Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Dodoma Jiji FC Melis Medo ameushukuru Uongozi na Mashabiki wa Klabu hiyo, baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba wake, usiku wa kuamkia leo.
Uongozi wa Klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, ulithibitisha kuachana na Kocha huyo kutoka nchini Marekani mwenye asili ya Misri, kwa kutoa taarifa maalum iliyosambazwa katika vyanzo mbalimbali vya habari.
Kocha huyo ametoa neno la shukurani kwa Uongozi na Mashabiki, huku akiitakia kila la kheri timu ya Dodoma Jiji FC katika kupambania alama tatu za kila mchezo wa Ligi Kuu msimu huu 2023/24.
Medo amewasilisha salamu hizo za shukurani kupitia taarifa maalum ambayo ameichapisha katika kurasa zake za mkitandao ya Kijamii, inayoseomeka: “Ningependa kuwashukuru usimamizi wote wa timu ya Dodoma jiji pamoja na mashabiki wa Dodoma jiji kwa msaada wenu kwa kunisaidia kuifikisha timu ya Dodoma jiji katika nafasi ya 4 nawashukuru sana kwa hilo.
Hivyo Ningependa kuwaomba radhi mashabiki wa timu ya Dodoma jiji kwa kutokuwepo katika michezo 3 iliyopita kutokana na mimi kusafiri kwenda Dubai kwa ajili ya kwenda kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayoikumba familia yangu.
Hivyo ningependa kuiambia timu yangu nikimaanisha usimamizi wa timu ya Dodoma Jiji nimeona ni vyema ikaajiri mwalimu mwingine/kocha mwingine kwa sababu bado sijui itanichukua muda gani kutatua matatizo yanayo ikumba familia yangu.
Nawatakia kila la heri timu yangu ya Dodoma Jiji, naipenda Dodoma jiji nawapenda mashabiki wa Dodoma jiji. Natumaini timu yangu itapata kocha mzuri na timu itarudi tena katika nafasi nzuri kama nilivyoiacha. Kwa upendo wangu wote naipenda Dodoma Jiji naitakia kila la heri.”