Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mechi hizi Kagere, Luis milioni 85 mezani

99118 Kagere+pic Mechi hizi Kagere, Luis milioni 85 mezani

Mon, 16 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

WACHEZAJI wa Simba kuanzia mtupiaji mwenyewe Meddie Kagere, Luis Jose, John Bocco na wengine wote watakabidhiwa fungu lote la Sh85 milioni za ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, uongozi umethibitisha.

Huo ni mkakati mzigo wa Simba kuhakikisha wanatwaa kombe hilo mapema na kujihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa kuanzia Agosti, mwaka huu.

Simba imepania kurudi kwa nguvu kwenye michuano ya kimataifa ili kurejesha heshima yake baada ya msimu uliopita kutolewa mapema tena kwenye ardhi ya nyumbani.

Habari za ndani ambazo Mwanaspoti limethibitishiwa na kigogo mmoja zinasema kuwa, “kutoa pesa kwa wachezaji wa kikosi chetu kila wakati ambapo wanafanya vizuri ni utamaduni kwani hata hiyo Sh85 milioni halitakuwa jambo la kushangaza kwani kwenye mechi ya ligi tu dhidi ya Yanga ambayo tulipoteza wachezaji wetu walikosa Sh230 milioni huku kwa kila ambaye alicheza alikuwa na uwezo wa kuchukua Sh10 milioni kama tungeshinda.”

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alipoulizwa alikiri kuwepo kwa mkakati huo. “Jambo hilo la kuwapa pesa yote ya ubingwa wachezaji linaweza kuwepo kama tutachukua ubingwa mapema, na hilo linatokana kutumia pesa nyingi katika kuendesha timu kuliko ile ambayo tunapata kama zawadi ya ubingwa, kwani hata sisi tunatafuta pia vyanzo vingi vya kiuchumi ili kuendesha timu katika mazingira sahihi.

“Miongoni mwa sababu ambazo zinasababisha kufanya vizuri kwa timu kwenye mashindano yoyote yale ni kuwepo kwa motisha ya posho kwa wachezaji na jambo hili nimelikuta hapa kabla ya kuanza kazi, hilo limekuwa likifanyika kwa wachezaji wetu.

Pia Soma

Advertisement
“Nguvu na akili yetu kwa sasa ni kuhakikisha kwanza ubingwa wa ligi tunachukua na baada ya hapo ndio masuala mengine yatafuata, lakini wakati huohuo si ubingwa wa ligi tu, bali tuna kombe lingine la Shirikisho (FA), ambalo nalo tuna kiu ya kuona tunapambana na kulichukua.

“Tunafahamu ugumu ambao tunapitia katika timu hasa kwenye masuala ya kiuchumi kama ambavyo nilieleza tunatafuta vyanzo vingi vya kutuingizia mapato miongoni mwa njia ya kufanikiwa hilo ni kuchukua mataji mengi yaliyoko mbele yetu, ndio maana tukishindwa kufanya hivyo katika mashi-ndano yoyote huwa tunaumia mno,” alisema Senzo.

MECHI HIZI

TANO SIMBA..

Simba wamebakiwa na michezo kumi, kati ya hiyo kama wataweza kushinda mitano watatangaza ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo huku wakiwa wamebakiwa na michezo mitano mkononi mwao tofauti na misimu miwili nyuma walipochukua taji hilo.

Hesabu zinaonyesha Simba kwa sasa wapo nafasi ya kwanza wakiwa wamecheza michezo 28, wakivuna pointi 71, kwa maana hiyo wakishinda mechi tano kati ya kumi watakuwa wamevuna pointi 15 ambazo ukijumlisha na walizonazo sasa watafikisha pointi 86, ambazo zitafikiwa na timu moja tu.

Timu ambayo inaweza kufikia pointi 86 ni Yanga ambao kwa sasa wapo nafasi ya tatu wakiwa wamecheza michezo 26, wakiwa na pointi 50, wakibakiwa na mechi 12 ambazo kama itashinda zote itakuwa na pointi 36, ukijumlisha na walizonazo sasa.

Yanga watafikia pointi 86 wakiwa wamemaliza michezo yao yote, lakini Simba wakati huo watakuwa na michezo mitano mkononi ambayo hata kama wakipoteza yote watakuwa pointi sawa na watani zao, ila watatwaa ubingwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kama ambavyo walifanya Yanga msimu wa 2016-17, walipomaliza pointi sawa na watani zao.

Azam ambao wapo nafasi ya pili kwenye msimamo wakiwa wamecheza michezo sawa na Simba wamefikisha pointi 54, wakibakiwa na mechi kumi ambazo kama watashinda zote watafikisha pointi 84, ambazo zitakuwa zimepitwa.

Mechi tano zinazofuata za Simba ni dhidi ya Ruvu Shooting na Mwadui ambazo watacheza Dar es Salaam, wakati dhidi ya Mbeya City, Tanzania Prison na Ndanda watacheza ugenini.

Rekodi zinaonyesha mzunguko wa kwanza Ruvu Shooting walifungwa mabao 3-0, wakati Mwadui walishinda bao 1-0, Mbeya City wao walifungwa 4-0 kama ilivyokuwa kwa Ndanda waliofungwa mabao 2-0 na kuendeleza rekodi ya kutoifunga Simba tangu walipopanda ligi wakati Prisons walitoka suluhu na vinara hao.

Ukiachana na mechi hizo nyingine tano ambazo Simba wamebakiza ili kufikisha michezo kumi ni dhidi ya Namungo, Coastal Union na Polisi Tanzania zote watakuwa ugenini huku dhidi ya Mbao na Alliance watachezea Dar es Salaam.

Kocha wa Simba, Sven Vendernbroeck alisema: “Nadhani tutakaporudi kwenye ligi licha baadhi ya wachezaji wangu wa kikosi cha kwanza kuwa katika timu zao za taifa watakuwa wamepata muda wa kupumzika kuliko wangekuwa kwenye timu wangetumika mara kwa mara, kwa maana hiyo watakuwa wamepata muda wa kutosha kumpumzika.

“Tukirudi tutakuwa na kasi ileile ya kuendelea kupata matokeo mazuri kama tulivyoacha tulipoishia kwa maana ya matokeo ambayo tuliyapata dhidi ya Singida United, kwa maana hiyo naona tutakamilisha zoezi hilo la kutwaa ubingwa mapema iwezekanavyo,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz