Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mcolombia Azam amkosha Dabo

Franklin Navarro Azam Mcolombia Azam amkosha Dabo

Tue, 2 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na mshambuliaji mpya wa timu hiyo raia wa Colombia, Franklin Navarro katika mchezo wake wa kwanza juzi kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Chipukizi.

Nyota huyo aliyesajiliwa dirisha hili dogo la usajili akitokea klabu ya Cortulua inayoshiriki Ligi daraja la pili huko kwao Colombia aliingia dakika ya 75 ya mchezo huo ulioisha kwa Azam kushinda bao 1-0, akichukua nafasi ya Kipre Junior.

Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Zanzibar, Dabo alisema Navarro anahitaji muda wa kuzoeana na wachezaji wenzake ndani ya timu hiyo.

"Licha ya kucheza dakika chache ila ameonyesha kiwango kizuri na ni mchezaji ambaye ni tumaini jipya hapa kikosini, hii michuano ya Mapinduzi ni muhimu kwake kupata muda mwingi wa kuzoeana na wenzake hivyo sina shaka naye kabisa," alisema.

Akizungumzia kiwango cha timu nzima kijumla katika michuano hiyo, Dabo alisema bado hajaridhishwa kwa asilimia 100 ila kadri ambavyo wanazidi kucheza wanazidi kujenga hali ya kujiamini kutokana na baadhi yao kuendelea na majukumu mengine.

"Kama tunavyojua wengine wako kwenye majukumu ya timu zao za Taifa hivyo tunapambana kadri ya uwezo wetu na wale waliopo hapa, michuano imeanza kwa ushindani mkubwa ingawa tutapambana ili kutimiza azma yetu ya kulitwaa taji hili," alisema.

Katia mchezo huo wa juzi usiku Azam ilipata bao la ushindi kupitia Alassane Diao aliyefunga dakika ya 12 na kuifanya timu hiyo ikae kileleni mwa Kundi A ikifikisha pointi nne baada ya mechi mbili ikifuatiwa na Mlandege na Vital'O ya Burundi zenye pointi mbili kila mmoja na Chipukizi ikishika mkia na pointi moja.

Chanzo: Mwanaspoti