Wenzetu wazungu wako makini sana katika suala la nidhamu na wanalipa uzito mkubwa.
Unapokosea haijalishi wewe ni nani na una ustaa kiasi gani au una kipaji gani, watakuchukulia hatua kwa mujibu wa utaratibu waliojiwekea.
Ni nadra kuona wenzetu wazungu wakiacha kumshughulikia mchezaji ambaye anafanya kitendo cha utovu wa nidhamu kwani wanaamini kwa kufanya hivyo, wanaweza kutengeneza sumu ambayo itaathiri timu nzima hapo baadaye.
Na mfano si mmesikia kilichotokea kwa mchezaji bora wa dunia, Lionel Messi ambaye kakutana na rungu huko kwenye klabu yake ya PSG kutokana na utovu wa nidhamu alioufanya?
Jamaa pasipo kupewa ruhusa yoyote na klabu yake, aliamua kuichukua familia yake na kuelekea Saudi Arabia kwa mambo yake binafsi sasa waajiri wake wakaamua kumshughulikia kwa kumfungia kwa wiki mbili.
Wanajua ni mchezaji muhimu kikosini, anafunga mabao, anapiga pasi nyingi za mwisho na akiwepo uwanjani thamani ya klabu inazidi kuwa kubwa lakini wamemfungia. Kwa nini?
Ni kwa sababu ya kuwafanya wengine wasirudie alichokifanya siku za usoni na kuiathiri timu.
Sasa wakati wenzetu wakimfungia mchezaji kama Messi, huku kwetu mambo yangekuwa tofauti iwapo mchezaji staa na tegemeo kwenye timu anafanya kosa kama hilo.
Zingetumika njia nyingi za kumsafisha mbele ya mashabiki na kujaribu kuficha kosa alilofanya ilimradi tu timu iweze kumchezesha katika mechi zilizo mbele. Mara utasikia mchezaji alikuwa na matatizo ya kifamilia, au wako tayari hata kusema timu ilimpa ruhusa maalum.
Mfano mzuri ni yule straika tegemeo wa ile timu pale Kariakoo. Kabla ya mechi moja ya kimataifa aliamua tu kususa na kutokwenda mazoezini kisa anadai hela halafu akarudi siku moja kabla ya mechi na bado akapangwa.
Ukiondoa huyo, kuna mwingine yupo timu nyingine ya Kariakoo sasa hivi hachezi mara kwa mara wakimtetea kuwa ana majeruhi lakini kiuhalisia jamaa kamezwa na ulevi unaopelekea hadi ashindwe kutokea mazoezini.