Yanga tayari ina uhakika wa kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuifyatua CR Belouizdad ya Algeria wikiendi iliyopita kwa mabao 4-0 na leo itatafuta heshima nyingine ya kutaka kuongoza Kundi B, wakati itakapoikabili Al Ahly ya Misri katika mechi ya mwisho ya kundi.
Yanga itakuwa wageni wa Ahly kwenye Uwanja wa Cairo International ambao ni watetezi wa taji la michuano hiyo katika pambano litakalopigwa kuanzia saa 1:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki, kila timu ikitaka kumaliza kama kinara ili kukwepa ule mtego wa mechi za robo fainali katika droo itakayopangwa wiki ijayo, jijini Cairo.
Al Ahly kwa sasa ndio vinara wa kundi ikiwa na pointi tisa, huku Yanga iliyopo nafasi ya pili alama nane na matokeo ya ushindi kwa timu mojawapo itaipa nafasi ya kuongoza kundi na kusubiri timu zitakazoshika nafasi ya pili katika makundi ya A, B na C na itakayomaliza ya pili itakuwa na kibarua dhidi ya vinara wa makundi hayo matatu katika robo, lakini mchezo ukimalizika kwa sare itakuwa faida kwa Ahly.
Yanga imetua jijini humo ikitambia rekodi nzuri kwenye kundi, kwani ndio timu inayoongoza kwa mabao mengi hadi sasa, lakini ikiwa ni pekee iliyoifunga bao Al Ahly katika sare ya 1-1 ya mechi iliyopigwa jijini Dar es Salaam.
Akili ya Yanga ni kuhakikisha inapata ushindi mbele ya Al Ahly, lakini wenyeji nao wakitaka kulinda heshima ya nyumbani kwa kutambua kama itaruhusu kupoteza leo itatibua rekodi tamu iliyonayo kwa timu za Tanzania kwenye ardhi ya nyumbani iliyodumu tangu mwaka 1982.
Al Ahly haijawahi kupoteza mechi yoyote nyumbani mbele ya klabu za Tanzania, hivyo inajua ikizembea kidogo kwa kikosi cha Miguel Gamondi mambo yanaweza kuwaendea kombo na kung'olewa kileleni kuwapisha wapinzani wao kuongoza kundi hilo lenye Medeama ya Ghana pia.
Soka la kisasa Licha ya kwamba haitakuwa kazi rahisi kwa Yanga kupata ushindi kama haitapambana kwelikweli, lakini kwa soka ambalo lililoonyesha wawakilishi hao wa Tanzania wanaowategemea nyota wenye kasi na waliotengeneza kombinesheni tamu ya kuzalisha mabao mengi msimu ya Stephane Aziz KI, Mudathir Yahya, Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua ambaye anashika nafasi ya pili kwa kufunga mabao, mbali na washambuliaji wasiotabirika kama Kennedy Musonda, Clement Mzize na Joseph Guede ambaye alifunga bao lililoipeleka timu hiyo robo fainali.
Juu ya ugumu wa mchezo huo, Kocha wa Al Ahly, Marcel Koller amekiri haitakuwa mechi rahisi kwa jinsi walivyoiangalia Yanga kwenye mechi iliyopita, huku Gamondi akiwataka wachezaji kukomaa ili kupata matokeo mazuri na kuongoza kundi ili kupata faida ya kuanzia ugenini na kumalizia nyumbani tofauti na kumaliza ya pili kundini.
Mashabiki wa Yanga wana imani kubwa na timu hiyo wakirejea rekodi iliyoweka msimu uliopita kwa kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria katika fainali za Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo wanaamini kama kina Pacome watakomaa wanaweza kuandika historia ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kuifunga Al Ahly nyumbani.
Rekodi sasa: Katika mechi saba zilizopita za Ligi ya Mabingwa kwa timu hizo kukutana, Al Ahl imeshinda mechi zote tatu za nyumbani iliifunga Yanga mwaka 2016 kwa mabao 2-1, ilishinda pia 2-0 mwaka 2014 na 2009, iliitandika Yanga mabao 3-0, huku mechi nne za ugenini ilishinda moja tu mwaka 2009, mbili ikitoka sare 2016 na msimu huu wakati mwaka 2014 ilipasuka bao 1-0 kwa bao la Nadir Haroub 'Cannavaro'.
Hivyo, mechi hiyo ni kipimo kizuri kwa Gamondi kudhihirisha ubabe wake kwa timu za Waarabu, kama ataibuka na ushindi mbele ya watetezi hao wa taji ambao kwenye mechi yao ya Ligi Kuu iliyopigwa Jumanne iliyopita ilishinda 5-1 dhidi ya Baladiyat El Mahalla, siku chache tangu Yanga ifyatue Belouizdad kwa mabao 4-0 katika mechi ya Kundi D.