Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mechi 11 za jasho na damu Ligi Kuu Bara

Simba Vs Yanga Mechi 11 za jasho na damu Ligi Kuu Bara

Sun, 8 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ligi Kuu imesimama kwa wiki mbili kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajiwa kuhitimishwa Januari 13, mwaka huu.

Kila timu imeshacheza michezo 19 kwa maana hiyo imebakiza michezo 11 ya kuhitimisha msimu wa 2022/2023. Kila mmoja aliyeko katika nafasi yake hana uhakika atabaki kwa pointi alizonazo pengine kuchukua taji au atashuka daraja.

Duru la mizunguko iliyobaki itakuwa ya moto, yenye presha ya kutafuta matokeo mazuri kujiweka sehemu salama kulingana na ndoto na safari ya kuelekea nchi ya matumaini.

VINARA Kuna timu tatu ziko juu zinaongoza ligi yaani, Yanga yenye pointi 50 ikiiacha Simba katika nafasi ya pili pointi 44 tofauti ya pointi sita na Azam FC katika nafasi ya tatu kwa pointi 40 tofauti ya pointi 10 dhidi ya kinara na pointi nne dhidi ya nafasi ya pili.

Yanga lazima itakuwa na presha kwa sababu ikipoteza michezo miwili tu inakuwa sawa na mtani wake wa jadi Simba.

Kasi ya Wekundu wa Msimbazi, Simba hakika inaweza kumwogopesha Yanga na hivyo, itacheza ikijua wazi kuwa ikiteleza kidogo kazi inayo, inaweza kumpisha mwenzake na safari yake ya kulitetea taji ikawa ndio mwisho.

Simba inaweza kuchukua taji na ina nafasi tena ikicheza kwa imani kwamba ipo siku mtani wake atateleza tu kwani katika michezo 11 kucheza bila kupoteza au kupata sare inaweza kuwezekana au kutowezekana.

Kasi yake kama itaendelea hivyo ina kila sababu ya kuchukua taji na takwimu zao za michezo mitano iliyopita zimekuwa bora wakishinda mechi zao kwa idadi kubwa ya mabao kiasi cha kuwaogopesha wapinzani.

Yanga imeshinda mechi tano lakini mechi zao za karibuni imekuwa ikipata matokeo ya kusuasua huku watani zao wakiwajibu kuwa sasa wamerudi rasmi na wako tayari kwa pambano.

Baadhi ya wachezaji wa Simba wakishangalia.

Simba imetoka kumfunga Tanzania Prisons mabao 7-1, kipigo ambacho ni kikubwa tangu kuanza kwa ligi.

Na zaidi usajili wa dirisha dogo waliofanya kwa kumuingiza Saido Ntibazonkiza umeonesha kuleta matunda baada ya mchezaji huyo kufunga mabao matatu na kuchangia pasi moja katika mchezo huo uliopita.

Wekundu hao licha ya kushika nafasi ya pili wanaonekana kuwa na safu nzuri ya ushambuliaji inayoongoza kwa kufunga mabao mengi kuliko timu yoyote. Imefikisha mabao 47 tofauti ya 10 dhidi ya kinara.

Kufunga idadi kubwa ya mabao kuna faida baadaye ikiwa watakuja kulingana pointi mshindi anachaguliwa kwa kuangalia idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa. Hilo linadhihirisha kuwa sasa Simba wako mawindoni na tayari kupigania taji sambamba na mtani wake Yanga.

Baadhi ya wachezaji wa Azam wakishangilia.

Kwa upande wa Azam FC walikuwa kwenye mbio vizuri walipoteleza katika baadhi ya mechi zao zilizopita wakarudi nyuma. Tofauti ya pointi 10 dhidi ya kinara ni sawa na Yanga apoteze mechi tatu kisha apate sare moja ili kwenda sambamba.

Lakini bado hawapaswi kubezwa wana kikosi kizuri na wanaweza kufanya mapinduzi ila wanahitaji kazi ya ziada kuwaondoa Yanga na mwenzake Simba katika nafasi mbili za juu ili yeye akae.

Ila nafasi ya pili na tatu Azam anaweza kuipigania kama atamwombea Simba mabaya kwa sababu wametofautiana pointi nne, hapo akiomba wekundu wapoteze michezo miwili. Jambo ambalo linaweza kuwa rahisi au gumu.

Lakini wanalambalamba hao wasipoangalia katika nafasi waliyopo wanaweza kushuka na kuwapa nafasi Singida Big Stars ambao wanakuja kwa kasi. Singida na Azam FC zimetofautiana pointi tatu ambazo ni rahisi kwa maana ya mechi moja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live