Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mechi dhidi ya Raja, Moses Phiri atangaza balaa

Moses Phiri X Simba Moses Phiri

Thu, 30 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba inatarajiwa kutua nchini Morocco muda wowote kucheza mechi ya mwisho ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca lakini mshambuliaji wake, Moses Phiri amepiga hesabu kali na kujipa muda zaidi wa kuendelea kufunga mabao akiwa ndani ya jezi ya wanamsimbazi hao.

Phiri anayeongoza kikosini hapo kwa kupachika mabao 10 kwenye ligi, ameingalia safu ya mbele ya Simba ambalo ndio eneo analocheza na kugundua kunahitajika kitu cha ziada ili Simba izidi kutisha zaidi na yeye kuendelea kufunga kama alivyoanza msimu ndani ya Wanamsimbazi hao.

Straika huyo raia wa Zambia ambaye kasi yake ya kucheka na nyavu ilipungua alipopata majeraha mwezi Disemba mwaka jana na tangu amerejea mwezi Januari mwaka huu hajawa na muendelezo mzuri jambo ambalo amesema ni kutokana na kutopata muda wa kutosha kucheza lakini pia mabadiliko ya timu huku akiamini bado ananafasi ya kufanya vizuri.

Baada ya kuumia kwa Phiri, katika dirisha dogo la usajili Simba ilimsajili straika Mkongomani, Jean Baleke ambaye amekuwa akicheza mara kwa mara na hadi sasa amefunga mabao matano kwenye Ligi Kuu Bara na mawili katika Ligi ya Mabingwa huku mechi nyingine katika eneo la ushambuliaji akipangwa nahodha John Bocco mwenye mabao tisa hadi sasa kwenye ligi.

Lakini pia ongezeko la kiungo mshambuliaji, Mrundi Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’ Simba mwenye mabao 10 na asisti tisa kwenye ligi kulifanya nafasi ya Phiri kucheza kuendelea kuwa finyu tangu ametoka majeruhi kutokana na ubora anaouonyesha staa huyo wa zamani wa Yanga.

Pamoja na yote hayo, Phiri anaamini kipindi hiki cha mapumziko kupisha mechi za kimataifa kimemsaidia kujifua zaidi na kuwa fiti na sasa hesabu zake ni kufunga kwenye kila mechi atakazopata nafasi.

“Majeraha yalivuruga kila kitu. Nilivyorudi sikupata muda wa kutosha kujiweka sawa kwani ligi ilikuwa inaendelea na tayari kulikuwa na cwachezaji wengine ambao walikuwa fiti zaidi hivyo hata muda wa kucheza ili kurejesha utimamu wangu ukawa mfinyu,” alisema Phiri na kuongeza;

“Muda huu wa mapumziko nimeutumia kujiweka sawa, sasa niko tayari kufunga kwenye mechi nitakazopata nafasi, najiamini na najua inawezekana hivyo mashabiki wa Simba waondoe shaka kwani nipo tayari kuwafurahisha zaidi.”

Kwa upande wa kocha mkuu wa Simba, Mbrazili, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ alisema Phiri ni mchezaji mzuri lakini majeraha yalimpunguzia kasi ila anaamini kwa sasa amerudi kwenye ubora wake na atampa nafasi katika mechi ijayo.

“Nmekuwa nikitoa nafasi kwa wachezaji wake, natambua ubora wa phiri na sasa yuko timamu nadhani atapata muda mwingi wa kucheza katika mechi zijazo na atafanya vizuri,” alisema Robertinho.

Kwa maana hiyo huenda Phiri akaanza kwenye mechi ijayo dhidi Raja ambayo ni kama ya kukamilisha ratiba kwani timu zote mbili zimeshafuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, lakini pia huenda akapata muda mwingi wa kucheza kwenye mechi za kombe la TFF (ASFC), na mechi sita za Ligi walizobakiza wababe hao wa Msimbazi kumaliza msimu.

Chanzo: Mwanaspoti