Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgosi: Huyu Miquissone ni noma

Mgosi Pic Data Mgosi: Huyu Miquissone ni noma

Mon, 26 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MWENDELEZO wa kiwango anachokionyesha winga wa Simba, Luis Miquissone umetafsiriwa na wadau wa soka kuwa, unatokana na kutoridhika na mafanikio anayoyapata, hajalewa sifa pamoja na kujipambanua anataka nini katika majukumu yake ya soka.

Mwanaspoti limezungumza na wadau mbalimbali kwa nyakati tofauti, walitoa mitazamo yao na kuwataka wachezaji wengi kuiga ili kuipa thamani Ligi Kuu Bara kuwa na ushindani utakaotoa vipaji bora.

Nahodha wa zamani wa timu hiyo, Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema kitu cha tofauti alichokiona kwa Luis tofauti na maproo wengine kuwa ni mchezaji asiyeridhika na anashawishi mashabiki kwenda kumuangalia kila anapokuwa na majukumu ya mechi.

“Mastaa wenzake wa kigeni wanajitambua lakini wanafika hatua ya kuridhika, Luis kila anapocheza anakuwa na jambo jipya, haridhiki licha ya kila mdau wa soka kumuamini kiwango chake na kuona kipaji alichonacho, haijamzuia kupambana kadri anavyoweza, hii inaonyesha dogo anamanisha kuja kufanya kazi Tanzania na sio kuja kushangashangaa jiji ambalo linawapoteza wengi kwa starehe,” alisema Mgosi na kuongeza;

“Luis ana vitu vingi anajua kukaba, kushambulia, kutoa pasi na anafunga vilevile, vitu hivyo ni adimu kwa wachezaji wengi, lakini bado anang’ang’ana kuendelea kuonyesha uwezo wa juu tangu ajiunge na Simba na ndio maana timu za mataifa mengine zinamtupia jicho sio kwa kumpendelea, bali kinachowavuta ni kazi zake.”

Mshambuliaji wa zamani wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma alisema Luis ni mchezaji asiyelewa sifa na kwamba kazi yake inaonyesha kwamba kuja kucheza Tanzania ni kama daraja la kutaka mambo makubwa zaidi.

“Wachezaji wengi wanalewa sifa wapokuwa midomoni mwa mashabiki hasa wa hizi timu za Simba na Yanga, ila ninaona Luis ameamua kujiweka kando nakufanya kazi iliyomleta, hilo litaendelea kumpa thamani yake kuwa juu na timu itakayomtaka kumpa mamilioni mengi, hilo liwaamshe wazawa wana vipaji lakini wanaishia kulewa sifa, wanapopita mtaani wanajiona wao ndio wao.”

Naye kocha wa Gwambina, Mohammed Badru alisema kwa namna ambavyo Luis alivyo na muendelezo wa kiwango chake, anaweza akacheza timu yoyote Afrika na akafanikiwa kupenya Ulaya, jambo kubwa aliloliona kwake ni nidhamu ya kazi.

“Nidhamu inawafelisha wengi, anapokuwa na nafasi ya kufanya jambo anakuwa anajisubilisha, bila kujua kwamba kuna watu wengi wenye taluma kama yake wanatamani nafasi hiyo, lakini mchezaji huyo amejipambanua na kujua soka linataka nini, ameliheshimu linamuheshimu,” alisema.

ALICHOFANYA

Luis ni mchezaji panga pangua chini ya Kocha Didier Gomes, hadi sasa ametoa asisti tisa za mabao, anamiliki mabao sita na kuasisti tisa katika Ligi Kuu, wakati michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (Caf) alifunga mabao matatu.

Aliwahi kukaririwa alipofananishwa na Lionel Messi kutokana na aina ya uchezaji wake, alieleza kwamba anataka kuwa Luis na sio mwingine, jambo linalompa kupambana zaidi ili kuacha alama yake katika ulimwengu wa soka.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz