Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfahamu Shekhan koungo mpya wa Yanga

Shekhan 23 12 16 At 14 Mfahamu Shekhan koungo mpya wa Yanga

Sat, 16 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shekhan Ibrahim Hamis, mwenye umri wa miaka 18 ambaye ni mchezaji mpya wa kikosi cha Yanga SC, amefunguka juu ya safari yake kisoka.

Nyota huyo mwenye uwezo mkubwa wa kucheza nafasi ya kiungo wa kati na winga, amejiunga na Yanga SC katika usajili huu wa dirisha dogo akitokea JKU Zanzibar.

Hivi karibuni, Shekhan alikuwa na kikosi cha timu ya taifa ya Zanzibar chini ya miaka 18, kilichoenda kushiriki mashindano ya CECAFA U18 nchini Kenya.

HISTORIA YAKE “Historia yangu kisoka ilianzia akademi, nilikaa kama miaka sita nikiwa akademi, nikaenda mashindano ya Copa Coca Cola Mtwara, kurudi tukaenda tena mashindano pale Karume, nikaonekana, nikarudi kuna timu nikatolewa kwa mkopo, timu inaitwa Makundi City ipo Ligi Daraja la Kwanza Zanzibar, nilienda dirisha kubwa, nikacheza nusu msimu, JKU wakanirudisha, wakanipandisha timu kubwa.

“Nikacheza msimu wa kwanza, Mungu alinijaalia nikakosa mechi kama tatu kwa msimu mzima.

ABADILISHWA NAFASI “Nikaenda msimu wa pili ambapo alikuja kocha mpya, nilikuwa nikicheza winga, akaniambia anataka kunijaribu namba nane kuniangalia kama ninaweza kucheza.

“Bahati nzuri tukaja Dar, tukacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Dodoma Jiji, ile namba moyoni mwangu haikuwepo, kocha akaniambia anataka kunijaribu nicheze hapo dhidi ya Dodoma Jiji.

“Nikacheza, bahati nzuri Mungu akanijaalia ile namba ikanikubali na mimi mwenyewe mwisho nikaikubali, kocha akaniambia umeona namba uliyokuwa huitaki, lakini nimekuchezesha umecheza vizuri na watu wote wamekuangalia, nikamwambia sawa, nimekubali kucheza namba hii.

“Tukaenda mechi nyingine dhidi ya Singida pale Chamazi, ile mechi tulipoteza, lakini kwa bahati nzuri nilicheza vizuri, kocha akaniambia sasa hivi nataka nikuweke hapo.

“Tukarudi Zanzibar, tukacheza Ngao ya Jamii, nikawa kivutio cha watu, nikimaliza kucheza watu wananifuata kunipa ushauri, nikakubali na kusema sasa natakiwa kucheza mpira unisaidie kimaisha.

“Ikatokea nafasi ya kucheza timu ya taifa na kwenda Kenya, wadau wengi wakawa wananiambia hii timu wewe ndiye utaisaidia na wewe utakuwa mshauri kwa wenzio.

“Kocha wa timu ya taifa ndiye yule kocha wangu aliyenifundisha wakati nilipoenda kwa mkopo Ligi Daraja la Kwanza (Makundi City), ananijua vizuri.

“Katika mfumo wake timu ya taifa, akaniweka namba sita, mechi ya kwanza tukacheza, ya pili mpaka ya tatu, tukakaa kikao, tukamwambia kocha hii mechi ngumu ambayo inatakiwa tushinde ndiyo tupite.

“Nikamwambia kocha mimi naweza kuisaidia timu, nataka kucheza kutokea pembeni, kocha akasema ameusikia ushauri wetu, lakini akatuambia kwa mfumo wake, lazima mimi nicheze namba kumi.

“Wakati wa mechi, dakika za mwanzo yule aliyepangwa winga akaumia, akaingizwa kiungo, mimi nikaenda kucheza pembeni mpaka mechi inaisha, kwa bahati mbaya mechi tukapoteza, tukarejea Zanziabar.

AJIUNGA NA YANGA SC “Tuliporudi Zanzibar, nikaja kupata fursa kama hii (kujiunga na Yanga SC).

“Kwanza nashukuru na nimefurahi kupata fursa kama hii kama mchezaji ambaye bado mdogo. Namshukuru Mungu nimepata fursa hii, kwa uwezo wa Mungu nitajitahidi kuhakikisha ninapata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza,” anasema kiungo huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live