Supastaa, Lionel Messi ameamua kuitoa tuzo yake ya nane ya Ballon d’Or na kuiweka kwenye makumbusho ya klabu ya Barcelona licha ya kwamba alishinda akiwa ameshahama kwenye timu hiyo.
Muargentina huyo tuzo zake saba za kwanza za Ballon d’Or alizibeba akiwa kwenye kikosi hicho cha miamba ya La Liga yenye maskani yake Nou Camp. Aliondoka Nou Camp mwaka 2021 baada ya Barcelona kuripotiwa kuwa na ukata wa kifedha na staa huyo alikwenda kujiunga na PSG bure.
Katika msimu wake wa mwisho Ufaransa, Messi alishinda Ligue 1 na kuiongoza Argentina pia kushinda ubingwa wa Kombe la Dunia 2022 huko Qatar.
Messi alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa fainali hizo baada ya kusaidia timu yake kuichapa Ufaransa kwenye fainali, mchezo ambao ulimshuhudia Kylian Mbappe akifunga hat-trick kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Dunia.
Majira ya kiangazi 2023, alijiunga na Inter Miami na alikabidhiwa kitambaa cha unahodha na kuwaongoza kushinda Kombe la Ligi. Mafanikio hayo kwa jumla yake yalimfanya ashinde tuzo ya Ballon d’Or na kuweka rekodi akinyakua kwa mara ya nane na kuwa wa kipekee duniani.
Lakini, badala ya kubaki na tuzo hiyo, au kuipeleka PSG, Messi aliamua kuipeleka Barca ikawekwe kwenye makumbusho ya timu hiyo ikiwa kama shukrani ya kushinda tuzo za aina hiyo mara saba alipokuwa kwenye kikosi hicho cha Nou Camp.
Messi alimbwaga Erling Haaland wakati anatwaa tuzo yake ya nane ya Ballon d’Or, huku Mbappe alimaliza kwenye nafasi ya tatu.