Timu ya Inter Miami inayomilikiwa na David Beckham imethibitisha mpango wake wa kuwanasa magwiji wawili wa Barcelona, Lionel Messi na Sergio Busquets katika dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Klabu hiyo ya Ligi Kuu Marekani imekuwa ikihusishwa na mpango wa kumnasa Messi, 35 na Busquets, 34, msimu huu na kuelezwa kwamba mpango wote unaweza kukamilishwa mwishoni mwa msimu huu.
Hata hivyo, kwenye usajili wa wakati hao Inter Miami itakabiliwa na upinzani mkali kutokana na timu nyingi kuhitaji huduma zake. Barca imeripotiwa kuwa na mpango wa kumwongeza mkataba Busquets na hilo pia linaweza kutokea kwa Messi, ambaye kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain. Barca pia wanahitaji saini ya Messi.
Kocha wa Inter Miami, Phil Neville amefichua mpango wa klabu yake kufukuzia saini ya wakali hao wa soka duniani, akisema: "Siwezi kukataa kwamba si kweli kinachozungumzwa, kwamba tunawahitaji Lionel Messi na Sergio Busquets.
"Tangu nilipojiunga na Miami, nadhani tumekuwa tukihusishwa karibu na kila mchezaji mkubwa kwenye soka. Kuanzia Sergio Ramos, Dani Alves, Robert Lewandowski, Willian, Cesc Fàbregas, Luis Suárez . . .wote hao.
Kawaida yetu kuhusishwa na wachezaji wa kiwango cha dunia. Kwa sasa tunao Gonzalo Higuaín na Blaise Matuidi.”