Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mganda Tabora United afunguka kuiua Prisons

Bernad Nakibinge. Bernad Nakibinge.

Thu, 21 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Winga Mganda wa Tabora United, Bernad Nakibinge amesema siri ya ushindi wa kwanza kwenye Ligi Kuu Bara ni maelewano mazuri yaliyopo kikosini ya wachezaji na benchi la ufundi pamoja na kumsoma vyema mpinzani.

Mchezaji huyo alifunga mabao mawili kwenye ushindi wa 3-1 ilioupata timu hiyo dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa ligi uliopigwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Ushindi huo ni wa kwanza kwa timu hiyo baada ya kucheza mechi tatu ikifungwa na Azam 4-0 na suluhu dhidi ya Singida Big Stars, huku ikivuna pointi nne na kukamata nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Nakibinge aliyefunga mabao hayo katika dakika za 42 na 90 huku lingine likipachikwa na Erick Okutu, alisema ni jambo la faraja kuanza kufunga na kuisaidia timu baada ya kuwa na mwanzo mbaya kwenye ligi kwani anatamani kuisaidia kufanya vizuri baada ya kuwepo tangu msimu uliopita. “Tulitumia makosa waliyofanya wenzetu tukapata mabao na ushindi wetu wa kwanza kwenye ligi,” alisema.

“Nashukuru kwa jinsi ambavyo tunacheza kwa kuelewana na wachezaji wenzangu, wamenisaidia nimefunga mabao mawili.

“Mechi ilikuwa nzuri tulikutana na timu nzuri yenye wachezaji wazuri ambao ni wazoefu wa ligi, lakini sisi ni wageni kwa hiyo tumewaheshimu vizuri, tulitumia nafasi ambazo tulipata na Mungu katusaidia tumepata ushindi,” alisema Nakibinge

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Bernad Fabian alisema benchi la ufundi linaridhishwa na maendeleo ya kikosi baada ya mechi tatu za ligi huku akitamba kuwa kadri mechi zinavyoendelea watazidi kuimarika na kufanya vizuri.

“Mchezo ulikuwa mzuri tulifanikiwa kwa mpango wa mechi ambao tulikuwa nao, tuliwaona Tanzania Prisons na tukaenda uwanja wa mazoezi kufanyia kazi mapungufu yao,” alisema.

Katika mechi ya ufunguzi, timu hiyo ilifungwa na Azam FC 4-0 mchezo ulioishia kuvunjika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live