Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Messi awagaragaza tena Mbappe na Benzema Ufaransa

Messi Best FIFA Messi awagaragaza tena Mbappe na Benzema Ufaransa

Tue, 7 Mar 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Supastaa, Lionel Messi anaendelea tu kukusanya tuzo zake. Muargentina huyo, anayekipiga kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain, usiku wa juzi Jumatatu alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa Fifa inayofahamika kama “Fifa Best” katika sherehe zilizofanyika Paris, Ufaransa.

Messi, 35, alinyakua tuzo hiyo baada ya kuiongoza Argentina kushinda taji lao la kwanza la Kombe la Dunia tangu mwaka 1986 walipofanya hivyo huko Qatar, Desemba mwaka jana na hivyo tuzo hiyo ya Fifa ni ya pili kwake kuwa bora duniani.

Messi, ambaye alifunga mara mbili katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia 2022 dhidi ya Ufaransa, alishinda pia Mpira wa Dhahabu katika fainali hizo za Qatar baada ya kutajwa kuwa mchezaji bora wa Kombe la Dunia, huku akiwa ametokea kubeba taji la Ligue 1 na kikosi chake cha PSG.

Mabao yake 12 kwenye ligi msimu huu yameisaidia mabingwa hao watetezi wa Ligue 1 kukaa kileleni kwa msimamo kwa tofauti ya pointi nane na hivyo kujiweka kwenye wakati mzuri wa kunyakua tena taji hilo mwaka huu.

Messi, ambaye kocha wake wa Argentina, Lionel Scaloni alitajwa kuwa kocha bora wa mwaka wa Fifa akimbwaga Pep Guardiola, alimpiku mchezaji mwenzake wa PSG, Kylian Mbappe na mkali wa Real Madrid, Karim Benzema katika tuzo hiyo baada ya watatu hao kuingia kwenye fainali ya kuwania tuzo bora ya Fifa kwa upande wa wachezaji wa kiumbe.

Messi sasa ameshinda tuzo mbili za ubora za Fifa, hivyo anamfikia straika Robert Lewandowski na mpinzani wake wa miaka tele, Cristiano Ronaldo, ambao pia walishinda tuzo hiyo mara mbili.

Na sasa mkali huyo wa zamani w Barcelona sasa ameshinda tuzo kubwa binafsi mara 10 ikiwamo ya FIFA Best, Ballon d’Or na mchezaji bora wa mwaka wa FIFA, akiwa amemzidi Ronaldo kwa tuzo mbili.

Mwenyewe alisema hivi: “Ni furaha kubwa kuwa hapa, sambamba na Benzema na Mbappe, ambao wamekuwa na mwaka mzuri. Ulikuwa mwaka mzuri kwangu na nilifikia ndoto zangu ambazo nilikuwa nazikimbizia kwa muda mrefu. Nataka kuwashukuru wachezaji wenzangu na kocha wangu, bila ya wao nisingekuwa hapa.”

Waliohudhuria sherehe hizo za utoaji wa tuzo alikuwamo pia mke wa Messi, mrembo Antonela pamoja na mastaa wengine kibao.

Kylian Mbappe aliandamana na baba yake Wilfried na fowadi huyo wa PSG alichaguliwa kwenye Kikosi Bora cha Kwanza cha Dunia cha Wanasoka wa kulipwa FIFPRO, sambamba na Messi, lakini hakufua dafu kwa mchezaji mwenzake kwenye tuzo hiyo, ambaye pia alimshinda kwenye fainali ya Kombe la Dunia 2022, licha ya kwamba alifunga hat-trick katika mchezo huo.

Mastaa wa Ligi Kuu England waliokuwapo kwenye tuzo ni kipa wa Aston Villa, Emi Martinez - ambaye alishinda tuzo ya Kipa Bora, kiungo wa Manchester United, Casemiro na beki wa kati wa Liverpool, Virgil van Dijk, ambao wote walitajwa kwenye kikosi bora cha mwaka 2022, na wote walihudhuria wakiwa na wake zao.

Kwa upande wa soka la wanawake, kocha wa England, Sarina Wiegman na mkali wa Manchester United, Mary Earps walishinda tuzo ya kocha bora na kipa bora mtawalia baada ya mafanikio yao makubwa kwenye Euro 2022 majira ya kiangazi mwaka jana.

Earps alisema: “Sijui hata cha kusema, nawashukuru mlionipigia kura. Najiona ni mwenye kuheshimiwa kwa kushika tuzo hii nzito. Nataka kuwashukuru wapendwa wangu wote mlionisaidia kunitoa jikoni na kunifikisha hapa.”

Wiegman, alishinda tuzo hiyo kwa mara ya tatu na aliongeza: “Euro ilikuwa safi na kama Waingereza wanavyosema tumerudisha nyumbani.”

Wakati huo huo, Beth Mead alibwagwa na Alexia Putellas kwenye tuzo ya ubora kwa upande wa wanawake, lakini alikuwamo katika kikosi bora cha mwaka cha timu ya wanawake, sambamba na wachezaji wenzake watatu wa Lionesses, Lucy Bronze, Leah Williamson na Keira Walsh.

Majina mengine makubwa ya mastaa waliohudhuria sherehe hizo za Paris ni gwiji wa Brazil, Ronaldo, Muivory Coast, Didier Drogba, Mfaransa Arsene Wenger, Mreno Joao Cancelo na rais wa FIFA, Gianni Infantino.

Staa za zamani wa Newcastle United na England, Jermaine Jenas alikuwa mtangazaji wa sherehe hizo. Kama ilivyotarajiwa na wengi, Messi alikuwa na usiku bora kabisa na amezidi kuendelea kung’ara kwenye soka, ambapo tangu kuanza kwa msimu huu wa 2022-23 amefunga jumla ya mabao 17 na kuasisti mara 16 katika mechi 28 alizochezea PSG.

Ameendelea kuwa kwenye kiwango bora tangu mwaka 2023 ulipoanza na Jumapili iliyopita mkali huyo alifunga bao lake la 700 katika ngazi ya klabu, wakati alipofunga moja kwenye mechi ya ushindi wa mabao 3-0 iliyopata PSG dhidi ya Marseille na aliasisti mabao yote yaliyofungwa na Mbappe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: