Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mechi 10 kali za derby

Mashabiki SImba K 1 1140x640 Mashabiki wa Simba ambae kesho atakuwa mwenyeji wa mchezo huo

Sat, 15 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Presha ya mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga imeanza kupanda na kushuka kwa wanachama na mashabiki wa timu hizo kongwe.

Timu hizo zenye upinzani wa aina yake kwenye soka la Tanzania, zinatarajia kupambana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea.

Timu hizo zimekutana mara nyingi kwenye Ligi Kuu na michuano tofauti. Hata hivyo kuna baadhi ya mechi ambazo hazitosahauliwa na mashabiki wa klabu hizo. Na hata kizazi kinachofuata husimuliwa na kingine kinachokuja kitakuja kusimuliwa.

Hizi ni mechi 10 za Ligi Kuu zilizowekwa kwenye rekodi ya kuwa mechi kali ambazo si rahisi kusahauliwa na mashabiki wa timu hizo. Hii ni kutokana na aina ya mechi yenyewe, matokeo na matukio yaliyotokea uwanjani

1. YANGA KUIPIGA SIMBA 5-0

Ni mechi pekee iliyokuwa kwenye rekodi ambayo Yanga iliifunga Simba magoli mengi. Mechi hiyo ilichezwa Juni Mosi mwaka 1968 jijini Dar es Salaam na Yanga kufumua Simba mabao 5-0. Hata hivyo wakati huo ilikuwa ikiitwa Sunderland. Mabao ya Yanga yalifungwa na Maulidi Dilunga na Salehe Zimbwe wakifunga magoli mawili kila mmoja, huku Kitwana Manara akifunga bao moja.

2. MECHI YA KIHISTORIA NYAMAGANA

Mechi hii imebaki kuwa na simulizi nyingi za kusadikika na kutosadikika, kutokana na matukio yaliyojitokeza. Ilichezwa Agosti 10, 1974 kwenye Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza. Katika mechi hiyo, Yanga iliifunga Simba mabao 2-1. Simba ilipata bao dakika ya 16 likifungwa na Adam Sabu.

Inasemekana kuwa tayari mashabiki wa Simba alishaanza kutunza pesa kwenye kombe la ubingwa wa ligi. Straika mwenye mashuti makali wakati huo Gibson Sembuli aliisawazishia Yanga bao dakika ya 87.

Sunday Manara (baba yake Haji Manara) aliifungia Yanga bao la pili dakika saba wa nyongeza. Hata hivyo, Simba ilimlalamikia mwamuzi marehemu Manyoto Ndimbo kuwa aliongeza dakika nyingi zaidi ya tisa ili kuibeba Yanga kwani dakika 90 zilikuwa zimemalizika. Katika mechi hiyo, historia inasema kuwa shabiki mmoja wa Simba alijitupa kwenye pipa la mafuta na kufariki dunia baada ya timu yake kufungwa.

Lakini pia mchezaji Saad Ally wa Simba alianguka chini na kuzirai, kiasi cha kukimbizwa hospitali ya Bugando. Hapo ndipo hadithi zinasema kuwa alipoangukia hakukuota tena nyasi hadi leo, ambapo kumewekwa nyasi bandia. Ndio maana wanachama na mashabiki wa timu hizo wanalichukulia kuwa lilikuwa ni pambano la kihistoria.

3. SIMBA YAILIPUA YANGA 6-0

Hii ndiyo mechi iliyoweka rekodi ya timu moja kati ya hizo kufungwa magoli mengi zaidi kwenye historia ya timu hizo. Yanga ilifungwa magoli 6-0 ambayo hadi leo hayajafungwa kwenye mechi za watani wa jadi.

Simba iliweka historia ya kuichapa mabao hayo ambayo hadi leo ndiyo rekodi ya juu zaidi. Mechi ilichezwa Julai 19, 1977 jijini Dar es Salaam. Straika wa wakati huo, Abdallah Kibadeni aliweka rekodi ambayo haijavunjwa na mchezaji yoyote wa kati ya timu hizo mbili kufunga hat-trick kwenye mechi za watani wa jadi. Alifunga mabao matatu kwenye dakika za 10, 42 na 89, Jumanne Hassan ëMasimentií akifunga mawili, moja Yanga ikijifunga yenyewe kupitia kwa beki wake Selemani Sanga.

