Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mchoro wa ubingwa wa Uefa kwa Masaka

Aisha Masaka Aisha Masaka

Mon, 19 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

BK Hacken FF anayoichezea nyota wa kimataifa kutoka Tanzania, Aisha Masaka huko Sweden, inasaka rekodi mpya na tamu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa upande wa soka la Wanawake ambayo imefika katika hatua ya robo fainali.

Masaka na wachezaji wenzake wana kibarua kizito mbele yao dhidi ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa, ambacho ni kuhakikisha BK Hacken FF inatinga nusu fainali ya michuano hiyo, wakifanikiwa hilo watakuwa wameweka rekodi mpya kwani tangu kuanzishwa kwa timu hiyo miaka 54 iliyopita hawajawahi kufika hatua hiyo.

Msimu wa 2011–2012 na 2012–2013, BK Hacken FF iliishia katika hatua ya robo fainali kwa kuondolewa dhidi ya Arsenal ya England kwa jumla ya mabao 3-2 na awamu nyingine ikaangukia pua dhidi ya Juvisy ya Italia kwa jumla ya mabao 4-1.

Hiyo ilikuwa misimu yao ya kwanza kwenye michuano hiyo na tangu hapo walishindwa kutamba kwa kufika katika hatua hiyo hadi msimu huu wa 2023–24 ambapo wanaonekana kuwa tishio kiasi cha kutajwa kuwa kati ya timu ambazo zinaweza kubeba ubingwa wa michuano hiyo kutokana na kiwango walichoonyesha kuanzia katika hatua za awali hadi makundi ambapo walipangwa na vigogo.

Ikiwa kundi moja (D) na Chelsea, Paris FC ya Ufaransa pamoja na Real Madrid ya Hispania, BK Hacken FF ilipenya kwa kushika nafasi ya pili baada ya kujikusanyia pointi 11, ilizidiwa pointi tatu tu na Chelsea iliyoongoza msimamo.

Kumaliza kwa chama hilo la Masaka katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi D kumewafanya wawakilishi hao wa Sweden kupangwa katika hatua ya robo fainali kucheza dhidi ya kinara wa kundi C ambaye ni Paris Saint-Germain aliyeoongoza kundi hilo mbele ya Ajax, Bayern Munich na Roma.

Kuwa kundi moja kwa BK Hacken FF na Paris FC kumetajwa kuwa inaweza kuwa faida kwa chama la Masaka katika michezo yao wa robo fainali (nyumbani na ugenini) ambayo itachezwa mwezi ujao wa Machi dhidi ya Paris Saint-Germain kwani walipata changamoto ya kiushindani kutoka kwa timu za Kifaransa.

BK Hacken FF ilivuna pointi nne dhidi ya Paris FC kwa kutoa sare nyumbani na kuwatandika huko kwao wababe hao wa soka la Ufaransa kwa mabao 2-1, hivyo kina Masaka na wenzake wanaweza kuwa na nafasi nzuri ya kufanya vizuri dhidi ya Paris Saint-Germain.

Kama watavuka katika hatua hiyo, kibarua kizito kinaonekana kwenye hatua ya nusu fainali ambayo watacheza na mashindi kati ya Benfica ya Ureno au Lyon ambao nao ni wababe wengine kwenye soka la wanawake Ulaya wakitokea Ufaransa.

Akiongelea kuwa kwao katika hatua ya robo fainali, Masaka alisema kilichowabeba ilikuwa ni ubora wa kikosi chao na kucheza kama timu kuanzia kwenye hatua za awadi hadi makundi na sasa shabaha yao ni kufanya vizuri kwenye michezo ya robo fainali ambayo alikiri itakuwa migumu.

“Tutaanzia nyumbani, ambacho ni muhimu kwetu ni kufanya vizuri ili tuwe kwenye nafasi nzuri ya kwenda nusu,” anasema Masaka ambaye anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kike kutoka Tanzania kucheza michuano hiyo. Wakati shughuli ikiwa hivyo kwa upande wa Masaka na njia yake hadi nusu fainali huko kwingine Brann ya Norway itacheza dhidi ya Barcelona na Ajax itapepetana na Chelsea mshindi wa jumla kati yao atasonga mbele. Nusu fainali ya upande huu itakuwa kati ya Brann/Barcelona dhidi ya Ajax/Chelsea.

BK Hacken FF ambayo juzi, Jumamosi ilikuwa ikijipima ubavu na Djurgarden, ina michezo miwili mbele yake ya Kombe la Svenska ambayo ni dhidi ya Vaxjo DFF na Lidkoping kabla ya kuikaribisha Paris Saint-Germain kwenye uwanja wao wa nyumbani kwa ajili ya mchezo wa robo fainali ya kwanza.

WASIKIE WADAU Wadau wa nje ya Bongo ambao wapo Sweden kwa shughuli za utafutaji, Frank Samwel na Johnson Michael wameeleza namna ambavyo timu hiyo inasapotiwa nchini humo ili kuleta heshima ambayo ilipotea kwa miaka mingi.

Samweli ambaye ni daktari anasema, “Mwenendo wa timu ni mzuri na Wasweden wanafurahia kile ambacho wanafanya, nimepata nafasi ya kuwashuhudia mara mbili wakicheza na mechi zote walishinda, wanaweza kushindana na ndio wamefika hatua hiyo sio timu ya kubahatisha lakini wanatakiwa kuongeza juhudi kwa sababu hatua waliyofika ni ngumu zaidi ukilinganisha na walipotoka.”

Kwa upande wake Johnson ambaye ni mfanyabiashara alisema kikwazo ambacho anakiona kwa BK Hacken FF ni katika nusu fainali.

“Naamini kuwa wanavuka robo fainali kwa sababu PSG ni timu ngeni kwenye soka la wanawake, sisi tuna uzoefu zaidi yao ni ngumu kutulinganisha nao, wao wana fedha lakini sisi tuna soka na wachezaji wengi wenye vipaji, tunaweza kuwafunga nyumbani na ugenini,” anasema mdau huyo.

Chanzo: Mwanaspoti