Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mechi Yanga, Simba utata

78362e6f7973a6b6bd7403283414c662 Mechi Yanga, Simbautata

Thu, 8 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imesogeza mbele mchezo wa Yanga na Simba uliokuwa uchezwe Oktoba 18, na sasa utachezwa Novemba 7, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na bodi hiyo, mabadiliko hayo yametokana na uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa vikwazo katika usafiri wa kimataifa baada ya kukamilika kwa michezo ya kimataifa iliyo kwenye kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), jambo linaloweza kuathiri vikosi vya klabu hizo mbili.

“Nchi nyingi bado zimeendelea kuweka masharti magumu katika taratibu za usafiri wa kimataifa tangu kuzuka kwa janga la corona,” ilisema taarifa hiyo.

Sababu hizo hazitoshi kuaminisha watu ndio chanzo cha kusogeza mbele mchezo huo kwani wachezaji wengi wa Simba wapo isipokuwa watatu tu, na Yanga hakuna aliyeondoka.

Pia, timu ya taifa ya Tanzania itacheza katika uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa, hivyo wachezaji wa klabu hizo walioitwa wasingepata shida ya kuungana na klabu zao baada ya mechi dhidi ya Burundi Jumapili kwa sababu hawasafiri umbali mrefu, kwani kambi itakuwa Dar es Salaam.

Hata hivyo, gazeti hili lilimtafuta Mtendaji wa bodi hiyo, Almas Kasongo kujibu maswali zaidi kuhusu taarifa hiyo, simu yake haikupatikana, lakini msemaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo alisema mabadiliko hayo hayataathiri ratiba ya Stars ya kufuzu kwa Afcon.

Msemaji wa Simba, Haji Manara alisema wanakubali mabadiliko hayo bila kinyongo chochote, ambapo timu yao Oktoba 10 na 14 itacheza mechi za kirafiki dhidi ya Pan Africans na Mlandege.

Licha ya kusogezwa hadi Novemba 7 bado kuna mkanganyiko wa ratiba, kwani Tunisia inatarajiwa kumenyana na Stars Novemba 13, mwaka huu ugenini nchini Tunisia mchezo wa kufuzu kwa Afcon.

Chanzo: habarileo.co.tz