4. SIMBA YANUSURIKA KUSHUKA DARAJA 2-1

Kipigo ilichoipa Yanga, kiliifanya Simba kubaki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara. kwenye mechi hiyo iliyochezwa Julai 23, 1988, Yanga ilihitaji sare au ushindi ili kutwaa ubingwa. Simba haikuhitaji kitu kingine zaidi ya ushindi. Baada ya Edward Chumila kuifungia Simba na Issa Athumani kuisawazishia Yanga, John Makelele ‘Zig Zag’ dakika ya 58 aliifungia Simba bao muhimu lililoibakisha kwenye ligi, Yanga ikikosa ubingwa uliokwenda kwa Coastal Union.

5. KOMBORA LA MAVUMBI OMAR

Hii ilikuwa ni Mei 26, 1990, timu hizo zilipopambana tena jijini Dar es Salaam kwenye mechi za Ligi Kuu, wakati huo ikiitwa daraja la kwanza. Simba ilishinda bao 1-0 lililofungwa mapema tu kwenye dakika ya sita na beki wa pembeni Mavumbi Omari, licha ya Yanga kukukuruka kutaka kurejesha mambo yalikwama na Mnyama akaibuka na ushindi huo wa kibabe.

6. MECHI YA MAGOLI MENGI ZAIDI

Katika historia ya Simba na Yanga, hii ndiyo mechi iliyozalisha magoli mengi zaidi kwenye mechi moja. Jumla la magoli manane yalifungwa kwenye mechi hiyo iliyochezwa Novemba 9, 1996 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, timu hizo zikifungana magoli 4-4. Yanga ilipata magoli yake kupitia kwa Edibilly Lunyamila, Mustafa Hoza wa Simba aliyejifunga, Said Mwamba ‘Kizota’ na Sanifu Lazaro ‘Tingisha’. Mabao ya Simba yalifungwa na Thomas Kipese, Ahmed Mwinyimkuu, Dua Said akifunga mawili.

7. IDDI MOSHI AIKACHA FUNGATE

Ilikuwa ni Agosti 5, 2000 Simba ilipokubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Yanga. Mechii imeingia kwenye zile ya kukumbukwa zaidi kwa sababu moja tu. Mfungaji wa magoli yote mawili alikuwa ni Idd Moshi. Alifunga magoli hayo akiwa anatoka kwenye fungate ya ndoa yake.

8. TV YAGEUKA KUWA REFA WA MECHI

Kituko kilitokea Machi 5, 2011 kwenye mechi baina ya timu hizo mbili zilipotoka sare ya bao 1-1. Mwamuzi Oden Mbaga alilikataa bao lililogonga nguzo ya juu na kudunda chini, kabla ya kurejea uwanjani. Kwa haraka haraka lilionekana kama si bao. Ndani ya Uwanja wa Taifa, TV kubwa upande wa Kaskazini mechi hiyo ilikuwa ikionyeshwa. Wachezaji wa Simba walimfuata mwamuzi na kumtaka aangalie marudio.

Na kweli. Kwenye marudio, ilionekana mpira ule ilivuka mstari wakati ukidunda chini. Mbaga alibadilisha maamuzi yake na kukubali goli hilo lililofungwa na Mussa Hassan Mgosi ambaye kwa sasa ni meneja wa timu. Ni bao pekee kwenye mechi ya watani limeingia kwenye rekodi hiyo ya kukubaliwa kwa msaada wa teknolojia. Lilikuwa la kusawazisha baada ya lile la Stephano Mwasika.

9. ZILE TANO ZA KINA OKWI

Yanga ilikubali kipigo cha mabao 5-0. Nusura Simba warudie rekodi ya mwaka 1977. Kama angepewa penalti moja tu na kufunga, Emmanuel Okwi angeweza kuifikia rekodi ya ëhat-trickí ya Kibadeni. Okwi aliwavuruga kabisa mabeki wa Yanga na kufunga magoli mawili, Mei 6, 2012. Magoli yaliyobaki yalifungwa na Patrick Mafisango, Juma Kaseja na Felix Sunzu kwa mikwaju wa penalti.

10.SARE YA KIBABE, SIMBA IKIIDUWAZA YANGA

Hadi mapumziko Simba ilikuwa nyuma kwa magoli 3-0. Kila mmoja alijua kuwa huenda ilikuwa ndiyo siku ya Yanga kurudisha yale mabao sita ya mwaka 1977, au kuvunja rekodi. Yalikuwa ni magoli mawili ya Hamisi Kiiza na moja la Mrisho Ngasa. Kibao kiligeuka. Simba ilianza kurudisha bao moja baada ya jingine. Mechi hiyo iliyokuwa kama mchezo wa kuigiza, ilichezwa Oktoba 20, 2013 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Simba ilirudisha magoli hayo kupitia kwa Betram Mombeki, William Lucian ‘Gallas’ na Joseph Owino.

Chanzo: Mwanaspoti