Mchezaji wa zamani wa Manchester City, Benjamin Mendy (28) amesaini mkataba wa miaka miwili ya kuitumikia klabu ya Lorient inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ufaransa (Ligue 1).
Mendy amesaini mkataba huo unaomrejesha katika soka la ushindani hadi 2025, siku chache baada ya Mahakama ya Chester Crown iliyopo nchini Uingereza kumkuta hana hatia katika kesi mbili zilizokuwa zinamkabili.
Lorient imethibitisha kunasa saini ya beki huyo wa kushoto leo Julai 19,2023 katika kurasa zake za mitandao ya kijamii kuwa imekamilisha dili la Mfaransa huyo kama mchezaji huru.
Usajili wa Mendy ambaye ni beki wa kushoto, umepokelewa kwa hisia tofauti na mashabiki wa soka duniani huku watu wengi wakionyeshwa kufurahishwa na taarifa hiyo.
Stephendonkah amemtia moyo huku akisema; "Ninakupongeza Mendy. Ni wakati wa kuuthibitisha ulimwengu wa soka kuwa haikuwa sawa, jitokeze tena kwa ustadi wa hali ya juu, watakuja kukutafuta hasa timu bora zaidi barani Ulaya..."
Lorient ilimaliza msimu wa 2022/23 ikiwa nafasi ya 10 katika msimamo la ligi hiyo huku Mendy akitarajiwa kuleta mabadiliko katika kikosi hicho.