa wanaenda kujiandaa kwa mechi dhidi ya Sports.

Mgunda alisema Sports kama ilivyo Coastal ni timu inayotoka Tanga na wanamjua kama anavyowajua yeye na kukiri itakuwa ni kama vita, kwani kila timu itakuwa na kiu ya kutaka kutinga robo fainali ya michuano hiyo inayotoa tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Hata hii haitakuwa mechi nyepesi. Itakuwa ni kama vita na kama nilivyosema kwamba kila mchezo una mipango yake na muda ukifika tutajipanga kwa mechi hiyo. Kwani lengo letu ni kuhakikisha tunashinda taji hili na ili tufanikiwe tunapaswa kushinda kila mchezo kwa kuwa huku hakutafutwi alama bali ushindi,” alisema Mgunda.

Mechi hiyo ya 16 Bora inatarajiwa kuchezwa mapema Machi na mshindi kwenda robo fainali na Simba kwa sasa inajiandaa na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Big Stars kabla ya kusafiri kwenda Guinea kwa mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AC Horoya mwezi ujao.

Chanzo: Mwanaspoti