Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Messi, Neymar na Ronaldo sababu Ligi Ufaransa kudoda

Lionel Messi 1692504890 114379 Messi, Neymar na Ronaldo sababu Ligi Ufaransa kudoda

Tue, 24 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Shirikisho la Soka Ufaransa (LFP), limesitisha kwa muda mchakato wa kutafuta mzabuni wa haki za matangazo ya runinga ya Ligi Kuu ya nchi hiyo (Ligue 1) kutokana na mwitikio usioridhisha.

Mpango wao ulikuwa kupata Dola 1 bilioni za Marekani kwa mwaka mmoja katika kipindi cha miaka mitano ijayo kuanzia 2024 hadi 2029.

Matarajio yalikuwa kuona wazabuni wa sasa waanzishe vita vya panzi ili kunguru apate faida. Wazabuni hao ni Amazon Prime Video, Canal+, BeIN Sports na DAZN.

Lakini ikawa kinyume chake, Amazon na Canal+ wakala kabunyau na kuwaacha DAZN na BeIN wajitose peke yao. Hata hivyo na wao madau yao yalikuwa madogo chini ya makadirio ya LFP.

Inasemekana DAZN inatunza misuli ya kifedha kwa ajili ya kuingia vita vya kuwania kupata haki ya kuonyesha Ligi Kuu England (EPL), huku BeIN ikitaka kuendelea na dau lilelile la mkataba wa sasa unaokwisha msimu huu.

Na Canal+, kituo cha kulipia cha Ufaransa hakina nia kabisa ya kununua haki za ligi ya Ufaransa baada ya mkataba wa sasa kumalizika.

MESSI NA NEYMAR

Ujio wa Lionel Messi kwenye Ligue 1 mwaka 2021 uliongeza mvuto na kusababisha thamani ya ligi hiyo kupanda. Amazon walilipa Euro 825 milioni (takriban Dola 1 bilioni) kununua haki ya matangazo kwa kuivua kampuni ya Mediapro ya Hispania.

Amazon ambao huonyesha mechi kwa intaneti walikimbilia ligi hiyo wakiamini ujio wa Messi na uwepo wa nyota wengine kama Neymar utasababisha watu wengi kuifutilia ligi hiyo.

Ujio wao kwenye kuonyesha Ligue 1 kukawakera Canal+ ambao walikuwepo tangu awali. Ukatokea mvutano mkubwa baina ya pande tatu ambazo ni LFP, Amazon na Canal+.

Lakini sasa nyota hao hawapo, Messi akienda Marekani na Neymar akitimkia Saudi Arabia. Hii imefanya Ligue 1 kupungua mvuto na Amazon kuona haina maana tena huku Canal+ wakisusa tangu wakati ule wa mgogoro.

Kuondoka kwa Messi na Neymar kumeleta hasara kubwa kwenye Ligue 1 kwa mapato ya kimataifa. Soko kubwa la biashara ya haki ya matangazo ya mpira ni nje ya nchi husika.

Kadri ligi inavyokuwa na mvuto nje ya nchi yake ndiyo biashara kubwa inafanyika na mapato makubwa kupatikana. Messi na Neymar walikuwa na mvuto mkubwa kimataifa, kuondoka kwao kumeipoozesha na kusababisha watu wengi kutoka nje ya Ufaransa kutotamani kuendelea kuiangalia Ligue 1.

RONALDO

Kitendo cha Ronaldo kwenda Saudi Arabia na kuvuta nyota wengine wengi akiwemo Neymar kumeongeza thamani ya ligi hiyo na kufanya vituo kadhaa duniani kukimbilia huko kutaka kuonyesha.

DAZN ambao wameipotezea ligi ya Ufaransa walisaini tangu Agosti, mwaka huu mkataba wa kuonyesha Ligi Kuu Saudi Arabia katika nchi 170 duniani.

Canal+ halikadhalika wameitosa ligi ya Ufaransa na kwenda Saudi Arabia ambako wamenunua hali ya kuonyesha ligi hiyo nchini Ufaransa na nchi za Afrika zinazozungumza Kifaransa.

Hii inamaasha kwamba ligi ya Saudi Arabia kwa sasa ina mvuto mkubwa kuliko ligi ya Ufaransa kutokana na nyota iliyosheni.

Jordan Henderson, Karim Benzema, N’Golo Kante, Sadio Mane, Roberto Firmino, Kalidou Koulibaly na wengine wengi ni wachezaji wakubwa waliong’ara kwenye ligi kubwa za Ulaya kwa muda mrefu na kuwavutia wengi

Cristiano Ronaldo ndiye anatajwa kuwa kinara wa mvuto wa ligi ya Saudi Arabia duniani. Vituo 48 vinaonyesha ligi hiyo katika nchi 170 duniani kwa lugha mbalimbali kama Kiingereza, Kifaransa, Kihispaniola, Kiitaliano, Kireno, Kipolandi, Kihindi, Kichina, Kitailandi na Kijapani.

Afrika Mashariki ni moja ya maeneo yanayotazama ligi ya Saudi Arabia kupitia Azam Media. Kwa kifupi ni kwamba Ligue 1 inapaswa kujipanga upya kwa kutengeneza mkakati utakaoisaidia kuongeza mvuto nje ya nchi ili kushindana na ligi kama ya England na Hispania.

Mkataba wa sasa wa haki ya matangazo ya runinga utaisha mwishoni mwa msimu huu. Kwa hiyo bado kuna muda wa zaidi ya miezi sita kurekebisha hilo.

Chanzo: Mwanaspoti