Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mechi tano za jasho na damu

Mechi Tano Mechi tano za jasho na damu

Wed, 31 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Azam FC ikiongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya mabingwa watetezi Yanga, vita inaanza upya Februari kwa timu tatu za juu kuwania nani atakuwa kinara baada ya mechi tano ndani ya mwezi huo.

Vita hiyo itazikutanisha timu tatu za juu ambazo zinakimbizana kwa pointi licha ya kuachana kwa idadi ya mechi zilizocheza huku Azam FC ikionekana kuwa juu baada ya kucheza mechi 13 na kufanikiwa kukusanya alama 31.

Katika msimamo huo watani wa jadi, Simba na Yanga wanafuatana, ambapo bingwa mtetezi amekusanya pointi 30 baada ya kucheza michezo 11 huku Simba ikiwa nafasi ya tatu baada ya mechi tisa ilizokusanya pointi 23.

Vigogo hao mapema mwezi ujao watapishana viwanja kusaka pointi 15 zitakazowahakikishia nani ataongoza msimamo wa ligi, huku vita nyingine ya timu zilizo katika nafasi mbaya kwenye msimamo ikiendelea baada ya usajili uliofanyika wakati wa dirisha dogo lililofungwa Januari 15.

AZAM FC

Februari 9, matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC wataanzia ugenini kuikabili Simba kisha Februari 16 watarudi nyumbani kumenyana na Geita Gold na baada ya hapo wataifuata Tabora United, Februari 19.

Baada ya Tabora wataifuata Tanzania Prisons, Februari 25 na kumalizia ratiba ya mwezi wa pili kwa kuikabili Singida Fountain Gate, Februari 28.

YANGA SC

Yanga itakuwa na kibarua dhidi ya Kagera Sugar ugenini ikishuka uwanjani Februari 2, kisa itarudi nyumbani kuwaalika Dodoma Jiji kabla ya Februari 5 kuifuata Mashujaa FC.

Mechi nyingine za Yanga za Februari zitakuwa ugenini zote ikianza kwa kuifuata Tanzania Prisons, Februari 11 na kumaliza na KMC ambayo iliifunga mabao 5-0 katika mzunguko wa kwanza Februari 17.

SIMBA SC

Wekundu wa Msimbazi wana mechi nne Februari - tatu zikiwa za ugenini na moja nyumbani wakianza na Mashujaa FC (Februari 3), Tabora United (Februari 6) zote ugenini na baada ya hapo watarudi nyumbani Februari 9 kuivaa Azam FC na kumalizia ugenini Februari 12 na Geita Gold.

Mechi ya tano watacheza na JKT Tanzania ugenini Februari 15 kwenye Uwanja wa Azam. Kutokana na kuwa na viporo Simba itakuwa na mchezo mwingine mwezi huo dhidi ya Mtibwa Sugar nyumbani Februari 18.

WASIKIE MAKOCHA

Akizungumzia ratiba ya mechi tano za Februari, kocha mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha alisema hazitakuwa rahisi kutokana na timu kutoka sehemu moja kwenda nyingine ambapo inahitaji kuwa na kikosi kilichoshiba ili kuhakikisha inapata pointi zote.

"Tuna ratiba ngumu, lakini pia tuna wachezaji wengi wazuri ambao nina imani wataweza kufanya kile nilichowaelekeza kwenye uwanja wa mazoezi, licha ya changamoto iliyopo mbele yao ya kutoka sehemu moja kwenda nyingine ndani ya siku mbili kabla ya mchezo," alisema.

"Simba ya kesho ni bora zaidi hivi sasa. Naamini ongezeko la wachezaji wapya litaongeza nguvu kikosini na kutoa mwanya kwa kila mchezaji kujipa umuhimu kutokana na ugumu wa ratiba tuliyo nayo."

Kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo alisema wanaendelea vizuri na maandalizi kuelekea mechi hizo.

"Kila mchezaji aliyepo ndani ya kikosi ana ari ya kupambana kutokana na kila mmoja kuwa kwenye nafasi nzuri, hivyo natarajia kuwa na mwendelezo mzuri," alisema.

Kocha Miguel Gamondi wa Yanga, alisema kila mchezo ulio mbele wataucheza kama fainali bila kujali watakutana na timu gani huku akiweka wazi kuwa huu ni mzunguko wa lala salama kila klabu inatakiwa kuvuna pointi.

"Kila mchezo ni muhimu kwetu. Lengo ni kutetea taji, hivyo tunatakiwa kukusanya pointi kwa kuhakikisha tunaandaa vizuri kikosi cha ushindani kwani haitakuwa rahisi ni mzunguko wa mwisho timu zimejiandaa," alisema.

Chanzo: Mwanaspoti