Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgunda: Aisee msichukulie poa!

Mgunda Pic Tanga Kocha wa Simba, Juma Mgunda

Sat, 3 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Simba ipo jijini Tanga tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wao, Coastal Union, huku mastaa wa timu hiyo wakionywa mapema wakiambiwa ‘msichukulie, poa tusiumbuke’.

Kocha Juma Mgunda ndiye aliyewaonya mastaa hao wa Simba kwa kuwaaambia kuwa, licha ya kuifahamu vizuri Coastal, hiyo sio sababu ya kubweteka kwenye mechi yao itakayopigwa leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini humo.

Mgunda aliiinoa Coastal kwa muda mrefu kabla ya Septemba mwaka huu kubebwa na Simba, alikiri mchezo huo wa kesho utakuwa mgumu na wenye ushindani na lazima wachezaji wake wawe makini ili wasiumbuke.

Akizungumza jana, Mgunda alisema kikosi kina malengo makubwa ikiwamo kuhakikisha wanavuna pointi tatu zitakazowaweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Alisema, anaihheshimu Coastal, hivyo amewataka wachezaji wake kuhakikisha wanazitumia vyema dakika 90 ambazo kila mmoja anahitaji matokeo ili kujiweka salama kutokana na ushindani mkali uliopo.

“Kuwa kocha muda mrefu Coastal na kuwafahamu vizuri sio sababu ya kwenda kuwadharau hapana, cha msingi ni wachezaji wangu kuwaheshimu ili tuweze kupata matokeo, na nimeongea nao juu ya hilo,” alisema Mgunda aliyeongezea kuwa ligi imekuwa na ushindani mkali hivyo kila mchezo una umuhimu mkubwa kwake na anaheshimu anayekutana naye.

Kocha huyo pia aliwataka mashabiki, wanachama na wapenzi wa klabu hiyo waendeleze moyo wa kuisapoti timu yao katika mazingira yoyote ambayo wanayapitia iwe kupoteza, sare na kushinda.

Simba inashika nafasi ya tatu katika msimamo ikiwa na pointi 31 mara baada ya kujitupa dimbani mara 14 ikishinda michezo tisa, sare nne na kupoteza mmoja huku Coastal ikishika nafasi ya 12 baada ya kucheza michezo 13 ikishinda mitatu sare tatu na kupoteza saba, ukiwamo wa juzi mbele ya Dodoma Jiji.

Chanzo: Mwanaspoti