Ni kocha asiyependa mambo ya kupindapinda. Yaani hapendi mbambamba kwenye mipango yake. Ukizungua naye anakuzingua, ila ni fundi wa mpira ambaye kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litaamua kupiga naye kazi bila konakona, anaweza kuipaisha Tanzania katika anga la kimataifa.
Ndio, namzungumza kocha mkuu mpya wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars Adel Amrouche, aliyetangazwa juzi kuchukua nafasi ya Kim Poulsen aliyetimuliwa kibaruani tangu Agosti 29, 2022 baada ya Stars kulala 1-0 nyumbani na Uganda The Cranes katika mechi za kusaka fainali za CHAN.
Mara baada ya Kim kutimuliwa nafasi ilikaimiwa na Honour Janza kutoka Zambia aliyekuwa akiinoa Namungo iliyopo Ligi Kuu Bara kabla ya kutimka kurudi kwao alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu ya Zesco United inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini humo.
TFF kupitia Kurugenzi ya Ufundi chini ya Oscar Mirambo iliendesha mchakato wa kusaka kocha mkuu wa Stars na hatimaye juzi Jumamosi mchana ilimtangaza Amrouche, kocha mwenye mzoefu mkubwa na soka la Afrika akiwa pia ni Mkufunzi wa makocha kutoka CAF.
Tunakuletea dondoo chache za kocha huyo raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Algeria aliyewahi kuzinoa timu mbalimbali za taifa pamoja na klabu za soka barani Afrika na Mashariki ya Kati, huku akiacha kumbukumbu nchini Kenya ya kuliburuza hadi Fifa Shirikisho la Soka (FKF).
UZOEFU MKUBWA
Amrouche ana uzoefu mkubwa na soka la Afrika baada ya kufundisha klabu na timu za taifa katika ukanda wa Kusini, Mashariki Kati na Kaskazini.
Amewahi kuwa Kocha Bora wa Afrika Mashariki mwaka 2013 wakati akiinoa na kuipa Kenya, Harambee Stars ubingwa wa michuano ya Kombe la Chalenji na kabla ya hapo alifika nusu fainali mara mbili akiwa na kikosi cha Burundi.
Akiwa na Harambee Stars, Amrouche aliweka rekodi ya kucheza michezo 20 bila ya kupoteza huku pia akiwahi kuzifundisha timu mbalimbali za taifa za Equatorial Guinea, Botswana, Libya na Yemen.
Wakati akiifundisha timu ya DC Motema Pembe aliiwezesha kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ameweza kuipa ubingwa mara mbili wa DR Congo na DRC Super Cup.
Uzoefu mwingine kwa klabu kwa Amrouche amezifundisha timu za RC Kouba, USM Alger ambazo amewahi kuzichezea na MC Algiers zote za Algeria.
Amrouche anayezungumza lugha ya Kiswahili, Kiarabu, Kifaransa na Kiingereza kwa nyakati tofauti amewahi pia kuwa Mkurugenzi wa Ufundi na Michezo katika klabu za Ubeligiji na Ukraine huku akiwa na UEFA pro Licence.
Kocha huyo mwenye Shahada ya Uzamili katika kuwasoma watu na utimamu (Masters in Ergonomics in Physical Activity) amefanya kazi za ukufunzi kwenye Shirikisho la Soka Afrika (CAF) katika kuzalisha walimu wa soka.
FALSAFA YAKE
Kocha Amrouche ni muumini wa soka la pasi nyingi maarufu kama soka la kitabuni linalotandaza mpira chini zaidi kuliko kutubua hovyo, mfumo ambao kwa mashabiki wa soka wa Tanzania wanapenda kuita soka biriani.
Anatumia zaidi mfumo wa 4-2-3-1 ambao unaifanya timu inapopoteza mpira kuwa na wachezaji sita wanaokaba na inaposhambulia inakuwa na wachezaji sita pia. Anapenda zaidi kumtumia straika moja huku akiwa na mawinga wenye kasi.
Mfumo uliyowasumbua Wanaigeria walipocheza na Harambee Stars katika fainali ya Chalenji 2013 iliyowapa Wakenya ubingwa waliousotea kwa miaka karibu 11.
Kwa aina ya wachezaji iliyonayo Tanzania ni wazi itawapa nafasi kubwa vijana wenye kasi kuiendesha timu huku nahodha Mbwana Samatta au John Bocco kusimama mbele kwa ajili ya kutupia mipira kambani.
HATAKI UTANI
Kocha Amrouche pia ni kocha asiyependa mzaha kazini, kitu ambacho kwa wachezaji wavivu na wanaofanya mambo kwa mazoea wanaweza wasimuelewe, ila ni mtu mzuri sana kwa wanaofuata maelekezo yake.
Ni kocha matata na mwenye misimamo mikali ambaye ukimzingua kidogo unazinguana naye na FKF wanakumbuka walipomfuta kazi kienyeji mwaka 2014 na namna alivyowachachafya kiasi cha kukaribia kufungiwa na FIFA baada ya kuwashtaki akitaka kulipwa fidia ya kuvunjiwa mkataba.
Mbelgiji huyo alipotangazwa kutimuliwa alionekana kukerwa na uongozi wa FKF kwa kushindwa kumlipa malimbikizo ya mshahara wake wa miezi mitatu na hivyo kwenda kushtaki Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa ya Michezo (CAS) iliiagiza shirikisho hilo la Kernya kumlipa Sh109 milioni (zaidi ya Sh 1 bilioni za Kitanzania).
