Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Messi alivyoboresha afya duniani

La Pulga Pic Mashabiki wa Argentina

Fri, 23 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Hatimaye Lionel Messi ‘La Pulga’ ndiye mchezaji aliyefanikiwa kubeba kila kitu katika soka na anamaliza ubishi wa siku nyingi kuwa nani ndiye G.O.T katika soka. Kirefu chake ni Greatest Of All Time yaani mshindi wa muda wote.

La Pulga, Lionel Andreas Messi ndiye mchezaji bora kuliko yeyote katika fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar baada ya kuisaidia Argentina kutwaa Kombe la Dunia. Fainali hizo zilifikia tamati Desemba 18, 2022 kwa ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Ufaransa.

Ilikuwa ni Messi dhidi ya Kylian Mbappe wa Ufaransa kila goli au shambulizi ni majina hayo ndiyo yaliyotawala vinywani mwa watangazaji.

Katika mechi ya nusu fainali kati ya Argentina na Croatia mtangazaji alisema katika dunia kuna maajabu saba, lakini hapa kuna ajabu la nane ambalo ni Messi.

Mtangazaji alisema hivyo wakati Messi akitoa pande la bao la pili la ushindi lililofungwa na Julian Alvarez baada ya kumhadaa beki wa Croatia kutoka katikati ya uwanja na kumuingiza ndani ya boksi na hatimaye kutoa pasi.

Mbappe aliibuka mfungaji bora wa mashindano, lakini macho na masikio yalikuwa zaidi kwa Messi ambaye ndiye mchezaji bora wa akiwa na umri wa miaka 35. Umaarufu wake huu katika soka ulisababisha mamilioni ya wadau mashabiki, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa na kiu ya kuona nini atafanya katika fainali.

Uwezo wake haukuongopa. Ulikuwa ni wa hali ya juu kiasi cha kutoa mchango wa kutwaa taji hilo limeweza kuwapa faraha wale wote waliotaka kumuona akifanikiwa. Furaha aliyowapa La Pulga mashabiki wa Argentina na wengine duniani imeweza kuwapa hisia chanya ambayo kitabibu imeboresha afya za mamilioni ya mashabiki duniani.

Katika fainali hiyo alitupia mabao mawili huku pasi yake ya madaha ilikuwa chanzo cha kupatikana kwa pasi nyingine iliyozaa bao la pili.

Kufanikiwa kupata ushindi katika hatua ya penalti kulifanya kulipuka kwa furaha kubwa kwa mamilioni ya mashabiki wakiwamo wenye matatizo ya akili ikiwemo huzuni kwa upande mwingine. Mpira ni burudani, lakini unaleta uchungu na furaha, na kwa wanaomshabikia La Pulga walipata hisia ya furaha ambayo inaboresha afya ya akili.

Nchini Argentina palikuwa na hekaheka za wazee kwa vijana, lakini la kuvutia ni moja ya picha za video ilionyesha moja ya hospitali wagonjwa wakifuatilia mechi hiyo kwa umakini kama vile wamepona. Wagonjwa hao waliokuwa katika viti vya kusukuma walifurahi na kuchangamka kama vile wamepona.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), afya njema maana yake ni ukamilifu wa binadamu kimwili, kiakili na kijamii na kutokuwepo kwa maradhi mwilini. Soka ni moja kati ya mchezo unaoshika namba moja duniani kwa kupendwa, hivyo kupata furaha kutoka kwa La Pulga ni faida kubwa kwa afya ya mwili.

TIBA KWA SABABU HIZI

Furaha iliyosababishwa na La Pulga imeboresha afya ya m watu wanaompenda soka kwa mujibu wa tafiti za kiafya kufurahi kunaongeza siku za kuishi.

Inaelezwa kwa sababu hali ya furaha inaondoa hisia hasi ambazo ndizo chanzo cha magonjwa ya moyo na akili ikiwamo shinikizo la akili na sonona kitabibu huitwa depression.

Furaha ni hisia chanya ambayo huambatana na kutiririshwa kwa vichochezi ambavyo vinaleta hisia nzuri ukilinganishwa na uchungu ambao unasababisha shinikizo mwilini. La Pulga ana mamilioni ya wafuasi ambao wanamfuatilia katika mitandao ya kijamii, na furaha kama ile hata kama mtu ana mawazo hasi yaliyomganda yatapeperushwa na kile alichompa.

Ni kawaida binadamu anayekuhusudu sana vilevile kuumizwa kirahisi ukilinganisha ni binadamu asiyehusudu. Ni dhahiri kama Messi angelikosa mafanikio yale, basi wafuasi wake wengi wangeumia kihisia. Na mbaya zaidi katika soka hutokea mpasuko wa hisia kwa ghafla na ndio maana watu hupoteza fahamu.

Hakuna mafanikio yasiyo na uchungu. Itakumbukwa kuwa katika mechi ya ufunguzi mabingwa hawa walipokea kipigo cha mabao 2-1 na Saudi Arabia.

Hii iliwaumiza mashabiki wa Messi ambao waliona timu hiyo katika mashindano si lolote. Wengi waliokuwa na mpasuko wa hisia walianza kupona kwani ni Messi huyohuyo ambaye kila mechi alikuwa anatupia mabao hatimaye kutibu hisia hasi za mashabiki.

Inaelezwa kile kizazi cha Diego Maradona ambacho kilishuhudia gwiji akilibeba kombe hilo 1978 na 1986 wengi ni wazee wakiwa na shida za kiafya kutokana na umri mkubwa. Wengi wa kizazi hicho walikuwa na matatizo ya kiafya ya kiakili ikiwamo hofu, huzuni na sonona lakini kadri timu hiyo ilivyokuwa ikivuka kila hatua ndivyo pia iliwapa furaha.

Kizazi hicho cha dhahabu ambacho kinaelekea ukingoni kinadaiwa kujiona kama ni wapya kwani zawadi aliyowapa Messi imetibu matatizo mengi ya kiafya ikiwamo sonona. Wanasema kuwa wangeumia kama wangelikosa kombe hilo. Wanajiona ni wenye bahati kubwa kutokana na kulibeba kombe hilo mara ya pili wao wakiwa wazee.

Wengine wanasema hawadhani kama wataweza kuona fainali nyingine ya Kombe la Dunia 2026 kwani umri umewatupa mkono na wanazongwa na magonjwa ya uzeeni yasiyoepukika.

Lionel Andreas Messi ‘La Pulga’ au ‘The G.O.T’ ndiye aliyeboresha afya za mamilioni ya mashabiki duniani kote, alishatangaza kutundika daluga lakini hatimaye ameghairi.

Staa huyo amesema ataendelea kuitumikia Timu ya Taifa ya Argentina.

Chanzo: Mwanaspoti