Ilitokea kule Zanzibar pale Azam FC ilipomtambulisha Franklin Navarro kwenye dirisha dogo. Mchezaji huyo aliikataa jezi aliyotambulishwa nayo na ikabidi abadilishiwe haraka sana.
Na sasa imetokea tena hapa Benslimane, Morocco ambako nyota katika usajili mpya wa matajiri wa Chamazi amekataa namba ya jezi iliyoandaliwa kwa ajili yake.
Nyota huyo ni Mamadou Samake ambaye alipewa namba 13, namba ambayo dunia nzima huiona kama yenye mikosi.
Kule Zanzibar, Mcolombia Navarro aliikataa namba hiyo na kupewa samba 8 ambayo ameitumia kwa muda mrefu hadi sasa alipochukua namba 10. Na Samake ambaye ametambulishwa hivi karibuni na kupewa namba hiyo, ameikataa kwa hofu zile zile za Navarro, mikosi.
Taarifa za ndani kutoka kambini hapa zinasema Samake amewapasua vichwa viongozi wa klabu hiyo kumtafutia namba nyingine kwa sababu zote zina watu. Suluhisho pekee lililopo sasa ni kumvua namba mmoja kati ya majeruhi wa muda mrefu ambao hawamo mwenye usajili.
Wachezaji hao ni Alassane Diao anayevaa namba 11 na Franklin Navarro aliyehamia namba 10 kutoka namba 8 ambayo sasa inavaliwa na Cheickna Diakite. Samake anaitaka namba 8 ambayo ni sahihi zaidi kwa kiungo kama yeye, na Diakite anaitaka namba 10 au 11 ambazo zinafanana na mchezaji mwenye kariba kama yake.
MKOSI WA JEZI NAMBA 13 Kwa mujibu wa taasisi ya utafiti ya Stress Management Center and Phobia Institute ya Asheville, North Carolina, Marekani, zaidi ya asilimia 80 ya majengo marefu nchini humo hayana ghorofa ya 13, na hoteli nyingi, hospitali na hata viwanja vya ndege hukwepa kutumia namba 13 kwenye vyumba na mageti.
Ubaya wa namba 13 unatokana na uzuri wa namba 12. Kwa tamaduni za kımagharibi, namba 12 inahusishwa bahati na ukamilifu, ndiyo maana kuna siku 12 za Krismasi. Kuna miezi 12 katika mwaka na kuna alama za unajimu yaani utabiri wa nyota.
Siku yenye saa 24 imegawanywa mara mbili katika vipindi vya saa 12 kila kimoja. Kuna miungu 12 wa Olympus (Kigiriki) na kuna makabila 12 ya Israel.
Kwa kifupi namba 12 ni ya baraka zote katika imani hizo. Namba inayofuata baada ya hapo ni 13 ambayo inakuja ikikuta baraka na bahati zote zimeshachukuliwa na namba 12…ikaishia kuchukua mikosi tu. Hii ni sawa na hadithi ya biblia ya watoto mapacha wa Isaka; Essau (kulwa) na Yakubu (doto).
Kulwa Essau alipoondoka, doto Yakubu akapata baraka na bahati zote, Essau aliporudi akachukua vilivyobaki ambavyo vilikuwa mikosi na bahati mbaya. Kwa hiyo namba 13 imechukua mabaya yote, mikosi yote na bahati mbaya zote.
Mfalme wa zamani wa Mesopotamia, Hammurabi, aliiondoa sheria namba 13 katika sheria zake maarufu zinazoitwa Code of Hammurabi yaani sheria za Hammurabi. Hii ni moja ya ushahidi mkuu wanaoutumia watu wote wajaoihofia namba 13 kuwa ya mikosi.
Hamuurabi aliiongoza Mesopotamia kati ya mwaka 1792 hadi mwaka 1750 kabla ya kuzaliwa Kristu. Mesopotamia kwa sasa ndiyo nchi ya Iraq. Sheria za Hammurabi ndiyo sheria za kwanza kabisa kuandikwa kwa ukamilifu wa hali ya juu duniani katika historia ya sheria.
Katika muendelezo wa ubaya wa namba 13, Magharibi kuna nadharia inaitwa Friday the 13th yaani Ijumaa ya 13. Nadharia hii inatokana na simulizi ya kibiblia ya kwenye karamu ya mwisho ya Alhamisi Kuu.
Watu 13 walihudhuria karamu hiyo, akiwemo Yesu na mitume wake 12 mmojawao akiwa Yuda ambaye baadaye alimsaliti. Siku iliyofuata ilikuwa Ijumaa Kuu, siku ambayo Yesu alisulubiwa. Mpangilio wao mezani kwenye ile karamu ukasababisha watu waogope kukaa 13 wakati wa kula.
Franklin Navarro anatokea Colombia, nchi ya Kilatini yenye utamaduni wa kimagharibi. Mambo yote haya wapo watu wanaoyajua na kuyafuata na kuyaamini. Navarro yawezekana kuna mambo yalimtokea na kuogopa moja kwa moja kuhusishwa na Namba 13.
WACHEZAJI NA NAMBA Mikasa ya namba za jezi kwa wachezaji imekuwa ikitokea kwa miaka mingi, kwa vyanzo tofauti. Wachezaji mbalimbali wamekuwa wakivaa jezi za namba kutokana na imani fulani, historia fulani au siri fulani.
Kalidou Koulibally na namba 26 Nahodha wa timu ya taifa ya Senegal, Kalidou Koulibally, amekuwa akivaa jezi namba 26 katika klabu anazochezea. Hii ni kwa sababu ya kufurahia maisha yake ya uhusiano na mpenzi wake, Charline Oudenot.
Koulibaly na mpenzi wake wanafanana siku zao za kuzaliwa, japo ni miaka tofauti. Wote wamezaliwa tarehe 20 mwezi wa 6 ndiyo maana ya 26 yaani 20+6. Akiwa Napoli, aliivaa namba hii kwa misimu minane, tangu ajiunge nayo mwaka 2014 hadi alipoondoka 2022.
Na hata alipohamia Chelsea aliikuta namba hiyo haitumiki kwa heshima ya nahodha John Terry. Koulibally akamuomba Terry amruhusu kuitumia. Terry akakubali na Koulibally akaivaa.
Phil Foden na namba 47 Nyota wa Manchester City na England, Phil Foden, anavaa jezi namba 47 klabuni kwake. Foden aliichagua namba hii kama kumbukumbu kwa bibi yake ambaye alifariki akiwa na miaka 47.
Bruno Guimeras na namba 39 Nyota huyu wa Newcastle United na timu ya taifa ya Brazil, anavaa jezi namba 39 klabuni kwake kama heshima kwa baba yake mzazi ambaye alikuwa dereva wa taksi yenye namba hiyo.