Amrouche pia aliwahi kusimamishwa na Shirikisho la Soka la CAF 2014 kwa muda wa miezi sita kwa kosa la kumtemea mate afisa mmoja aliyekuwa miongoni mwa wale waliosimamia mechi ya Harambee Stars dhidi ya Comoros. Kifungo hicho ndicho kilichowazi kuzaa bifu lake na Rais wa FKF enzi hizo, Nick Mwendwa aliyekuwa akimzungusha kumlipa.
Licha ya kudai kiasi hiki kikubwa cha fedha, Amrouche hakutaka kuona Harambee Stars inakosa kushiriki michuano ya kimataifa hivyo akawaagiza mawakili wake kuhakikisha wanatengeneza njia Harambee Stars kucheza mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2022.
Lengo la Amrouche kuchukua hatua hiyo ni kwamba asingependa kuona anakatisha ndoto ya baadhi ya wachezaji aliowakuza kisoka jambo analosema angeishi kujutia maishani mwake.
Alisisitiza atapambania haki yake lakini hatawaruhusu FIFA kuchukua maamuzi magumu dhidi ya Kenya kutokana na makosa ya mtu moja.
“Kwangu mimi naleta uhai na sio kifo au kitu kingine, hivyo nitatafuta njia mbadala kudai haki yangu na kuruhusu wachezaji wa Harambee Stars kufukuzia ndoto zao za kufuzu Qatar 2022. Nabaki kuwa shabiki wa Kenya. Nataka waende umbali na vipaji vyao vitawafikisha,” alikaririwa Amrouche.
Amrouche aliongeza alichelewesha kuruhusu FIFA kushusha rungu lake dhidi ya Kenya ili kuipa nafasi Harambee Stars icheze Kombe la Afrika 2019 nchini Misri na haya yote yanatokana na mapenzi yake kwa Kenya.
KAZI KWAKE
Amrouche ametua Stars ikikabiliwa na kibarua kigumu cha kuivusha kwenda fainaliza Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, zitakazofanyika mwakani nchini Ivory Coastal, ikiwa Kundi F na timu za Uganda, Niger na Algeria.
Stars inakabiliwa na mechi ngumu mbili za kundi hilo dhidi ya Uganda zitakazopigwa ndani ya mwezi huu, ikianzia ugenini Machi 24 kabla ya kurudiana Machi 28, mechi zitakazotoa taswira ya timu hiyo kwenda Ivory Coast au ndio itakuwa ‘Asante na kwaheri’ kama ilivyokuwa katika CHAN.
Timu hiyo hadi sasa ina pointi moja tu katika mechi mbili za awali, ikifungwa na Algeria kwa mabao 2-0 baada ya awali kutoka sare ya 1-1 ugenini mbele ya Niger. Stars inatakiwa kushinda mechi hizo ili kufufua matumaini ya kwenda Afcon kwa mara ya tatau baada ya kufanya hivyo awali mwaka 1980 na 2019.
Hivyo kwa sasa kocha huyo aliyepewa mkataba wa miaka mitatu na atakayekuwa akilipwa na serikali anapaswa kuita wachezaji watakaombeba kwenye mechi hizo dhidi ya Uganda za Cranes ambayo ndio iliyosababisha Kim Poulsen kutemeshwa kibarua baada ya kuchapwa 1-0 kabla ya Janza kwenda kumalizia mechi ya marudiano kwa kichapo cha mabao 3-1 na kuaga michuano hiyo.
Kupoteza mechi hizo itakuwa na maana mechi mbili za kukamilisha ratiba dhidi ya Niger na vinara Algeria hazitakuwa na maana yoyote, hasa kama wapinzani wengine wa kundi hilo wataendelea kukusanya pointi katika michezo yao kabla ya Juni na Septemba mwaka ambao itakuwa funga dimba.
AMROUCHE NI NANI?
Kocha huyo alizaliwa Machi 7, 1968, Kouba jijini Algiers na alianza kucheza soka tangu utotoni akimudu nafasi ya kiungo na klabu zilizomtangaza zikiwa ni CR Belouizdad aliyoichezea kati ya 1983-1985 kisha kutua JS Kabylie (1985-1988).
Kuanzia 1988-90 alikipiga OMR El Annaser kisha kutua USM Alger (1990-91) na kurudi tena OMR na mwaka 1992-993 aliichezea Favoritner AC kisha La Lauviere nksiha Mons kabla ya kugeukia ukocha akifanya kazi Ubelgiji katika klabu ya FC Brussels kama Mkurigenzi wa Ufundi 1995-1996.
Klabu nyingine alizofanya nazo kazi ni R.U Saint Gilloisse, DC Motema Pembe, FC Volyn Lutsk, FK Genclerbirliyi, USM Alger na MC Alger, huku kwa timu za taifa amezinoa Guinea ya Ikweta, Burundi, Kenya,. Libya, Botswana na hadi anakuja Tanzania alikuwa kocha wa Yemen.
Mafanikio makubwa ni kubeba Kombe la Chalenji 2013 akiwa na Harambee ya Kenya na ubingwa wa Ligi Kuu ya DR Congo pamoja naSuper Cup la nchi hiyo akiwa na DC Motema Pembe.