Wakati Simba ikipiga hesabu kali za kuhakikisha wanatinga hatua ya Robo Fainali Michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
Tayari wameingia kambini kujiandaa na mchezo huo baada tu ya ushindi wao wa jana dhidi ya African Sports ya Tanga mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam hatua ya 16 bora ambapo waliibuka na ushindi wa bao 4-0.
Akizungumza leo katika mkutano na Waandishi wa Habari, Meneja wa Mawasiliano wa Klabu ya Simba Ahmed Ally amethibitisha;
"Kikosi kimeingia kambini leo baada ya mchezo wa jana wa ASFC, na leo jioni kikosi kitaanza mazoezi. Bado siku tano kabla ya mchezo dhidi ya Vipers, tumeingia kambini kwa umuhimu wa mchezo wenyewe, tunauhitaji kwelikweli."
"Tulikwenda kufufukia Uganda, na kweli tumefufuka. Jumanne ni mechi ya marudio katika mechi hii tunakwenda kuamua hatma ya Simba kwenye michuano ya CAF. Tukimpiga tutafikisha alama 6 na kuanza kuchungulia robo fainali."
"Hatupo tayari kuishia hatua ya makundi. Tulikwenda kuchukua alama tatu kwa Vipers lakini hatujamaliza, tunakwenda kuzichukua alama zingine hapa nyumbani. Niseme tu tuko tayari kwa mchezo."
Mechi dhidi ya Vipers itakuwa Jumanne Machi 7, 2023 saa 1:00 usiku katika Uwanja wa Benjamini Mkapa.