Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mechi ya pointi tatu muhimu

Simba Vs Singida.jpeg Mechi ya pointi tatu muhimu

Tue, 12 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Simba itajiweka katika mazingira mazuri ya kuiondoa Azam FC kwenye nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi ikiwa itaibuka na ushindi dhidi ya Singida Fountain Gate leo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 1:30 usiku.

Simba imerejea Chamazi baada ya uwanja wa nyumbani iliyokuwa imeuchagua, Jamhuri Mororogo kufungiwa na Bodi ya Ligi.

Matokeo ya ushindi katika mechi ya leo, yataifanya Simba iwe nyuma ya Azam FC iliyo katika nafasi ya pili kwa pointi tatu, kwani itafikisha pointi 41 huku ikibaki na mechi mbili mkononi tofauti na Azam FC ambayo yenyewe ina pointi 44 hivi sasa.

Kwa Singida Fountain Gate, ushindi kwenye mechi ya leo ni muhimu kwake kwani utaifanya iweze kusogea hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ambapo itafikisha pointi 27 lakini kama itapoteza inaweza kujikuta ikishuka kwa nafasi moja au mbili kutoka ile ya 11 iliyopo sasa kwenda ya 12 au ya 13.

Simba inaingia katika mechi ya leo ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ubabe dhidi ya Singida Fountain Gate ambapo katika mechi tatu zilizowahi kukutanisha timu hizo kwenye Ligi Kuu, Simba imeibuka na ushindi mara mbili na kutoka sare moja, ikifunga mabao sita na yenyewe imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.

Muenendo wa kila timu katika mechi za hivi karibuni za Ligi Kuu, unatoa ishara kuwa Simba ina nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi dhidi ya Singida Fountain Gate leo ingawa bado inapaswa kuwa na tahadhari kubwa katika mechi hiyo.

Katika mechi tano zilizopita za Ligi Kuu, Simba imeibuka na ushindi mara tatu, kutoka sare moja na kupoteza moja huku ikifunga mabao sita na nyavu zake zimeguswa mara nne.

Kwa upande wa Singida Fountain Gate, katika mechi tano zilizopita, haijashinda hata moja, imetoka sare moja na kufungwa mechi nne, ikipata mabao mawili na yenyewe imeruhusu mabao manane.

Singida Fountain Gate itaingia katika mechi ya leo ikiwa na kaimu kocha mkuu, Ngawina Ngawina ambaye amesema kuwa wanaweza kuishangaza Simba kwa kupata ushindi dhidi yao.

“Tunafahamu kwamba katika mechi nne zilizopita hatujapata alama tatu na tumepata pointi moja. Simba ni moja ya timu nzuri ila tuko tayari kuikabili.

“Tumeona udhaifu wao na pia tunajua ubora wao. Tumekaa kwenye kiwanja cha mazoezi kurekebisha udhaifu wetu na tunamaini tunaweza kupata ushindi,” alisema Ngawina.

Kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola alisema kuwa mchezo wa leo dhidi ya Singida Fountain Gate ni mgumu lakini wana imani ya kufanya vyema.

“Siku zote hakuna mechi rahisi kati ya Simba na Singida. Ni timu ambayo huwa inatupa shida sana tunapokutana nayo. Tunajua ubora wa Singida na ugumu waliokuwa nao. Lakini tumejipanga pamoja na ubora na ugumu wao kuhakikisha tunafanya vizuri,” alisema Matola.

Bado kocha mkuu wa Simba Abdelhak Benchikha atakosekana kwenye mchezo huu kwa kuwa alikwenda nchini kwao Algeria kwa ajili ya kozi fupi.

Chanzo: Mwanaspoti