Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mechi ya ubingwa EPL inapigwa Anfield

Skysports Klopp Guardiola Pep 4436355 Mechi ya ubingwa EPL inapigwa Anfield

Sun, 10 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Liverpool inaikaribisha Manchester City leo katika Uwanja wa Anfield, mchezo ambao una nafasi kubwa ya kutoa muelekeo wa vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya England (EPL), msimu huu.

Ushindi wa leo, utakuwa ni hatua kubwa kwa Liverpool kwani utaifanya iongoze kwa tofauti ya pointi nne mbele ya Manchester City na pointi mbili dhidi ya Arsenal na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Kwa upande wa Manchester City, yenyewe ikiwa na pointi 62, ushindi utaifanya iipiku Liverpool kwa pointi mbili na hivyo kujiweka katika mazingira mazuri ya kusaka taji hilo la EPL.

Mechi hiyo ya leo inakumbushia mchezo uliopita wa timu hizo kwenye EPL ambapo timu hizo mbili zilitoka sare ya kufungana bao 1-1, Manchester City ikipata bao lake kupitia kwa Erling Haaland wakati lile la Liverpool likipachikwa na Trent Alexander-Arnold.

Shilingi imesimama

Takwimu mbalimbali za mechi ambazo timu hizo zilicheza iwe kwa kukutana zenyewe au kuumana na nyingine, zinatoa ishara ya ugumu wa pambano hilo la leo.

Uwanja wa Anfield umeonekana kutokuwa sehemu salama kwa Man City kila inapoenda kukumbana na Liverpool katika mechi za ligi na kuthibitisha hilo, katika mechi 20 zilizopita baina yao kwenye Uwanja huo, imepata ushindi mara moja tu, ikitoka sare sita na kupoteza mechi 13.

Lakini ukiondoa ubabe huo wa Liverpool dhidi yao, kingine ambacho kinaweza kuipa hofu Manchester City kwenye mechi hiyo ni rekodi nzuri ambayo Liverpool wamekuwa nayo katika Uwanja wake wa nyumbani ambao umeonekana kuwa mwiba kwa timu nyingine pia tofauti na Man City.

Tangu ilipofungwa bao 1-0 na Leeds United, Oktoba 19, 2022 hadi sasa, Liverpool imecheza idadi ya michezo 25 ya Ligi Kuu England katika Uwanja wa nyumbani bila kupoteza ikipata ushindi katika mechi 20 na kutoka sare mara tano.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Liverpool, Man City nayo inaonekana haina unyonge ugenini kwani imetoka kupata ushindi katika mechi tano mfululizo za ugenini za ligi.

Lakini pia Man City imekuwa na moto wa kuotea mbali katika siku za hivi karibuni kwani inakutana na Liverpool ikiwa imetoka kucheza mechi 20 mfululizo za EPL bila kupoteza ikipata ushindi mara 18 na kutoka sare mbili.

Refa hana mzaha

Mwamuzi wa kati, Michael Oliver (39) ndiye amepangwa kuchezesha mechi hiyo akiwa na historia ya kutoendekeza wachezaji wanaopenda rafu na kujihusisha na makosa ya utovu wa nidhamu.

Msimu huu, refa huyo amechezesha idadi ya mechi 18 za Ligi Kuu ya England, akitoa idadi ya kadi 78 ambapo kati ya hizo, kadi za njano ni 76 na kadi nyekundu mbili huku akitoa adhabu ya pigo la penalti mara nne.

Mchezo wa mwisho baina ya timu hizo ambao refa Oliver alishika filimbi, ulimalizika kwa Manchester City kuibuka na ushindi wa 1-4 ugenini.

Wasaidizi wa Oliver katika mechi ya leo ni Stuart Burt, Dan Cook na refa wa mezani akipangwa kuwa David Coote na kwenye teknolojia ya usaidizi wa video kwa marefa (VAR) atakuwa Stuart Attwell na Nick Hopton.

Majeruhi presha Liverpool

Timu hizo zinaingia huku Manchester City ikiwa na faida ya kuwa na majeruhi wachache kikosini kulinganisha na idadi ambayo ipo kwa Liverpool.

Manchester City itamkosa Jack Grealish huku ikiwa katika hatihati ya kuwakosa Jeremie Doku na Matheus Nunes.

Wenyeji Liverpool itaendelea kuwakosa Trent Alexander-Arnold, Alisson Becker, Diogo Jota, Thiago Alcantara na Curtis Jone.

Kwingine hakujapoa

Ukiondoa mechi hiyo, kwenye Uwanja wa Villa Park, Aston Villa itaikaribisha Tottenham Hotspur, Brighton itakabiliana na Nottingham Forest wakati West Ham itaikaribisha Burnley.

Chanzo: Mwanaspoti