Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mechi ya Azam, Yanga hatihati kufanyika

Fei Toto Mzez Mechi ya Azam, Yanga hatihati kufanyika

Tue, 5 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ratiba ya Bodi ya Ligi iliyotoka Jumatatu, Januari 29, ilionyesha kwamba mechi namba 168 ya Dabi ya Dar es Salaam kati ya Azam FC na Yanga itafanyika Machi 17 saa moja usiku uwanjani Azam Complex Chamazi.

Na hadi sasa ratiba rasmi inabaki kuwa hivyo kwa sababu hakuna mabadiliko yaliyotangazwa na mamlaka husika.

Lakini hata hivyo, kuna hatihati kubwa mechi hiyo kuwepo kutokana na mwingiliano wa ratiba.

Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), limeanzisha mashindano yanayoitwa Fifa Series ambayo yataanza Machi 22, mwaka huu katika vituo vitano tofauti.

Kama jina lake lilivyo, SERIES, mashindano haya yatafanyika kwa series yaani mfululizo kutoka kituo hadi kituo.

Tanzania imealikwa na kuthibitisha kushiriki mashindano hayo yatakayoshirikisha timu 20 kutoka mabara yote wanachama wa Fifa.

KUTOKA CAF (Afrika)

Tanzania

Algeria

Afrika Kusini

Cape Verde

Guinea

Guinea ya Ikweta

Jamhuri ya Afrika ya Kati

KUTOKA UEFA (Ulaya)

Azerbaijan (kama wenyeji)

Bulgaria

Andorra

Kutoka CONCACAF (Amerika Kaskazini)

Guyana

Bermuda

KUTOKA CONMEBOL (Amerika Kusini)

Bolivia

KUTOKA AFC (Asia)

Mongolia

Cambodia

Brunei Darussalaam

Sri Lanka

Bhutan

KUTOKA OFC (Oceania)

Vanuatu

Papua New Guinea

Vituo vya mashindano haya ni Algeria, Azerbaijan, Saudi Arabia A na Saudi Arabia B, na Sri Lanka.

Ratiba ya mashindano haya ambayo kimsingi ni mechi za kirafiki za kimataifa zilizoandaliwa na kuratibiwa na FIFA, inaonyesha yataanza Machi 22.

Kwa utamaduni wa Tanzania ambayo timu yake imepangwa kuwa kituo cha Azerbaijan, lazima kuwe na kambi angalau ya siku moja ya kujiandaa na kusafiri.

Kutoka Tanzania hadi Azerbaijan ni safari ya takribani siku mbili.

Hata kama kambi haitakuwepo, haiwezekani kusafiri Machi 18 baada ya mechi kwa ajili ya kuwahi tarehe 22 kule.

Hapa ndipo panapotia shaka ya uwepo wa mechi hiyo ambayo inaweza kuamua hatima ya ubingwa. Ndiyo maana ni muhimu Bodi ya Ligi kusema chochote mapema ili timu husika ziweze kupanga mambo yao.

Bahati mbaya sana kwa mamlaka za soka Tanzania hujisahau kutoa ufafanuzi mikanganyiko kama hii na kuja kuibuka ghafla na maelekezo mapya.

Vikao vya kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi vinafanyika kila mara, lakini hawagusii hili. Matokeo yake litakuja kama zimamoto. Kwa namna ligi inavyokwenda, hii mechi ni muhimu sana kwa hatima ya ubingwa wa ligi msimu huu.

Yanga wanaongoza ligi hadi sasa kwa alama 43 sawa na Azam FC, lakini wakiwa na faida ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Hata hivyo, Azam FC wamecheza mechi tatu zaidi ya Yanga (19 kwa 16), hivyo Azam FC wanaweza kutaka kuutumia mchezo huo kuwapunguza kasi Yanga, huku Yanga wakitaka kujiimarisha.

Hapo ndipo utamu na umuhimu wa mchezo huu unapokuja. Kwa hiyo Bodi ya Ligi inapaswa kuweka mazingira sawa kuelekea mchezo huu ikiwemo kuondoa shaka shaka za kuwepo au kutokuwepo ili kuwe na umakini wa maandalizi.

Mchezo wa Yanga na Azam FC ndiyo unaofuata kwa umaarufu hapa nchini baada ya watani wa jadi, Yanga na Simba. Lakini ukiacha umaarufu, mchezo huu unaweza kuwa unaongoza kwa soka la uhakika kuchezwa uwanjani na kutoa burudani.

Ukiangalia matokeo ya mechi nne zilizopita za Ligi Kuu baina yao utaona ni namna gani mechi zilikuwa za kuburudisha kutokana na mabao mengi kufungwa japo mwisho wa siku Azam FC walipoteza zaidi.

NNE ZILIZOPITA

Azam FC 1-2 Yanga

Yanga 2-2 Azam FC

Azam FC 2-3 Yanga

Yanga 3-2 Azam FC

Mechi za namna hiyo zinaonyesha ni namna gani mashabiki waliishi maisha ya roho juu muda wote wa mchezo, huku wengine wakishindwa kukaa kwenye viti. Hiki ndicho kinachoongeza msisimko kwenye mechi ya timu hizo mbili.

Watu wameshaanza kuwekeza kwenye mchezo huo kwa kufanya matangazo kuelekea siku ya mchezo. Kwa hiyo ni jambo jema kwa Bodi ya Ligi kutoka na kuthibitisha kwamba mchezo utakuwepo ili watu waishi pasi na shaka ya kuukosa.

Alipotafutwa kuhusiana na hilo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Bodi ya Ligi (TPLB), Karim Boimanda alisema hadi sasa hakuna mabadiko yoyote yaliyofanyika au kujadiliwa hivyo ratiba itabaki kama ilivyo hadi watakapotoa maelezo mengine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live