Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mechi walizokimbiana Simba, Yanga

Upupu Pic Data Mechi walizokimbiana Simba, Yanga

Tue, 11 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga uliokuwa ufanyike Mei 8, 2021 kwenye Uwanja wa Mkapa ulishindikana kutokana na matatizo ya mawasiliano kati ya mamlaka za kiserikali, za soka na wahusika wakuu yaani klabu zenyewe.

Hata sitaki kuingia sana huko maana kuna SI HASA nyingi kuliko SIASA. Leo nataka nikuletee mechi za watani ambazo zilitakiwa kufanyika, lakini zikashindikana kutokana na mtani mmoja kutotokea uwanjani.

Mechi hizi ni tofauti na zile zilizovunjika. Hizi ni zile ambazo hazikufanyika kabisa. Lakini kabla zikaanza kuzijadili mechi hizo, kwanza ningependa kukemea hii tabia inayozidi kukomaa ya kuishusha thamani mechi kwa kuiita jina la DABI.

Utandawazi ulioanza kuikumba Tanzania zaidi katika miaka ya 2000 umewafanya waandishi wa habari wa Tanzania kulijua neno dabi na kulileta nchini kama lilivyo na kulipandikiza kwenye mechi ya timu hizi mbili kongwe.

Hii ni dharau kubwa kwa mechi hii ya kihistoria. Hii mechi ni zaidi ya dabi, ni watani wa jadi. Dabi ni mechi baina ya timu mbili kutoka eneo moja la kijiografia; mtaa mmoja, kitongoji kimoja, kijiji kimoja, mji mmoja au hata ukanda mmoja.

Siyo lazima timu hizo ziwe na historia yoyote ya upinzani, mradi tu zinatoka eneo moja. Kwa mfano, Ashanti na African Lyon ni Dabi, Azam FC na Pan African au Cosmopolitan ni dabi.

Yanga au Simba wakicheza na yeyote katika hao hapo juu, ni dabi. Kwa hiyo dabi siyo kitu kikubwa saaana. Ni kakitu kadogo tu. Ni kutoka eneo moja tu, basi.

Kutumia neno dabi kwenye mchezo wa Simba na Yanga ni kuufanya uonekane wa kawaida tu, yaani wa timu za eneo moja tu, basi. Lakini Yanga na Simba ni zaidi hapo. Ni zaidi ya eneo moja. Ni historia, visasi, itikadi na harakati za maisha. Ni ya WATANI WA JADI.

Jadi maana yake ni seti ya mila, mazoea, maadili na maarifa ambayo hurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi na ambayo ni sehemu ya utamaduni wa jamii husika.

Natoa wito kwa waandishi kulitumia zaidi jina la WATANI WA JADI kuliko DABI kwa sababu linaleta hadhi tofauti.

WATANI KUKIMBIANA

Katika historia ya ligi ya Tanzania tangu kuanzishwa kwake 1965, huu ni mchezo wa tani kushindwa kufanyika kutokana timu moja kutofika uwanjani kwa sababu moja au nyingine.

Lakini kwa ujumla ni mchezo wa sita, ukichanganya na mashindano mengine.

1.SIMBA KUIKIMBIA YANGA 1969

Ilikuwa Machi 3, 1969, wakati huo ikiitwa Sunderland (Simba) ilikataa kucheza na Yanga kwa sababu walikataliwa rufaa yao dhidi ya African Sports ya Tanga.

African Sports na Sunderland walitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa ligi, lakini Sunderlabd walilalamika kwamba Sports walimchezesha kipa ambaye hakusajiliwa.

Hata hivyo, Sports wakasema waliruhusiwa na FAT (Chama cha Soka Tanzania wakati huo) kwa barua kufuatia maombi yao kwa sababu walikuwa na makipa wawili tu; mmoja alikuwa anaumwa macho na mwingine alikuwa safarini. Kwa hiyo mechi ilipofika wakawa hawana kipa. Wakaomba kwa FAT wamtumie kipa mwingine, FAT ikakubali.

