Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Messi, Lewandowski, kuumizana, Tunisia yasubiri maajabu

Messi X Lewandowski Messi, Lewandowski, kuumizana, Tunisia yasubiri maajabu

Wed, 30 Nov 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Usizubae. Ukizubaa tu, unalizwa. Hivyo ndivyo hali ilivyo kwenye Kundi C la fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar.

Msimamo unasomeka hivi baada ya mechi mbili, Poland ya Robert Lewandowski inaongoza ikiwa na pointi nne. Kisha inafuatia Argentina ya Lionel Messi na pointi tatu. Wanafuatia Saudi Arabia na pointi tatu pia na wa nne ni Mexico wenye pointi moja. Zinatakiwa timu mbili tu za kutinga hatua inayofuata ya 16 bora kwenye fainali hizo. Kipute ni leo Jumatano.

Nani atatoboa? Kasheshe lilivyo ni kwamba timu mbili za juu kwenye kundi hilo zitakutana zenyewe kwa zenyewe na timu za chini zitakutana zenyewe kwa zenyewe kwa maana ya Poland kukipiga na Argentina na Saudi Arabia kukipiga na Mexico. Kazi ipo. Sare itakuwa na matumaini makubwa kwa Poland, lakini kwa Argentina, Saudi Arabia na Mexico matumaini yao ya kutinga hatua ya 16 bora yatapatikana kwa ushindi tu kwenye mechi zao.

Ushindi utawaweka pazuri Argentina kwa sababu watakuwa wamefikisha pointi sita zitakazowafanya waongoze kundi, la kama Saudi Arabia itaichapa Mexico kwa idadi kubwa ya mabao.

Argentina yenyewe ina +1 ya tofauti ya mabao, wakati Saudi Arabia ina -1 ya tofauti ya mabao. Hivyo, miamba hiyo miwili itakuwa kwenye vita kali na huenda wakafuzu wote kama watashinda mechi zao za mwisho. Nani atakubali kubaki?

Poland ina +2 ya tofauti ya mabao, wakati Mexico ina -2 ya tofauti ya mabao.

Argentina na Poland zimeshawahi kukutana mara moja kwenye mechi ya kirafiki, mwaka 2011, ambapo taifa hilo la Amerika Kusini lilikubali kichapo cha bao 2-1. Je, safari hii Argentina watapindua meza kwenye mechi ya ushindani au Poland wataendeleza ubabe? Subiri tuone.

Saudi Arabia na Mexico ni mechi nyingine inayotazamiwa kuwa na upinzani mkali kwani kila moja inaamini inaweza kufuzu hatua ya 16 bora kwa kuzingatia matokeo ya mchezo Poland na Argentina. Uzuri wa mechi hizo, zote zinachewa muda mmoja, saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki ili kukwepa upangaji wa matokeo.

Mchakamchaka mwingine wa kukamilisha mechi za hatua ya makundi utaendelea kwenye Kundi D, lenye timu za Ufaransa, Australia, Denmark na Tunisia.

Msimamo wa kundi hilo, Ufaransa wameshapenya kwenye hatua ya 16 bora baada ya kukusanya pointi sita, wakafuatia Australia wenye pointi tatu kisha Denmark na Tunisia kila moja ina pointi moja.

Utamu wa kundi hilo ni mechi baina ya Denmark na Australia. Patachimbika. Denmark inaamini kusonga mbele ni lazima waichape Australia katika mchezo huo, huku wapinzani wao wakiamini sare inaweza kuwavusha kama Tunisia watachapwa na Ufaransa kwenye mchezo mwingine.

Matumaini ya Tunisia watakaokipiga na Ufaransa ni hafifu, kwa sababu watahitaji kushinda kwa mabao mengi dhidi ya Ufaransa na si vinginevyo. Kwa sasa Australia nafasi yao ni kubwa, lakini watahitaji kukwepa kipigo kutoka kwa Denmark yenye mastaa wa maana akiwamo kiungo fundi wa pili, Christian Eriksen. Nani atatoboa na kuungana na Ufaransa kwenye hatua ya 16 bora kutoka kwenye kundi hilo. Mechi za kundi hilo zitapigwa saa 12:00 jioni leo.

Denmark na Australia zimewahi kukutana mara nne huko nyuma, mara moja kwenye Kombe la Dunia 2018, mchezo wa Kundi C, ambapo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mechi tatu nyingine walizokutana zilikuwa za kirafiki, ambapo Denmark imeshinda mara mbili na Australia kushinda moja. Nani atakuwa kidume safari hii kwenye mechi muhimu kwelikweli?

Tunisia na Ufaransa rekodi yao zimewahi kukutana mara tatu kwenye mechi za kirafiki, Les Bleus ikishinda moja na mechi nyingine mbili zilizomalizika kwa sare. Mchezo wa leo, Ufaransa haitakuwa na presha yoyote, hivyo kazi ni kwa Tunisia.

Chanzo: Mwanaspoti