Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mechi zilizomponza Paqueta hizi hapa

Lucas Paqueta Matatani Mechi zilizomponza Paqueta hizi hapa

Sun, 26 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kiungo wa West Ham United, Lucas Paqueta yupo kwenye hatari ya kukumbana na adhabu kubwa zaidi kwenye soka baada ya kufanyiwa uchunguzi kufuatia madai ya kubeti juu ya kadi nne za njano alizoonyeshwa hivi karibuni.

Paqueta, 26, amefunguliwa mashtaka hayo na FA wiki iliyomalizika kwa kukiuka sheria za kubeti.

FA inamshutumu kiungo huyo wa Kibrazili kuonyeshwa kadi za njano za makusudi kwa dhamira ya kubeti ili kumnufaisha mtu mmoja au kundi la watu kinyume na utaratibu.

Na kilichoelezwa kwenye madai hayo ni kwamba Paqueta alitafuta kadi za njano za makusudi kwenye mechi dhidi ya Leicester City, Novemba 2022, Aston Villa, Machi 2023, Leeds United, Mei 2023 na Bournemouth, mechi ya kwanza iliyocheza timu yake kwenye Ligi Kuu England msimu wa 2023-24.

1.Tukio la kwanza: West Ham 0-2 Leicester, dakika 60

Kwenye tukio la kwanza, Mbrazili huyo alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu ya nyuma, staa wa Leicester, Boubakary Soumare. Awali mwamuzi Jarred Gillett aliacha mchezo kuendelea kwa sababu Leicester ilikuwa ikishambulia, lakini baadaye alirudi kumwonyesha kadi ya njano Paqueta.

2.Tukio la pili: West Ham 1-1 Aston Villa, dakika 70

Mara ya pili ilitokea miezi minne baada ya tukio la mwanzo, kwenye mechi dhidi ya Aston Villa iliyofanyika kwenye Uwanja wa London. Paqueta aliteleza kumchezea rafu John McGinn katikati ya uwanja na baada ya kuukosa mpira, alicheza miguu ya mchezaji wa timu pinzani na hivyo, akaonyeshwa kadi ya njano.

3.Tukio la tatu: West Ham 3-1 Leeds, dakika 65

Tukio la tatu lilitokea mwishoni mwa msimu wa 2022-23 kwenye mechi dhidi ya Leeds, kwenye uwanja wa nyumbani wa West Ham huko London. Wakati Leeds ikifanya shambulizi la kushtukiza, Paqueta alikwenda kumchezea rafu Crysencio Summerville kwa nyuma. Mwamuzi Peter Bankes alimwonyesha kadi ya njano Paqueta kwa tukio hilo.

4.Tukio la nne: Bournemouth 1-1 West Ham, dakika 93

Zikiwa zimebaki dakika chache mechi ya kwanza ya msimu kumalizika, Paqueta aliruka juu kujaribu kuzuia shambulizi, lakini badala yake alishika mpira. Mwamuzi alikuwa amesimama mbele yake na kuona tukio zima, hivyo alimwonyesha kadi ya njano Mbrazili huyo.

Hata hivyo, Paqueta amekanusha madai hayo, akisema anashangaa kwa uamuzi huo wa FA kumfungulia mashtaka. Paqueta hakubeti mwenyewe, lakini kinachoelezwa akaunti iliyobeti imesajiliwa kama Paqueta Island iliyopo huko Rio de Janeiro, Brazili, mahali ambako staa huyo wa West Ham United alizaliwa.

Chanzo: Mwanaspoti