Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mdamu bado sana kutundika daluga

GERALD Mdamu Gerald Mdamu

Mon, 17 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Gerald Mdamu anayeendelea kujiuguza majeraha yake anasema anaona matumaini makubwa msimu ujao kurejea uwanjani.

Nyota huyo wa zamani wa Mwadui, alisema kwa sasa hatumii tena magongo na chuma zote zilizokuwa miguuni mwake zimetolewa na anafanya mazoezi ya kutembea mwenyewe.

“Kwa sasa nina mwezi tangu niache kutumia magongo, kikubwa namshukuru Mungu kwa maendeleo makubwa ninayoyaona juu ya afya yangu tangu tulipopata ajali.

“Mguu wa kulia ndio naona unahitaji matibabu zaidi japo sio kama awali ni vitu vidogovidogo vya kuzingatia, hivyo nina uhakika hadi msimu ujao afya itakuwa imeimarika zaidi na ninaweza kurejea uwanjani kama awali,” alisema Mdamu.

Aliongeza kwa kuwashukuru mabosi wake wa Polisi kwa kuendelea kumsapoti kwani anapokea mshahara wake kama ilivyokuwa mwanzo alivyokuwa anacheza.

Julai 9 mwaka jana itabaki kwenye kumbukumbu ya maisha ya Mdamu wakati kikosi cha Polisi kilipopata ajali wakiwa wanatoka mazoezini katika Uwanja wa TPC, Moshi wakijiandaa na mechi za mwishi za Ligi Kuu Bara.

Katika ajali hiyo, Mdamu alivunjika miguu yote miwili na kuwahishwa Hospitali ya KCMC kwa ajili ya matibabu zaidi na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Mdamu amewahi kuzichezea timu kadhaa za Ligi Kuu kabla ya kujiunga na Polisi, ikiwemo Mwadui Kagera Sugar na Biashara United.

Mwaka 2016 ndio aliibuliwa na Mwadui baada ya kung’ara kwenye michuano ya Ndondo Cup akikipiga timu ya Tabata United na kulimsha kwenye timu ya vijana kabla ya kupanda timu ya wakubwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live