Lakini baada ya mechi kwisha kwa sare, Sunderland wakakata rufaa ikakataliwa, ndipo nao wakagomea mechi na Yanga. Yanga wakapewa alama za mezani na Sunderland kupigwa faini ya Sh500 ambayo hata hivyo walirudishiwa.

2.YANGA KUIKIMBIA SIMBA 1992

Ilikuwa Septemba 26, 1992 kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza Bara. Yanga walikataa kuingia uwanjani kucheza na Simba kwa sababu tayari walikuwa wameshachukua ubingwa.

Wakasema hiyo mechi haikuwa na maana kwao kwa sababu ubingwa tayari wanao. Simba wakapewa alama za mezani na Yanga kupigwa faini ya Sh250,000 ambazo zililipwa na mfadhili wao mpya, Murtaza Dewji aliyejiunga nao akitokea Pan Africa.

3.SIMBA KUIKIMBIA YANGA 1996

Ilikuwa Februari 26 ambapo Simba waligoma kucheza na Yanga kwa sababu walikuwa wanataka kujiandaa na mechi ya kimataifa ya Kombe la Washindi Afrika dhidi ya Chapungu Rangers ya Zambia.

Simba waliandika barua FAT kuomba ibadilishe tarehe ya mechi hiyo, lakini FAT ikakataa. Simba wakagoma kucheza na Yanga wakapewa alama za mezani. Hata hivyo, Chapungu wenyewe hawakuja kucheza hiyo mechi, Simba wakapewa ushindi wa mezani na kuvuka hadi hatua iliyofuata.

4. YANGA KUIKIMBIA SIMBA 2002

Yanga ilimsajili Said Maulid kutoka Simba mwaka 2002. Julai mwaka huo, Wizara ya Mambo ya Ndani ikatangaza kwamba mchezaji huyo siyo raia wa Tanzania. Tangazo hilo lilitoka wakati pambano la Yanga na Simba likikaribia.

Yanga wakagomea huo mchezo hadi Said Maulid aruhusiwe kucheza. Serikali ikasema mchezaji huyo ni Mkongomani na akitaka kuendelea kucheza Tanzania, basi awe na hati ya kusafiria ya Kongo.

Said Maulid akafungua kesi mahakamani na akashinda, akarudishiwa uraia wake. FAT iliahirisha hiyo mechi hadi mchezaji huyo aliporejeshewa uraia wake mahakamani.

5.YANGA KUIKIMBIASIMBA KAGAME2008

Yanga na Simba zilitakiwa kukutana kuwania mshindi wa tatu wa Kombe la Kagame baada ya zote kutolewa nusu fainali. Lakini Yanga hawakuingia uwanjani bila sababu zilizoeleweka.

Baadaye mwenyekiti wao, Imani Madega akasema walikubaliana na Simba, TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na Cecafa (Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati) kwamba wapewe Sh50 milioni kabla ya mchezo huo, lakini hadi siku ya mchezo pesa hizo hawakupewa ndipo wakagoma.

Akaongeza kwamba walikubaliana na Simba kugoma pamoja, lakini Simba waliwasaliti na kwenda uwanjani. Cecafa wakaifungia Yanga kushiriki mashindano hayo kwa miaka mitatu. Hata hivyo baada ya miaka miwili wakasamehewa.

TFF pia ikaifungia Yanga kushiriki mashindano yoyote ya kimataifa kwa miaka mitatu. Yakatoka mashinikizo kutoka serikalini kwenda TFF huku wabunge wakiwa na mjadala mkali bungeni kuhusu sakata hilo. Ikaundwa kamati ya kiandamizi kuhakikisha kinatafutwa kipengele cha kuichomoa Yanga kwenye adhabu, na kweli ikachomolewa.

Kwa hiyo haya mambo ya mmoja kumkimbia mwenzake yameshatokea mara kadhaa huko nyuma kiasi cha mechi kutofanyika kabisa. Na hapo ni mbali na mechi ambazo tayari zilishaanza, lakini hazikumakizika kwa mmoja kumkimbia mwenzake.

Siku ikitokea mchezo umevunjika, nitakuletea orodha ya mechi hizo.

Kwa maoni tuandikie SMS au WhatsApp kupitia namba 0658 - 376417

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz