Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mchongo mzima Ligue 1 ulikuwa hivi

PSG Ligue 1 France.jpeg Mchongo mzima Ligue 1 ulikuwa hivi

Mon, 20 May 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1) ilimalizika wikiendi iliyopita ambapo ubishi wote ulimaliza juu ya nani atakuwepo msimu ujao na nani atacheza michuano gani ya kimataifa.

Kama kawaida PSG ndio ilikuwa mabingwa ukiwa ni ubingwa wake wa 12 ambao pia ulikuwa wa tatu mfululizo tangu msimu wa 2021-22.

Clermont na Lorient zilishuka daraja moja kwa moja wakati Nantes ikiwa inasubiri kucheza mechi ya mtoano dhidi ya timu moja kutoka Ligi Daraja la Kwanza ili kujua hatima yake ikiwa itabaki au itaondoka.

Kwa upande wake, Lens ilifanikiwa kufuzu kucheza michuano ya Uefa Conference League, Nice na Olympique Lyon zimefuzu Europa League wakati Monaco na Brest zikiungana na PSG kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa pamoja na Lille iliyomaliza nafasi ya tano lakini itatakiwa kucheza kwanza hatua za awali kabla ya kuingia makundi.

Takwimu zinaonyesha Marseille ndio timu iliyoachana na makocha wengi kwa msimu uliomalizika ikianzia na Igor Tudor aliyejiuzuru mwenyewe wakati timu ikiwa katika maandalizi ya msimu, Juni 1, 2023, kisha akafuata Marcelino Septemba 20,2023 na baadaye Gennaro Gattuso, Februari, mwaka huu.

Tuzo ya mfungaji bora ilikwenda kwa Kylian Mbappe wa PSG aliyefunga mabao 27 katika mechi 29 za Ligue 1 ambaye pia aliongoza kwa kufunga hat-trick akifanya hivyo mara mbili.

Kipa wa Nice, Marcin Bulka aliongoza kwa kucheza mechi nyingi bila kuruhusu bao akifanya hivyo katika mechi 17, lakini tuzo ya kipa bora alipewa Gianluig Donnarumma wa PSG.

Wachezaji Facundo Medina wa Lens, Pierre Lees-Melou (Brest) na Denis Zakaria (Monaco) waliongoza kwa kadi nyingi za njano ambapo kila mmoja ameonyeshwa mara 11.

Vilevile Brest ndiyo timu ambayo wachezaji wengi wameonyeshwa kadi za njano ambapo kwa ujumla zinafika 80, wakati Monaco inaongoza kwa kuwa na wachezaji wengi walioonyeshwa kadi nyekundu ambapo ni nane.

Mchezaji bora wa msimu ni Mbappe wa PSG, kinda bora ni Warren Zaïre-Emery ambaye pia anatokea PSG huku kocha bora ni Eric Roy anayekinoa kikosi cha Brest.

Chanzo: Mwanaspoti